Thursday, May 24, 2012

KWA NINI NCHI ZA ASIA MASHARIKI AU ASIA MASHARIKI YA MBALI ZIMETUPITA KI-MAENDELEO?

Na Africar T Kagema
Huu ni wakati muafaka; tunahitaji kufundishana juu ya nchi hizo za Asia Mashariki na ya Mbali (au mojawapo tu) zilizotuacha nyuma, ki-maendeleo.
Kusudi la makala haya ni kujaribu kukidhi haja ya kujaza ombwe linalozidi kuongezeka kutokana na makelele mengi ya kujilinganisha na nchi za Asia Mashariki na ya Mbali (au mojawapo ya nchi hizo) nikizingatia, kwa ujumla, vigezo au viungo-tosheleza vingine (zaidi ya elimu) katika mapishi yaliyokwamua nchi za Indonesia, Malaysia na Singapore na kuiacha Tanzania nyuma.

Tukizidi kujaliwa, nitachangia kwa kina mfano wa Kisiwa cha Singapore (Zanzibar ni kubwa) katika kujaribu kuelewa kwa nini Singapore imetuacha nyuma.
Macho … Asia Mashariki na ya Mbali, Elekeza!
Uduni wa elimu nchini Tanzania umezalisha umbumbumbu wa kutojua Kiingereza miongoni mwa vijana wetu kiasi cha kuathiri ajira kwao; hususan katika hoteli za utalii huko Kasikazini ya Tanzania.

Zaidi, uduni huo umezalisha umasikini mkubwa kiasi cha nchi yetu kuachwa nyuma sana na baadhi ya nchi zilizolingana kwa umaskini (na zilizojitawala wakati karibu mmoja) na Tanzania, yaani, Indonesia, Malaysia na Singapore. Leo hii zinatengeneza magari na makomputa na zinaingia kundi la nchi zilizoendelea.
Rais Benjamin W. Mkapa (wakati anaanza u-Rais) katika mkutano wake na wa-Tanzania nyumbani kwa Balozi Daudi N. Mwakawago (sasa marehemu) katika Mt. Vernon, New York, alishauri wa-Tanzania wageuze macho yao kuelekea huko Asia Mashariki na kuiga mifano ya ‘tigers’ hao katika jitihada za kuharakisha maendelo ya Tanzania.

Tanzania tayari imeiga baadhi ya mikwamuo ya nchi hizo. Miradi ya ujenzi wa viwanda vya ‘Special Economic Zones (SEZ)’ au ‘Special Export Processing Zones’ katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mtwara, Mwanza, Pwani, Shinyanga na Tanga ni mifano ya kutekeleza lengo la ‘Tanzania Mini-Tiger 2020’, kama ulivyo mfano wa sehemu ya Benjamin William Mkapa Special Economic Zone (BWM-SEZ), Mabibo, Dar es Salaam.
Matokeo-dhamiriwa (anticipatory results) ya ‘Special Economic Zones (SEZ)’ au ‘Special Export Processing Zones’ ni pamoja na kuongeza mauzo nje (utajiri), ajira na kumaliza umasikini (pengine, isomeke, kupunguza; sio rahisi kumaliza umasikini) ili kufikia lengo la ‘maisha bora’.

Ndoto ya kutaka kuiga nchi za Asia Mashariki pia imewakumba baadhi ya wana-siasa wa-Zanzibari wenye kutaka kuiondoa Zanzibar kutoka mabano ya uchumi wa Muungano na kuiendeleza, mithili ya Hong Kong, Dubai ama Singapore. Kwa mfano, katika hotuba ya Maridhiano na Mustakbali wa Zanzibar, 2010, mwana-siasa Seif Hamadi Shariff (Katibu Mkuu – CUF) anasikika na/au anasomeka (kwa kifupi) kuifanya Zanzibar kuwa ni Hong Kong ya Afrika:

“Binafsi naamini kuwa sasa ile ndoto yetu ya muda mrefu ya kuifanya Zanzibar kuwa ni Hong Kong ya Afrika Mashariki itaweza kutimia ndani ya muda mfupi kabisa. Naamini Wazanzibari wote… kuikwamua Zanzibar katika umasikini ambao hauna sababu ya kuwepo…Zanzibar ina utajiri mkubwa…inaweza kurudia nafasi yake ya kuwa kituo kikuu cha biashara na harakati za uchumi katika Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi… itakuwa johari na siyo tena jeraha katika Afrika…Tusiruhusu kidudu mtu yeyote akaingia kati kuturudisha kule tulikotoka.” – (rejea: hakinaumma.wordpress.com/2010/01/23/maridhiano-na-mustakbali-wa-zanzibar/
Sio tu wana-siasa wetu wanaoota kuiga hayo ya maajabu ya kujikwamua kwa nchi za Asia Mashariki na ya Mbali. Wengi wetu pia tumepiga makelele sana (na miangwi yake imeenea milimani, mabondeni na kwenye tambarare za nchi yetu) kuitaka Tanzania yetu iendelee, kama nchi hizo (au mojawapo).

Kutokana na sababu sita hivi kubwa, naunga kwa mkono upande ujenzi wa ‘Special Economic Zones (SEZ)’ au ‘Special Export Processing Zones (SEPZ) zenye madhumuni ya kuifanyaTanzania yetu ijulikane kama ‘Tanzania Mini-Tiger 2020’:
Mosi, nachelea kidogo kutumia jina la ‘mini-tiger’ kwa Tanzania ya mwaka 2020; hatuna ‘tiger’ Tanzania! Badala yake ninapendekeza kuiita kwa kutumia msamiati wa ‘cheetah’ – mnyama wetu mwenye spidi kali! Tanzania ianze kama ‘a cheetah cub’ na itakapotimia umri wa kujikwamua hasa, iitwe, ‘a cheetah economy’. Pendekezo hili linahusu pia kila nchi za Afrika Mashariki-tegemewa itakayojikwamua; zote kwa pamoja ziitwe, ‘cheetah economies’.

Pili, hizi ‘Special Economic Zones (SEZ)’ au ‘Special Export Processing Zones (SEPZ)’ zenye kuwapa misahaha mingi tu ya kodi na kadhalika wawekezaji wa nje zinapunguza kodi ya mapato sana. Tatizo la upungufu wa kodi ya mapato lilibainika mbele ya Taasisi ya Fedha ya ki-Mataifa (IMF) – rejea: english.peopledaily.com.cn/200604/12/eng20060412_257859.html/
Tatu, viwanda vingine vinalazimika kutumia malighafi za nje, kama yalivyo baadhi ya masharti ya AGOA ya Amerika kwa Afrika kuhusu biashara ya nguo na kadhalika; tunabakia ni washonaji tu.

Nne, ndio viwanda vya namna hii vinaongeza ajira. Lakini vinatumikisha wafanyakazi wake mithili ya punda. Rejea, malalamiko ya wafanyakazi huko Fort Hall, Kenya, na soma baadaye Addidas na makampuni mengine ya huko Asia Mashariki na ya Mbali.

Tano, wawekezaji ni wa nje au wanatafuta waendeshaji kutoka nchi ambazo zina ujuzi zaidi ya wa-Tanzania. Kwa mfano, viwanda vingi vya ushonaji vinaajiri waendeshaji kutoka huko Asia Mashariki. Wawekezaji wakiisha kuchuma, huhama wakati mwingine bila ya kutoa ‘transfer of technology’ kwa wazawa (kama wazawa watakuwepo tayari), kama walivyofanya huko Thailand.
Sita, wakati mwingine kuhama au kukunja virago kunatokana na ufisadi wa wakubwa wazawa kudai % zao kabla ya kuwakubalia kuendelea upya na mikataba ya kuwekeza!

Tunapenda sana kuipima Tanzania yetu kwenye mizani moja na nchi za Asia Mashariki na ya Mbali; Tanzania inaonekana inapungua. Wakati mwingine tunaipima na nchi nyingine za Afrika, kwa mifano, Mauritius na Botswana, na kuonekana kuwa inapungua, pia.
Hivi karibuni, wa-Tanzania wengine wameanza kubaini kuwa nchi ya ujirani mwema ya Rwanda huenda nayo ikajikwamua na kuiacha Tanzania yetu mataani! Pengine, inabidi tujifunze kutoka Rwanda ya ujirani mwema!

Kwamba elimu inachangia katika kuleta maendeleo ya watu na vitu ni suala lisilo na malumbano. Lakini hakuna uwiano wa moja kwa moja baina ya elimu na maendeleo. Kwa kuwa kuna wasomi, kwahiyo kuna maendeleo!
Kwa mfano, miaka ya muongo wa 1980 sehemu moja ya Ukanda wa Ziwa Victoria, Afrika Mashariki (kwa wa-Jaluo wa Kenya) iliongoza kwa wasomi wengi wenye PhD kutoka vyuo vikuu vya Afrika na nchi za nje kwa kila maili mraba Kusini mwa Sahara. (Nafikiri mpaka leo hiyo sehemu bado inaongoza.) Lakini sehemu hiyo haikuongoza kwa maendeleo katika Bara la Afrika.

Tasnifu (thesis) ya makala haya inazingatia kuwa elimu ina mchango wa lazima (necessary) lakini si wa kutosheleza (not sufficient) katika kukwamua nchi kutoka dimbwi la umasikini; kuna viungo vingine tosheleza katika hayo mapishi-kwamuzi.
Inafaa tutoe elimu bora ili kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu na kushindana katika ulimwengu wa usasa, ikiwa ni pamoja, pengine, na kufanikisha hayo ya ndoto ya ‘maisha bora’. Lakini itabidi tuangalie pia viungo vingine tosheleza katika mapishi-kwamuzi ya nchi yetu.

Tanzania inahimizwa kuelekeza macho yake huko Asia Mashariki na ya Mbali. Kwa nini? Kwa sababu nchi hizo zimepiga eti hatua kubwa za maendeleo. Ndio. Lakini maendeleo hayo yametokana si kwa kuwekeza katika elimu bora tu; yameungwa zaidi na siasa/sera nyinginezo, kama ifuatavyo:
Nchi hizo zilifanikiwa kujikwamua kwa sababu ya mikakati na michakato ya hali halisi ya kila nchi (domestic starters), kwa upande mmoja, na jinsi zilivyosaidiwa na hali halisi ya kutoka nje (external starters), kwa upande mwingine.

Nchi hizo zilitawaliwa na u-dikiteta wa/na chama kimoja na kupaliliwa na nchi za ki-bepari za Ulaya Magharibi na Amerika ili kudhibiti u-Komunisti; serikali zake ziliongoza dira ya maendeleo; mikakati ya ubia wa ‘partnerships’ na ‘transfer of appropriate technologies’ kati ya nchi hizo na nchi tajiri za Ulaya Magharibi na Amerika; zilifuata siasa na sera za kujitegemea (self-reliance policies); hata biashara ya makasino, kamari, umalaya, na madawa ya kulevya yalichangia; ubia wa wawekezaji wazawa na makampuni ya nje uliwanyonya wafanyakazi katika viwanda vya ‘sweatshirts’ (ushonaji): zalisha nafuu lakini uza ghali; na kila mmoja alihimizwa kuchapa kazi.
Baadhi ya siri za ndani (domestic starters) na za nje (external starters) ‘zinatisha’ mbele ya Tanzania yenye kuamini demokrasia na mfumo wa vyama vingi vya siasa na yenye kulilia maadili mazuri dhidi ya ufisadi; biashara ya makasino, kamari, umalaya na madawa ya kulevya; u-dikiteta/chama kimoja cha siasa.

Nchi za Asia Mashariki na ya Mbali zote hazikulingana au hazikufuata mfumo sawa wa maendeleo. Kuna nchi zilizoitwa, ‘four tigers kwanza (Japani, Korea Kusini, Hong Kong na Singapore); zilizoitwa, ‘emerging tigers’ (Indonesia, Malaysia na Thailand); na iliyokuwa inajaribu, ikaitwa, ‘entigerment’ (Philippines).
Asia Mashariki kwanza zilipendelewa na nchi tajiri na ma-benki ya Amerika, baadhi ya Nchi za Ulaya Magharibi pamoja na Benki Kuu ya Dunia na Taasisi ya Fedha ya ki-Mataifa (International Monetary Fund). Kati ya mwaka 1965 na 1990 Benki Kuu ya Dunia ilianza kuyaita mafanikio ya nchi hizo, ‘East Asian Miracle’.

Uingereza ikawa ya kwanza kuzibatiza nchi nne za Asia Mashariki kwa jina la ‘Asian Tigers’: Hong Kong, Korea Kusini, Singapore na Taiwan. Ma-bepari wa London mwaka 1995 (wakiongozwa na Waziri wa Fedha wa Uingereza Sir Kenneth Clarke na Makamu wa Rais wa Nchi za Ulaya Sir Leon Brittan) walipanga mkakati wa kuhamasisha mfumo-kusudiwa kwa nchi hizo.
Mabepari hao mwaka 1996 walifanikiwa kumpata mweza wao Waziri Mkuu wa Singapore Goh Chok Tong (aliyemfuata Lee Kuan Yew Waziri Mkuu tangu uhuru) katika kuzindua mfumo-kusudiwa.

‘Emerging tigers” za Indonesia na Malaysia zilianza na ajira katika kilimo, kama Thailand pamoja na hiyo ya ‘entigered” (Philippines), ambayo ilianza kujikwamua wakati wa utawala wa Rais Fidel Ramos ikifadhiliwa na Amerika.
Mbali ya Indonesia, Malaysia na Singapore kuelea juu ya utajiri wa mafuta na gesi, faida yake iliendeleza sera za kujikwamua kati ya mwaka 1985-86. Singapore pia ni kisiwa kidogo sana (City State) ina bandari-ghala (entrĂªport) na uwanja wa ndege maarufu duniani kwa ajili ya biashara kubwa zinazopita mlango-bahari wa Malacca (sawa na Gibraltar, Istanbul na Panama) kati ya Bahari za Hindi na Pasifiki.

Kudhibiti Biashara Haramu na Tabia Zake
Biashara kubwa ya huko Asia Mashariki ya Mbali ilikuwa ya haramu (the illegal ‘black” economy) yenye faida kubwa: u-malaya, madawa ya kulevya, riba ya uajiri (labor export brokerage fees), magendo ya silaha, wizi wa mafuta, kamari, ma-kasino, bahati nasibu za njia za panya na kupiga kamari mipirani.
Kwa mifano, Singapore na Hongkong zilijengeka kama masoko makubwa ya kikoloni ya ki-fedha na dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya chini ya China; ‘kufua fedha’ (money laundering): umalaya uliingiza mapato ya $17.7-20 bilioni; madawa ya kulevya $3.9 bilioni; riba ya uajiri (labor export brokerage fees) $2.4-3.2 bilioni; magendo ya silaha kati ya $512 milioni na $2.4 bilioni; wizi wa mafuta $334 bilioni; na kamari (ma-kasino, bahati nasibu za njia za panya na kupiga kamari mipirani $17.71-53.21 bilioni.

Malaysia ilijiepusha na balaa la kuanguka kwa uchumi kwa kufungua uchumi wa ma-kasino huko Labuan Island, mwaka 1990 ili kushindana na Hong Kong katika ‘money laundering’. Hata hivyo, ilipoteza $10 bilioni katika kumshinda ‘mega-speculator George Soros’.
Zaidi, Malayasia ilizidi kujenga ‘casino economy’ kwa kuwekeza huko Kambodia kwenye ma-kasino ya Sihanoukville, mabarabara, viwanja vya ndege na nishati. Shirika la Ekran lilijenga ma-kasino ya ‘offshore’ huko Davao.

Philippines mwaka 1995 ilifuata mkumbo wa Malaysia na kuwekeza katika Kisiwa cha Mindanao – kufuatia muafaka na wa-Islamu baada ya vita miaka zaidi ya 20. Philippines ilizindua mafao ya wafanyakazi, reli, nishati, bandari na viwanja vya ndege, na kufungulia wawekezaji ikiwa na kurejesha ugenini faida yote ya ‘joint-ventures’.
Baada ya Hong Kong kurudishwa kwa wa-China, wawekezaji walitoka Hong Kong) na kuwekeza huko Phillipines – kwa kaulimbiu, The Hongkongization of the Philippines. Leo hii kasino kubwa ni ile iliyojengwa kwenye uwanja wa zamani wa ndege za ki-vita wa Amerika, Clark Field, (the Las Vegas of Asia) pamoja na viwanja vitano vya ma-kasino-tamasha ya Disney.

Ubia: Serikali/Sekta Binafsi
Siri nyingine zilitokana na serikali kuwekeza katika elimu bora na tosheleza kukidhi ajira na kuuzika kwa wabunifu mbele ya wawekezaji wa ndani (domestic entrepreneus); uzalendo wa kuchapakazi, mishahara bila matabaka na akiba.

Serikali zilifuata na zilidumisha sera zenye tija (pragmatism) kwa nchi na kukubali kuoanisha sera hizo kwa mahitaji ya nchi (eclecticism); mishahara ya wafanyakazi wa serikali iliyolingana karibu sawa sekta binafsi; faida ya matunda ya uhuru kwa wote bila kubagua rangi au miji/vijijini; na kujiwekea akiba binafsi na taifa.

Kulikuwepo pia na upendeleo mkubwa kutoka kwa ma-bepari. Ikifuatia nyayo za Japani, Uingereza ilijaribu ‘to recolonize’ Asia Mashariki ya Mbali kupitia kuwekeza katika taasisi na shughuli za fedha (financial control): mabenki ya biashara na bima ya maisha. Iliwekeza huko Indonesia baada ya kufunga biashara huko Singapore na Hong Kong.

Ubia wa serikali na sekta binafsi ulivuta wawekezaji wa nje. Lakini serikali haikujiondoa katika kuongoza dira ya maendeleo kwa kuweka malengo na mipango ya taifa. Ubia huo uliwezesha kuhamisha ujuzi na uzalishaji (transfer of information and appropriate technologies).
Shirika la Mafuta la Malaysia (Petronas) ni mfano mzuri wa (‘transfer of technology’). Shirika hili liliundwa na Waziri Mkuu Mahathir Mohamad kwa kukopa mfano wa Indonesia na kujenga Heavy Industrial Corporation of Malaysia (HICOM).

Uongozi wa serikali za nchi hizo uliingilia kati uzalishaji wa miradi ya maendeleo iliyoendana na wakati. Hili ni la muhimu kuzingatia. Historia ya nchi nyingi zilizoendelea kwa kasi inaonyesha miingilio ya serikali zake katika kuongoza mikakati ya maendeleo.
Kwa mfano, ukoloni ulifuata sera za kusetri kwa nguvu zote wawekezaji binafsi: Uhispania, Ureno, Italia, Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji na Uingereza tangu enzi za ‘ugunduzi’ (the age of overseas discoveries) na wakati wa ukoloni.

Mfano wa Amerika pia unafuata huo wa Nchi za Ulaya Magharibi. Mbali ya utajiri wake kukuzwa na kuendelezwa na mfumo-unyama wa utumwa, serikali ilieneza ukoloni wake ikilinda wawekezaji na wakazi kuelekea pande za Amerika (kusini na magharibi), Visiwa vya Pasifiki, Panama City – wakati waujenzi wa Mfereji wa Panama – hadi huko Hawaii na Alaska.
Urusi nayo ilifanya hivyo hivyo, kama serikali ya Amerika. Serikali ilieneza ukoloni wake huko Ulaya Mashariki na, baadaye, kujenga himaya ya Soyuz Sovietskikh Sotsialisticheskikh Respublik (Union of Soviet Socialist Republics) au USSR, kwa kifupi.

Serikali ya Nazi-Ujerumani iliingilia kati uchumi wa nchi hiyo kwa ubia kati ya serikali na sekta binfasi (cartels) kiasi cha kuwa na uchumi uliokuwa ukikua kwa ari, nguvu na kasi sana kushinda uchumi wa nchi yeyote duniani wakati huo.
Huu ndio mchango mkubwa wa siri ya kujikwamua kwa nchi za China, India, Brazil na (sasa) Vietnam!

Hazikufungwa na Itikadi Moja
Nchi hizo hazikufuata itikadi ya aina moja (a single-ism); chache (Hong Kong na Singapore) zilisaidiwa na nafasi ya jiografia. Nchi hizo pia hazikuendelea kwa spidi moja. Ndio kusema kulizaliwa ‘tigers’ wengi sio mmoja. Sera za serikali ziliendana na wakati (fluidity in the policies) na zilijenga u-hakika (generated confidence) miongoni mwa wadau wote wa uchumi.

Hong Kong ilifuata sekta binafsi iliyojipangia mipango na miradi ya maendeleo bila serikali kuingilia au kupanga cha kuzalisha.
Indonesia, Malaysia na Singapore serikali zake zilikuwa na ubia na sekta binafsi na kuunda timu ya mipango na miradi ya maendeleo (zikiiga mfano wa Korea Kusini) na mabenki nchini yalishirikiana na wazalishaji na kupendelewa na Uingereza, Amerika na Benki Kuu ya Dunia ili zicheze mchezo na ‘the big boys’.

Taiwan ilikuwa na sera za bora liende – mchakato mchanganyiko; ilifanikiwa kuwa kiwanda cha dunia kilichozalisha bidhaa kwa kuongezea thamani (value-added products).
Nchi nyinginezo ziliiga mfano huu wa viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kulisha viwanda mama (mother plants) vyenye uwezo wa kubuni na kuongeza uzuri na thamani ya vizalishavyo, kuongeza maarifa katika ajira na kutengeneza mashini bora.

Kujitegemea, Kujinyima, Kuweka Akiba
Zaidi, nchi hizo pia zilijikwamua kwa matokeo ya siasa na sera za kujitegemea (self-reliance and import substitutions policy) katika kutoa elimu na uzalishaji/ulaji wa vya nchini kuliko kununua vya usasa kutoka nchi tajiri na kuuzwa na mawakala-uchwara. Sera hizi zilisaidia kuzuia faida isitoroshewe nchi za nje bali itunzwe nchini. Wananchi walijinyima kununua vya anasa kutoka nje; sawa na kijito kunywesha mto, kunywesha bahari.
Nchi hizo pia zilijinyima na kuweka akiba kwa kwa upande wa wananchi na serikali zao na kuwekeza katika mipango ya maendeleo – siri kubwa ya maendeleo. Wananchi walijiwekea akiba bila kufuja pesa zao kwa kukimbilia kununua vya usasa kutoka nje. Mishahara ya wafanyakazi ilipunguzwa bila kuwafukuza ili kulinda ajira kwa wote.

Kutokana na kuweka akiba, riba ya mabenki ilikuwa juu; wafanayakazi waliweka mapesa yao ma-benkini. Hii ilisaidia kuhimili uwekezaji kutoka ndani kuliko kutegemea wafadhili kutoka nchi za nje au kutembeza mabakuli ya mikopo nchi na kulipa riba kubwa.
Hata hivyo, kutokana na kupendelewa na wakubwa, nchi nyingi zilitembeza mabakuli mbele ya IMF na kupewa ‘grants’ sio mikopo.

Kuna nchi zilizoweza kujinyima kiasi cha 30-40% (GDP). Uzalishaji ulikua sana na kuzalisha vingi vya kuuzwa nchi za nje kwa faida kubwa. Thamani ya pesa haikupanda sana ili zizalishe kwa u-rahisi, ziuze nchi za nje ghali, uchumi uzidi kukua, na kuacha kuwa mawakala wa vya nje.
Kwa mfano, Singapore ili kuwawezesha wananchi wake kutofuja utajiri wao, serikali ilihimiza kutunza zaidi ya 20% ya GNP. Ni kutokana na sera hii Singapore ilifanikiwa kutunza karibu 42% ya GNP. Wananchi walihimizwa kununua vya nyumbani kuliko kununua vya kutoka nje.

Pesa zilizohifadhiwa zilitumika katika uwekezaji wa vitu, mashini, mali, vifaa, miundombinu, mabarabara, bandari na viwanja vya ndege, na katika kutandaza njia za mawasialiano (broadband infrastructure), elimu, afya, kukidhi bidhaa na vifaa-chakavu, ufanisi wa wafanyakazi ili kuweza kushindana na wengine bila kudororesha uchumi.
Utandawazi ulipoanza kurindima, nchi hizi zilijikuta zina mapesa ya ziada kuliko miaka ya nyuma. Mapesa hayo yalisaidia kukuza ajira na kuzalisha zaidi. Hivyo, toka mwaka 1960 hadi 2000, nchi hizi kwa miaka 40 ziliweza kujikwamua kutoka umasikini.

Serikali na sekta binafsi zilikuwa macho katika kupanga na kuchagua ni wapi pa kuwekeza kupitia mipango ya taifa ya maendeleo.
Malaysia imeboresha miundombinu, na kuufanya mji mkuu wa Kuala Lumpur mji wa kisasa unaojitegemea: makazi, maofisi, na burudani – mji uliounganishwa na miundo mbinu ya reli na mji wa serikali huko Putrajaya.

Mitandao ya mabarabara imesaidia sana kuunganisha viwanda na bandari na viwanja vya ndege ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kati ya Kuala Lumpur-Bangkok-Kuala Lumpur kwa kutumia makontena ya Asean Rail Express (ARX). Na njia kuu ya Trans-Asia Rail Link kuunganisha nchi za Singapore, Vietnam, Cambodia, Laos na Myanmar hadi huko Kunming nchini China.
Malaysia pia imekuza bandari zake ili kuchuma kutokana na biashara za ki-mataifa: Penang, Klang, Johor, Tanjung Pelepas, Kuantan na Kemaman (Jimbo la Malaysia) na Bintulu (Jimbo la Sarawak).

Lakini haikuishia kujenga bandari hizo tu; imebidi kuimarisha na kuboresha huduma zake. leo hii bandari hizo ni ‘free-zones’ zinazovutia biashara ya majini.
Malaysia pia inajivuna shirika lake la ndege na viwanja vya ndege vyenye hadhi ya ki-mataifa kwa ajili ya abiria na mizigo: Kuala Lumpur, Penang na Langkawi (Jimbo la Malaysia), Kota Kinabalu (Jimbo la Sabah) na Kuching (Jimbo la Sarawak).

Kwa kushirikiana na sekta binafsi, serikali ya Malaysia imewekeza katika kuboresha viwanda vyake 18 vya ‘Free Industrial Zones (FIZs’) vilivyosambazwa nchini na kuunganishwa na miundombinu na huduma nyinginezo: barabara, umeme, na maji, na mawasiliano.
Viwanda hivyo vilidhamiria kuzalisha bidhaa za kuuzwa nje na kuingiza pembejeo bila malipo ya forodha: mali ghafi, vipuri, mashini na vifaa muhimu.

Kuna pia sehemu zimetengwa (specialised parks) kwa ajili ya viwanda maalum: viwanda vya teknolojia huko Bukit Jalil, Kuala Lumpur na Kulim huko jimbo la Kedah, ikiwa ni pamoja na kubuni miradi ya maduka, hospitali na burudani.
Malaysia imeboresha sana miundo ya ‘hi-tech telecommunications’ ya ki-‘digital’ na ‘fibre optics’ (bandwidth, medium and high-end technologies: IDSL, IP, VPN na ATM) na matumizi mengine ya satellites (FLAG, SE-MA-WE, APCN, China-US, Japanese-US, Measat na Intelsat) ili kuharakisha mchakato wa mawasiliano.

Chama Kimoja, u-Dikiteta, u-Komunisti, Kuzawadi Dhuluma
Kila nchi (kutoka Korea Kusini, kupitia Taiwan, hadi Indonesia) iliongozwa na u-dikiteta na chama kimoja! Nchi za ma-bepari zilinyamaza kimya; hazikuhubiri injili ya demokrasia na heshima ya haki za binadamu! Nchi hizo zilitawaliwa ki-babe au ki-dikteta na maisha ya wananchi kudhibitiwa ki-‘nanny’ (yaya-mlezi mkali) – amani yenyewe ilijengeka kwa nidhamu ya woga, ki-jeshi jeshi.

Nidhamu kali ilisaidia kuleta amani (political stability) na kusetri uwekezaji. Kwa mfano, ungekamatwa ukitema ulimbo wa ‘chewing gum’ huko Singapore au kuchafua mazingira, ungetozwa faini au kuchapwa viboko.
Nchi zenye vyama vingi, chama-tawala kilicholeta uhuru kiliendelea kushika madaraka kana kwamba ni nchi ya chama kimoja, kwa mfano, huko Taiwani na Singapore.

Demokrasia na utawala bora (kama tukiondoa nchi ya Japani) ulikuwa ni utata mtupu; serikali zilihujumu haki za binadamu na huku zikishirikiana na serikali za nchi za ma-bepari kutaka kujenga ngome za kudhibiti kuenea kwa u-Komunisti.
Sera-ongoza za mambo ya ndani na nje za nchi hizo zilioana dhidi ya kulinda wawekezaji, mitaji ya nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na kudhibiti kuenea kwa u-Komunisti (to contain communism) bila kujali haki za binadamu.

Maslahi ya ki-amani, ki-usalama na ki-uchumi ya Nchi za Magharibi wakati wa tawala za vyama vya siasa vya ki-hifadhina (conservative) huwa hayajali cha haki za binadamu. Wakubwa wakikupenda hata ukiwa ni dikteta, watakusetri! Ninatoa mfano wa hivi karibuni.
Kwenye mahojiano tarehe 19 January 2011 kati ya Waziri mstaafu wa Mambo ya Nchi za Nje na Mshauri Mkuu wa Usalama wa Taifa (Amerika) Henry Alfred Kissinger (m-Jerumani/m-Amerika) akihojiwa na Charlie Ross (Public Broadcasting Corporation, Channel Thirteen), kuhusu masuala mbalimbali ya uhusuano kati ya Amerika na China, kufuatia ujio wa ugeni wa Rais Hu Jintao wa China nchini Amerika, Kissinger alitamka bayana kuwa maisha au utamaduni wa ki-Magharibi (maslahi yao katika nchi za kigeni) ni tunu au azizi kushinda utamaduni mwingine duniani. Kwahiyo, Kissinger hataki kuiona China ikizipiku nchi za Ulaya Magharibi na Amerika.

Mpaka sasa China inaendelea kujikwamua na kuogopwa kwamba huenda baada ya miaka 25 itashika kilele cha ubabe duniani.
Hao ma-bepari wakubwa, wakiongozwa na Amerika, Uingereza, Benki Kuu ya Dunia na Taasisi ya Fedha ya ki-Mataifa, walipendelea nchi hizo kuwa tunu au vito (economic showcases) mbele ya nchi za u-Komunisti: China, Korea Kasikazini, Mymmar, Kambodia, Laos na Vietnam.

Wakati wa enzi za uhasama wa ‘Vita Baridi’, Nchi za Magharibi zilionesha upendeleo mkubwa kwa kuzikinga nchi hizo za Asia Mashariki na ya Mbali dhidi ya mwingilio na kuenea kwa u-Komunisti. Zilizawadishwa sana wakati wa tawala za mkondo wa kulia za Waziri Mkuu wa Uingereza Margaret Thatcher na Rais Ronald Reagan wa Amerika.
Zaidi, Balozi wa Amerika Paul Dundes Wolfowitz huko Indonesia hakutaka kukutana na wanaharakati wa haki za binadamu ili kujadili jinsi serikali ya Rais General Haji Mohammad Suharto (Soeharto) ilivyokuwa ikihujumu haki hizo.

Wakati wa enzi za Rais Ronald Reagan, Balozi Wolfowitz alisukuma suala la demokrasia na haki za binadamu ukumbi wa nyuma kuhusu uhusiano kati ya Amerika na Indonesia. Ziara ya Rais Reagan iliyobatizwa, ‘The Winds of Freedom Tour’, Balozi Wolfowitz hakupenda waandishi wa habari wa Amerika na Australia waalikwe wasije wakamwaibisha mwenyeji wao mbele ya Rais Reagan. Alipendekeza masuala ya uchumi tu ndio yaletwe mbele ya meza kati ya ma-Rais hao wawili.
Rais Suharto na Waziri wa Teknolojia B.J. Habibie walizawadiwa kuzindua sera ya viwanda mkakati (strategic industries) katika viwanda vinane kwa matumizi ya kijeshi na kiraia.

Korea Kusini na Taiwan zote zina historia karibu sawa na hiyo ya Indonesia katika kuhujumu haki za binadamu na kudumaza demokrasia. Taiwan ilipendelewa sana dhidi ya u-Komunisti wa ‘panda’ (China). Taiwan iling’aa wakati China (yenye wingi wa watu duniani) ikikosa maendeleo ya vitu na huduma.
Korea Kusini ilikingwa na kupambwa (a show case) na wakubwa dhidi ya m-Komunisti Korea Kasikazini – nchi ya siasa ya ‘juche’ – kujitegemea!

Serikali ya Indonesia (sawa na South Korea na Taiwan) ilijenga muundo wa maendeleo ki-muhula. Na huku ikitawaliwa kwa u-dikteta wenye kuhujumu haki za binadamu na kudumaza demokrasia eti kulinda haki za ‘constitutional liberties’ kupitia ubepari: ubinafsi (individual good) ulisheheni dhidi ya umma (common good).
Pamoja na nchi ya Indonesia kuua watu wengi nchini humo enzi za Rais Gerard Ford mwaka 1975, ilishambulia na kuua wananchi wa Timori Mashariki eti kwa kupinga u-Komunisti. Zaidi, ilitumikisha wafanyakazi kwa bei duni chini ya u-dikiteta wa mabuti ya viongozi wana-jeshi na chini ya tawala za chama kimoja!

Unyonyaji, Sweatshops, Economic Processing Zones, Uporaji wa Maliasili
Mvuto mwingine ulikuwa unyonyaji katika ‘sweatshops’ kwa vibarua wasio na elimu na wenye kulipwa kiduchu (faida kwa wawekezaji) kufuatia kuanguka kwa Latin Amerika ya Mexico. Wafanyakazi hao walilipwa kwa kumaliza ‘ngwe’ ya kazi waliyopewa, kwa mfano, kushona mashati 50 kwa siku.

Zaidi, kulikuwepo na hali ya unyonyaji wa maliasili (misitu, mafuta na madini).
Msomaji, pengine utakumbuka kisa cha wawekezaji wa Amerika, Adiddas, waliotuhumiwa sana kwa kuwatumikisha wananchi wa Indonesia na kuwalipa kiduchu.

Mstaafu Balozi wa Amerika Umoja wa Mataifa Andrew Young (enzi za Rais Jimmy Carter) alitumwa na makampuni ya Amerika yenye viwanda nchini Indonesia kujaribu kutoa ripoti za hujuma hizo. Ripoti ya Balozi Young ilishangaza wengi: alikataa kuwepo kwa hujuma hizo!
Mstaaafu Balozi Andrew Young leo hii ni mmoja wa wawakilishi wa makampuni ya Amerika yanayopora rasilimali za Bara la Afrika, ikiwamo kampuni ya madini ya Barrick nchini Tanzania. Ni mshiriki sana katika Mikutano ya Sullivan; alikuja kwenye Mkutano wa Sullivan Arusha!

Tunu Kuitwa ‘Tiger’
Msomaji, jina la ‘tiger’ linavuta na limeanza kuvuka mipaka ya uchumi na kuingilia uga wa elimu. Kwa mfano, sasa hivi Amerika kuna malumbano kuhusu hoja ya Prof. Amy Chua (a John M. Duff, Jr. Professor of Law at Yale Law School) – mama wa ki-China na mumewe mzungu wa ki-Amerika).
Prof. Chua anatetea akina mama wa ki-China kwa kujikita kwao katika mikakati na mapambano ya kulea, kufunda na kuwasaidia watoto wao wafaulu maishani, ikiwa ni pamoja na utii kwa wazazi na katika mashindano ya elimu mashuleni, bila kudekezwa, kama walivyo watoto wa Amerika.

Kitabu chake (The Battle Hymn of the Tiger Mother) kinafaa kusomwa kwa malinganisho (comparative purposes). Katika mada tofauti ya ‘Why Chinese Mothers Are Superior’ (tafsiri yangu – ‘Kwa Nini Mama wa ki-China ni Mahiri’) katika malezi ya watoto wao, Prof. Chua anajaribu kueleza siri ya kufanikiwa kwa watoto wake katika hisibati na muziki.
Kuna wenye kuwapigia debe akina mama-wazazi wa ki-China na kuwabatiza kwa jina la ‘Tiger Mothers’. Wataalam wengine wa taaluma ya elimu wanaanza kuamini kuwa huenda wa-Asia wana 1Q ya juu. Dai hili halina ukweli; ufaulu huo unachangiwa sana na mila za mashindano, kulingana na dhana ya Confucianism.

Kuna wa-Ulaya/Amerika ambao hupenda sana kula maini ya bata. Baadhi ya wafuga-bata wa Amerika, kwa mfano, wanamlazimisha bata kula chakula kingi hata kama ameshiba; chakula husukumizwa kooni kwa mashini ili bata aweze kujenga ini kubwa; kwani ini kubwa, pesa nyingi.
Hoja ya Prof. Chua imepokelewa kwa hisia tofauti. Wengine, wanamkosoa kwa kulea watoto wake, kulingana na dhana-tata ya ‘tabula rasa’ na kuwalazimisha kwa nguvu ‘wale chakula’ cha elimu, kama hao bata, ili waongoze madarasani na mashuleni! Wanaofaulu, hufanya vizuri maishani.

Lakini kushinikizwa huko hakuwaletei furaha maishani. Zaidi, watoto wengine (kwa kushinikizwa na wazazi wao) hujiua kama hawafanikiwi. Huko China na Korea Kusini kuna idadi kubwa ya vifo vya kujiua miongoni mwa vijana wa kati ya miaka 15 na 25!
Wanafunzi wa ki-Asia ni wengi sana na wanazidi kung’aa kwenye vyuo vikuu vya Amerika, hasa wa kutoka China na India. Zaidi, wakitahiniwa, ki-mataifa, wanafunzi wa huko Asia (na watoto wenye asili ya ki-Asia walioko, kwa mfano Amerika), wanafanya vizuri kuliko watoto wa kutoka kwingineko.

Hii inalifanya taifa la Amerika kujiuliza kwa nini linashika nafasi karibu ya nane katika masomo ya hisibati na sayansi!
Nimeingilia hili la ‘mashindano’ kushadadia hoja kuwa nchi tunazozizungumzia (hasa zenye watu wa asili ya ki-China na wenye kufuata dhana ya Confucianism) zilikumbatia kwa dhati kuchapakazi kwa mashindano.

Kwa mfano, kuna kisa cha Waziri Mkuu wa Singapore kuchapa kazi kiasi cha kukosa usingizi na mkewe (daktari) kumpa vidonge vya usingizi. Kuna siku alipokea ugeni kutoka kwa Malkia wa Uingereza na huku akiwa amelazwa hospitalini.
Tuzungumzia mfano wa Singapore katika juhudi yetu ya kuangalia kwa u-karibu na u-ndani kwa nini kisiwa hiki (kisicho na maliasili na kinachoagiza mchanga wa kujengea kutoka nje) kimeiacha Tanzania yetu mataani.

Singapore (The City of Lions) ipo kwenye Ukanda wa Joto wa Ikweta wenye joto na ufukutu mkali. Sehemu hiyo iko ki-mkakati (strategically) kwa usafiri wa majini kwenye Mlangobahari wa Malacca kutoka na kuingia Bahari ya Hindi, Bahari ya China Kusini, Bara la Australasia (Asia ya Mbali, Australia na New Zealand) na ina uwanja wa ndege mkubwa kwa usafiri wa angani.
Singapore, ‘chunusi kwenye uso wa Malaysia’, ina eneo dogo sana (kilomita-mraba 646 sawa na eneo la Jiji la Chicago, Amerika). Idadi ya watu haifikii milioni tano, ambao wamejigawa ki-uzawa; yaani, wa-Hindi, wa-Malay na wa-China. Zaidi, wamejigawa ki-dini; yaani, wa-Islamu na wa-Budha. Masuala ya siasa, ubaguzi wa rangi au dini hayaruhusiwi kuwa viini-zungumziwa na wasanii.

Kisiwa cha Singapore kilianza kama kijiji cha wavuvi wachache. Kilijaa mabwawa ya mbu wengi wenye kueneza ugonjwa wa malaria. Bandari na mandhari ya ufukwe wake kulijaa mitumbwi (sampans na junks). Walevi wa madawa ya ‘opium’ walijaa kwenye sehemu walikoishi jamii ya wa-China, ambao walikuwa wakichungulia madirishani na huku wamewaka chakari, mbali ya wapigakamari na kusheheni biashara ya u-malaya na u-shoga (changudoa).
Licha ya sifa hizo mbaya, Kisiwa cha Singapore kilikuwa kikishindaniwa kati ya Uingereza na China kutokana na jiografia yake. Waingereza walikitawala kwa muda wa miaka 149 kwa lengo la kukifanya mahali pa biashara na maghala/soko makubwa (commercial emporium), kama Hongkong, kwa masoko makubwa ya kikoloni ya ki-fedha na dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya chini ya China.

Mwaka 1963 kilijitawala chini ya Muungano wa Malaya na Majimbo ya Sabah na Sarawak. Lakini Mungano ulivunjika 1965 kutokana na wa-China na wa-Malaysia kugombana. Vyuo vikuu vilijaa wasomi wa mkono wa kushoto; ma-Komunisti waliiingilia vyama vya wafanyakazi; na haikuwa na jeshi la ulinzi. Haikuwa na maliasili na eneo la kuzidi kupanuka; mji mchafu wa kunuka; mifereji ya maji machafu na taka kila mahali; na ajira haba.
Zaidi, ilikuwa inaagiza maji na chakula kutoka nje ili kusaidia lishe nchini ingawa ilikuwa na nguruwe, matunda na mboga; majitaka yalinuka kila mahali; na ajira haba sana kiasi cha 14%; na wenye manywele marefu (hippies) kutapakaa kila mahali.

Serikali (Waziri Mkuu) Yauvalia Njuga u-Masikini
Kujikwamua kwa Singapore kunalingana na methali ya wa-kuria: “Inyanyi ilatangata Ubukama.” (Tafsiri: Sumbuka (Henya) au taabu kwanza; ufalme uko (raha iko) mbele.”)
Singapore ilijiuliza maswali mazito: Singapore inaishi katika ulimwengu wa hali gani? Singapore imetoka, iko na inakwenda wapi? Singapore itilie mkazo mafunzo gani mashuleni ili kuweza kufanikisha ndoto ya maisha bora kwa wananchi wake?

Kutokana na jiografia ya Singapore, Waziri Mkuu wa kwanza Lee Kwan Yew (msomi wa Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza) – ambaye alitokana na ukoo wa ki-fisadi wa wacheza kamari – alitamka, “Singapore ilirithiwa bila ukanda wa bara; moyo bila mwili.”
Singapore iliamua kujijenga ili kujikomboa kutoka ma-dhambi, majuto na mavune ya miaka mingi kabla ya 1960. Ilipiga marufuku ma-kasino, kamari (iliyokuwa imefilisi ukoo wake), kuongeza kodi kwa tumbaku, na vinywaji vikali; na kudhibiti biashara ya madawa ya kulevya. Singapore ikawa ya walokoke.

Ili kudhibiti umaskini na mazoea yasiyo ya maadili mema, serikali ililivalia njuga suala la u-masikini. Singapore ilianza kufyeka na kujenga upya bandari na madhari yake, ingawa iliashiria kutambulika kama nchi itakayojiunga na maswaiba wa nchi fukara za Dunia ya Tatu. Lakini Singapore ilijinasua kuitwa hivyo!
Wafanyakazi walihimizwa kuchapakazi, mithili ya punda! Kwa mfano, siku moja ilimbidi huyo Waziri Mkuu Lee Kwan Yew akutane na Balozi wa Uingereza (akibeba ujumbe kutoka kwa Malkia wa Uingereza) akiwa hospitalini alikolazwa kutoka na uchovu na mavune ya kutolala kwa muda mrefu akichapakazi. Mkewe alikuwa ndiye daktari wake, na ilibidi kumpa dawa za usingizi au kumlaza (tranquilizers).

Singapore ilibadilika na kuwa kiota cha biashara, pesa na usafiri na kuwa jiji la kisasa (a prissy and trendy city). Ilijenga ma-kasino (mithili ya Las Vegas) na viota vya maraha, kwa mifano, Ministry of Sound ya London na Bangkong Q Bar, Velvet Underground, Vivo City Mall, jengo la zamani la watawa wa Convent of the Holy Infant Jesus sasa ni restauranti ya Chijmes, na hoteli za kuvutia, kama hiyo ya Fullerton Hotel (jengo la posta ya zamani) yenye kusifiwa huko Asia na kuna majumba ya ‘miendo ya paka’ kwa ajili ya ubunifu wa mavazi (fashion industry).
Zaidi, iliweka boti za fahari kwa watalii, madhahari safi, na mataa kila mahali ili kuvuta watalii kuzishinda Thailand na Malaysia na ilijenga majumba ya sinema, tamasha na burudani za utamaduni za wasanii wengi – waliokuwa wanapigwa marufuku mwanzoni na kukimbilia Bangkong, Thailand.

Viota vya minuso na maraha yake na burudani vilipigwa marufuku. Wasanii wengi walikimbilia Thailand na Malaysia. Ni hivi majuzi tu walipoaanza kuingiza hayo ya burudani na wafanyakazi kutakiwa kwa lazima kutabasamu ili kulegeza mavunde ya kazi!
Kulegeza u-Chapajikazi; Tabasamu
Wakati wa awamu ya pili, Singapore ilikuwa ni mojawapo ya nchi nne za Asia Mashariki kuitwa na Uingereza kwa jina la ‘Asian Tigers’. Zingine zilikuwa ni Hong Kong, Korea Kusini na Taiwan. Ma-bepari wa London mwaka 1995 (wakiongozwa na Waziri wa Fedha wa Uingereza Sir Kenneth Clarke na Makamu wa Rais wa Nchi za Ulaya Sir Leon Brittan) walipanga mkakati maalum wa kuhamasisha mfumo-kusudiwa kwa nchi hizo.

Mabepari hao mwaka 1996 walifanikiwa kumpata mweza wao Waziri Mkuu wa Singapore Goh Chok Tong (awamu ya pili) katika kuzindua mfumo-kusudiwa. Serikali ilifanikisha kuweka mipango kabambe ya elimu. Iliweka mikakati ya mustakabali wa taifa; ni wajibu wa serikali (sio wa sekta binafsi) kuandaa mipango ya elimu-kombozi ya taifa.
Wakati wa awamu ya pili chini ya Waziri Mkuu Goh Chok Tong mwaka 2004 na awamu ya sasa, chini ya Waziri Mkuu Lee Hsien Loong (mtoto wa Waziri Mkuu Lee Kwan Yew – shauri la siasa za kitanda kuzalisha viongozi wa nchi), serikali ilibidi kufungua madirisha (msemo wa ‘Mzee Ruksa’ mstaafu Rais Hassan Mwinyi) ili hewa ya maraha. Kuchapakazi kulilazimu kulegezwa (fine tuning) ikiwa ni pamoja na kuwataka wa-Singapore watabasamu ili kuficha uchovu na mavune ya kuchapakazi.

Zaidi, Serikali iljiingiza katika sakata la mipango na miradi ya maendeleo –sakata ambalo likiachiwa sekta binafsi, wachezaji watafanyiana rafu. Serikali ilikuwa na ubia na sekta binafsi na kuunda timu ya mipango na miradi ya maendeleo (ikiiga mfano wa Korea Kusini) na mabenki nchini yalishirikiana na wazalishaji huku ikipendelewa na Uingereza, Amerika na Benki Kuu ya Dunia ili icheze mchezo na ‘the big boys’.
Kama njiapanda ya kuingilia Asia Mashariki na ya Mbali kupitia Mlangobahari wa Malacca, Singapore ina vivutio vitatu muhimu: ‘location, location, location’, (a) kutoka na kuingilia Bahari ya Hindi; (b) kutoka na kuingilia Bahari ya China Kusini; na (c) uwanja wa ndege kwa sehemu hizo ikiwa ni pamoja na kuhudumia Bara la Australasia (Asia ya Mbali, Australia na New Zealand).

Leo hii, Singapore ni bandari-ghala (entrĂªport) kubwa kwa nchi zote za Australia, New Zealand na Asia Mashariki ya Mbali. Biashara ya huko ni kubwa sana; haiwezi kulinganishwa na biashara inayopita Dar es Salaam kwenda nchi za jirani!
Biashara nchini humo ilikuza miundombinu iliyojengwa kwa ajira ya unyonyaji wa mfumo wa manamba (wa-China, wa-Sri Lanka na wa-Hindi). Wananchi walitokana na mchanganyiko wa mataifa, dini na lugha nyingi, kwa mifano, wa-Uingereza, wa-Hindi, wa-Malalysia, wa-China na wa-Japani; dini nyingi, kwa mifano, wa-Budha, wa-Tao, wa-Islamu, wa-Confucius, wa-Kristo na wa-Hindu); na lugha nyingi, kwa mifano, ki-Ingereza, ki-Mandarini, ki-Malaysia, na ki-Tamili). Lakini leo hii kuna mataifa matatu makubwa” wa-Hindi, wa-China na wa-Malasia.

Waziri Mkuu awamu ya Tatu Lee Hsien Loong alipanua mianya ya biashara. Alitaka Singapore kutengeneza “fweza, fweza” kwa wingi. Aliruhusu watalii, na kuzidisha biashara kwa ajili ya kujenga tabaka la kati bila upendeleo.
Singapore ikatajirika kushinda nchi nyinginezo za Asia, ki-income per capita; Shirika la Ndege (Singapore Airlines) linaongoza duniani kwa sifa za juu; kiasi cha 90% ya wananchi wake wanaishi majumbani mwao; biashara inasheheni bila urasimu, ufisadi/rushwa na u-wazi (the freest).

Singapore inasifika kwa uwazi na utawala bora huku ikishindana kila mara kuwa ya kwanza; ilikataa kuwa namba mbili. Kuna majengo marefu na alama za utajiri. Mji ni msafi sana – hakuna uchafu wa mazingira. Bandari yake leo hii inag’aa kwa biashara.
Elimu ni ya kiwango cha juu na wengi wameelemika hadi chuo kikuu na wengi wamehitimu elimu-kazi/ajira kupitia vyuo vya ufundi (technicals and polytechnics) mbalimbali; wanatumia ‘internet’ ya spidi kali (broadband); kuna uhuru wa biashara na serikali inapendelea wawekezaji; kuna uwazi wa hali ya juu katika fani za kazi na biashara; na hakuna ufisadi na rushwa.

Kuna utawala bora; hakuna upendeleo kazini – wafanyakazi wanaajiriliwa na kupandishwa vyeo kulingana na sifa zao za ujuzi na ufanisi (meritocracy) – sio u-shemeji, u-kabila, u-dini, u-chumba, u-jomba, nk); wafanyakazi wa umma wanalipwa SAWA na wale wa sekta binafsi.
Serikali inaendeshwa kama bodi ya wakurugenzi wa kampuni/shirika binafsi; hakuna cha urasimu; na wala haikuachana na mfumo wa u-Koloni: elimu, lugha ya ki-Ingereza, mabarabara yalibakia na majina ya ki-Koloni.

Singapore ilipiga vita ubaguzi wa rangi na dini ili matunda ya uhuru yawafikie wananchi wote – maisha bora kwa kila m-Singapore! Mapato ya nchi yanagawanywa sawa miongoni mwa wananchi wenye asili tofauti: wa-Hindi, wa-China na wa-Malaysia; na inasemekana imetumia ufanisi wa kazi na hali halisi kwa ukatili zaidi kushinda serikali yeyote.
Kujenga Tabaka la Kati; Watengeneza/Wanunuzi ‘Goods/Services’ (Bidhaa na Huduma)

Singapore imetawaliwa mithili ya ki-dikiteta ikiongozwa na chama kimoja kikubwa na familia moja ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza Lee Kwan Yew tangu uhuru! Singapore, yenye kutamba ‘maisha bora kwa wote’, imejengeka kwa ‘high-end’ za viwandani na mauzo kwa nchi za nje.
Kutokana na uhaba wa maliasili na ardhi ya kupanua, ilibidi ijikite katika kuzalisha huduma (high-end products or upmarket commodities) zilizolenga matajiri, kwa mfano, bidhaa fahari (magari, manukato, saa, kamera, komputa), majumba na mauzo ya vifaa vya uganga (biomedical exports) ambayo imesaidia sana nchi hiyo kufikia kukua kiasi cha 14% GDP (kutokana na mauzo ya biomedical exports).

Kama sikukosea, wastani wa ‘income per capita’ yake ni karibu $30,000; na ‘gross national product’ yake ni zaidi ya $182 bilioni. (Linganisha na Tanzania: i/c ni $440; GNP ni $20 bilioni).
Singapore imefanikiwa kuondoa tabaka la chini; tabaka wavuvi, makuli, malaya, wachuuzi wadogo, watembeza madaya ya kulevya na wengineo. Tabaka hili lilimezwa na wafanyakazi viwandani, maofisini na katika shughuli nyingine za huduma – tabaka la kati (middleclass) – lenye kuuza nguvu zake na kulipwa mishahara.

Hapo juu nimegusia suala la tabaka la wazalishaji. Mchambuzi mahiri wa mambo ya jamii m-Amerika Alvin Toffler analiita tabaka hili: ‘prosumers’; yaani, ‘producers and consumers’). Ninaliita, kwa kifupi, ‘wazalishalaji’ (wazalishaji na walaji).
Sisi hapa Tanzania, tabaka hili ni la wakulima, wafugaji, wawindaji au waokota porini, wahunzi/wasusi na machinga. Kwa ujumla, ni tabaka la wazalishaji na walaji wakati huo huo; yaani, tabaka la wenye kuzalisha na kuvitumia wazalishavyo (producers and consumers.

Kwa bahati mbaya, Tanzania imedhamiria kuliua tabaka hili la chini kwa kuandikisha ‘plots’ za mashamba na mfumo wa ufugaji huko vijijini ili utajiri (asset) huo utumike, kama rehani (collateral) ya kukopa mabenkini. Mabenki mengi sio ya wazawa; hivyo, mustakabali wa wazalishaji wetu utawekwa mikononi mwa wageni – wageni. Polepole, wageni wataanza kumiliki ardhi yetu!
Dhana za uchumi wa ki-Magharibi hauzingatii kabisa mchango wa wazalishaji! Nchi zinapimwa kwa kile kiitwacho, ‘income per capita’ (yaani, utajri wa mapesa kugawiwa sawa kwa wananchi) au ‘gross domestic national product’ (yaani, uzalishaji wote wa nchi ki-uchumi kwa mwaka).

Dhana hizo zinashindwa kubaini na kukubali kuwa vingi wa wazalishaji havipitii soko-pima! Kwa mfano, wazalishaji hawapati mahitaji yao kupitia ‘Shoprites’! Tunapimwa kwa mizani ya vigezo vya nchi ambazo ni ‘industrialized’ bila kujali kuwa Tanzania bado ni ‘prosumer’!
Chama Kimoja; Serikali Yaya-Mkali; Kufundisha Uungwana; Kudhibiti Tabia Mbaya
Singapore ni dola la yaya-mkali (a nanny State), chini ya chama-tawala kimoja chenye nguvu toka uhuru, People’s Action Party. Ilibidi serikali kujiuliza maswali (na kupata majibu) mazito kuhusu ni dunia ya namna gani Singapore inatakiwa kuishi ndani? Singapore inatoka, imefika, na inakwenda wapi? Je, ni vipi vya kufundisha mashuleni ili Singapore ifikie lengo lake?

Kuna malalamiko ya kuhujumu maisha ya mtu binafsi. Maslahi ya kundi ni juu ya yale ya u-binafsi kulingana itikadi ya ki-dini ya Confucianism na Uhuru wa binafsi haulindwi sana bali wa kundi. Hata hivyo, haifuati itikadi ya u-Jamaa au u-Komunisti.
Wananchi wanatii amri ya serikali/viongozi na kuheshimu wazee. Wazazi wanaweza kuwashitaki watoto wao kama wakikosa maadili. Dhana ya Confucianism ilijenga hulka ya utii au nidhamu ya woga na kudumaza ubunifu na uthubutu (creativity and risk-taking) kutokana na kuwa na viongozi waangalizi kila mahali.

Baadhi ya magazeti ya Ulaya yalipigwa marufuku kwa ubaguzi wa rangi (kwa mfano, gazeti la Cosmopolitan); hakukuwa na viota vya maraha na minuso; mabaa yalifungwa kabla walevi hawajavinjari kuweka nishai kidogo – watu ilikuwa ni kuchapajazi, kuchapakazi; na ukiangusha kishungi cha sigara, utafainiwa $328.
Ukichafua mazingira na majengo kwa graffiti au ukitema ‘chewing-gum’ barabarani, utachapwa viboko (ilinunuliwa kwa ruhusa ya daktari ili kulinda afya); ukipatikana na gramu 15 za heroin, utanyongwa kama unazidi miaka 18 (na imenyonga watu wengi); ukivuka taa za barabarani bila ruksa ya kwenda au kuendesha kuzidi spidi zilizoruhusiwa.

Kwenye majumba ya kupanga (yenye idadi ya wakazi 10%) usipovuta maji baada ya kutumia choo (kuna kamera za video) utatafutwa na polisi na kupewa adhabu; na kama hufuati maadili ya adabu kwenye kadamnasi, kwa mfano, kuongea kwa simu katika jumba la sinema au kutovuta maji msalani, utapelekwa kwenye taasisi za kurekebisha tabia (behaviour).
Zaidi, kama ukichelewa tafrija wakati wa arusi utapigwa faini na kama utawahi utatozwa $60 za vocha ya kununua chochote dukani; wanawake walihongwa wasizae, kama sungura; wenye akili walihimizwa kuoana; na wenye manywele marefu walipigwa marufuku.

Uhalifu nchini ni chini sana; kila kitu inakwenda kwa wakati (very efficient); hakuna foleni za magari kwenda au kutoka makazini kwa sababu ya ushuru wa kutumia barabara; na hakuna kuchafua mazingira na upandaji wa miti ulihimizwa kuufanya mji uwe wa kijanikibichi.
Singapore kujiingiza katika nyenzo muhimu za uchumi wake bila kuiachia sekta binafsi ili iweze kudhibiti mienendo ya uchumi. Inatoa ruzuku kwa wanafunzi waweze kufikia chuo kikuu (mfano wa Ujerumani) na kuruzuku makazi kwa kila mtu kuwa na nyumba kuliko kupanga.

Kuna vyuo mbalimbali vyenye kutoa elimu/ajira sio nadharia tu kwa kila mhitimu kuuzika na kupata ajira. Ina soko huru kabisa; hakuna cha ushuru wa vya kutoka nje. Mishahara ya chini, ajira pamoja na bima ya maisha kwa wananchi wote.
Zaidi, Singapore haifuati itikadi zilizoandikwa kwenye mbao za mawe za mkono wa kulia au kushoto – bora tu itikadi hiyo inaleta manufaa. Kila itikadi yenye manufaa kwa Singapore inapokelewa na kuahamishwa nchini (pragmatism); na inafuata na kuiga kutoka popote duniani (eclecticism), pia. Kwa kuchanganya u-bepari na u-jamaa (chini ya ‘yaya-mkali’), imeweza kuleta mafanikio kutoka ‘both worlds’.

Singapore ilifuata siasa ya kujitegemea (self-reliance and import substitutions policy). Wananchi walijimyima kununua vya anasa kutoka nje; sawa na kijito kunywesha mto, kunywesha bahari.
Ilijiwekea akiba kwa kwa upande wa wananchi na serikali na kuwawezesha wananchi wake kutofuja utajiri wao, serikali ilihimiza kutunza zaidi ya 20% ya GNP. Ni kutokana na sera hii Singapore ilifanikiwa kutunza karibu 42% ya GNP. Wananchi walihimizwa kununua vya nyumbani kuliko kununua vya kutoka nje.

Biashara kubwa ya huko Asia Mashariki ya Mbali ilikuwa ya haramu (the illegal ‘black” economy) yenye faida kubwa: u-malaya, madawa ya kulevya, riba ya uajiri (labor export brokerage fees), magendo ya silaha, wizi wa mafuta, kamari, ma-kasino, bahati nasibu za njia za panya na kupiga kamari mipirani.
Msomaji, umevisoma baadhi ya vigezo au viungo vya mapishi ya kuzikwamua nchi za Indonesia, Malaysia na Singapore. Umesoma, pia, namna Singapore ilivyojikwamua. Sijui umejifunza yepi ya kulinganisha na Tanzania yetu?

Kama nilivoandika hapo mwanzoni, pengine, cha maana kwetu sisi sio kurudufisha mifano ya Indonesia, Malaysia na Singapore kwa Tanzania. Hata hivyo, tunaweza kujifunza baadhi ya vigezo vichache na “very eclectically” na ‘pragmatically’ na kubakia na vilivyo ‘constructive’ kwa mustakabali wa Tanzania
Msomaji, makala yeyote haina budi kufikia mwisho.
Asante kwa kunisoma kwa kirefu na karibu kwa michango, nyongeza na maoni zaidi!

Naomba kuwasilisha.

No comments:

Post a Comment