Thursday, 28 June 2012 08:50 (Mwananchi) |
DHANA ya ujasiriamali Tanzania imeshika kasi hasa katika karne hii ya 21 licha ya kuwapo duniani kwa muda mrefu. Kimsingi, ujasiriamali Tanzania umeshika kasi miaka ya 2000, hasa kutokana na juhudi za Serikali kuboresha sera na sheria mbalimbali za uchumi kwa mfano, sera ya maendeleo ya biashara ndogo ndogo. Kutokana na hili, tumeshuhudia watu wengi wakijitoa kimasomaso kuanzisha biashara au kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali. Je, hao wote ni wajasiriamali halisi? Kupima kama kweli wewe ni mjasiriamali halisi karibu kupitia mada hii inayotumia stadi ya David McClelland ambaye ni mwanasaikolojia kutoka chuo kikuu cha Havard nchini Marekani aliyegundua tabia za kisaokolojia zinazojengeka ndani ya mjasiriamali ambaye amefanikiwa kibiashara. Stadi hiyo inaonyesha tabia kuu 10 kiujasiriamali na zilizovunjwa katika tabia ndogo ndogo 30 zikiwa kama viashiria vya mjasiriamali halisi kama inavyoelezwa hapa chini. 1.Kutafuta fursa na uwezo wa kujituma. Katika hatua hii, mjasiriamali anakuwa na tabia ya kufanya mambo kabla kulazimishwa. Mjasiriamali ambaye anaona fursa kwa haraka na anafanya uamuzi kwa wakati kuboresha biashara yake kwa kuongeza ubora wa bidhaa au huduma kwa wateja wake. 2. Jitihada. Mjasiriamali anachukua hatua bila kujali vikwazo wala matatizo, anatumia mbinu mbadala kuondokana na matatizo yanaomkabili. Pia anajiona anawajibika kwa mafanikio anapotimiza lengo alilokusudia. Kimsingi mjasiriamali hachoki na wala hakati tamaa, muda wote akishindwa hili hufanya hili au kubadilisha mbinu ili afikie malengo. 3. Mkweli na kutimiza ahadi. Mjasiriamali anajitoa kwa hali na mali ili kumaliza kazi aliyojipangia, inapowezekana huuingilia hata majukumu ya wengine ili kumaliza kazi haraka na kwa wakati. Pia anahakikisha wateja wake wanaridhika. Pia anapokea oda na kutoa ahadi anazoweza kuzitimiza. 4. Ubora na ufanisi. Mjasiriamali anatafuta mbinu mbalimbali kufanya mambo vizuri, haraka na kwa gharama nafuu. Pia anaweka utaratibu na kuzifuata ili kuhakikisha kazi inamalizika kwa muda na katika kiwango stahiki. 5. Anakuwa makini na vihatarishi. Muda wote anachukua tahadhari na kutafuta njia mbadala zisizo na hatari kubwa, anachukua hatua kupunguza hatari na kudhibiti kutokea kwa hatari yoyote ya kibiashara. 6. Malengo. Mjasiriamali, anajipangia mikakati na shabaha ya kupunguza matatizo kwa kutumia fursa. Pia anaweka malengo ya muda mfupi, wa kati na mrefu. Kimsingi mjasiriamali halisi hapati faida kwa bahati bali inapangwa. 7. Anatafuta taarifa. Mjasiriamali anatafuta taarifa nyingi kutoka vyanzo mbalimbali kutoka kwa wateja, wagavi au washindani. Anafanya utafiti wa jinsi ya kutoa bidhaa au huduma bora, na vilevile anaomba ushauri kutoka kwa watalaamu katika mambo ya biashara au kitalaamu. 8. Mipango na ufuatiliaji. Kupunguza majukumu makubwa na kuwa madogo yenye kutekelezwa ndani ya muda mahususi. Mjasirianali anapaswa kupitia mipango yake mara mara kutokana na tathimini katika ufanisi au kubadilisha mazingira. Vilevile anatunza rekodi na taarifa zake za fedha na huzitumia kufanya uamuzi. 9. Ushawishi na kujenga mtandao. Anatumia mbinu mbalimbali kuwashawishi wengine (wateja). Anatumia watu mashuhuri au wenye nafasi fulani kama wakala wake kufanikisha lengo au shabaha, na pia anachukua hatua madhubuti kutafuta na kudumisha mtandao wa kibiashara. 10. Kujiamini na kujitegemea. Anapenda kujitawala mwenyewe na kutenda kulingana na msimamo wake. Anajiweka katika nafasi ya kuona kushindwa au kufanikiwa ni kwa sababu yake mwenyewe. Pia anaonyesha dhahili ustadi na uwezo wake kufanya mambo magumu yenye changamoto. Hizi nitabia kuu 10 walizonazo wajasiriamali. Wanafanikiwa katika biashara. Jipime tabia zako zikoje unapofanya biashara. Mjasiriamali anaweza kujifunza tabia hizi kama hana. kwanamas@yahoo.com 0712 066 064 |
Thursday, June 28, 2012
Sifa kumi za mjasiriamali
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment