“ Mwandishi alifanya utafiti na kubaini kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya mafunzo ya biashara/ujasiriamali na kufanikiwa kibiashara. Lakini aligundua kuwa asilimia 80 ya wajasirimali hawana elimu ya ujasiriamali. Hii ni hatari kwa mafanikio ya sekta hii.’’
Wengi wanataka kujua kama wana sifa za ujasiriamali au pia wanawezaje kufanikiwa kibiashara.”
Tambwe katika kitabu hiki alichokiandika kwa lugha rahisi na rafiki kwa kila anayejua kusoma anamchambua mjasiriamali kama mtu mwenye ari, msukumo na nia ya kufanikiwa katika malengo aliyonayo. Huyu anatumia akili za ziada na rasilimali zinazomzunguka ili ajiletee na hata kuwaletea wengine faida.
“Ni mtu ambaye anajituma, anaweka akili, hisia na mawazo yake yote kwa kile anachokifanya, huwa mbunifu, mtundu wa kufanya vitu vipya na kuleta ufanisi katika jamii inayotuzunguka," anaongeza.
Kwa sura hii, mwandishi anayejinadi kuandika kitabu hiki na hata vingine kadhaa muhimu kwa wajasirarimali anasema dhana ya ujasiriamali ni ule uwezo wa kutambua fursa za biashara haraka na uthubutu wa kuzitekeleza zinapojitokeza.
Anasema hiyo ni hali ya kuwa na msukumo wa kukamilisha malengo na anapinga wazo la baadhi ya watu wanaodhani kuanzisha biashara pekee kunamfanya mtu kuwa mjasiriamali.
“Ujasiriamali ni zaidi ya kuanzisha biashara na hata wale walioajiriwa wanaweza kuwa wajasirimali kwenye kazi zao kwa kuwa wabunifu na kuwa wanapenda kuleta na kuanzisha mbinu mpya zitakazorahisisha kazi zao na kuleta ufanisi," anabainisha katika moja ya maelezo yake.
Anatuasa kwa kiwango kikubwa kuepuka kuwa wabangaizaji na wahangaikaji na bado tukitaka kuitwa wajasiriamali. Anawaeleza hawa kama watu wasio na malengo, wafanyabiashara kiujanja ujanja alimradi mkono uende kinywani.
Japo anakiri kuwa zipo baadhi ya jamii zenye historia nzuri ya ujasirimali ikiwemo dhana hii kuwa kama waliozaliwa nayo, bado anapinga mawazo ya baadhi ya watu kuwa wengine hawawezi kufanikiwa katika ujasiriamali.
Tunajipima vipi kujua kama nasi ni wajasiriamali au ndiyo wale tunaobangaiza kama walivyo wengi wa wanaojiita wajasiriamali hivi leo? Tambwe anataja sifa kadhaa ikiwemo kuwa na maarifa ya biashara anayoifanya mtu hali itakayomfanya pamoja na mambo mengine, ajue mazingira ya biashara yake, sheria, mwelekeo wa uchumi na masuala ya kifedha.
Sifa nyingine muhimu ni utaalamu wa biashara kama kutunza kumbukumbu, kufanya utafiti na kuyatumia matokeo yake, jinsi ya kushawishi wateja na wazalishaji na uwezo wa kufanya shughuli za kimasoko.
Nyingine ni hulka ya utafutaji, mtu wa vitendo, mtu wa malengo, anayejiamini, ana nidhamu, anaona mbali, ni king’ang’anizi, mbunifu, anafanya kazi kwa bidii, mwenye malengo ya muda mrefu, ana uwezo wa kutatua matatizo, anashughulikia matatizo na kuyakabili, anatumia taarifa azipatazo.
Sifa nyingine ni mwanzilishi wa mambo, mbeba majukumu, anapenda mashindano na wengine, anakubali na kuwajibika kwa matokeo, ni mkweli na mwaminifu, mtu wa faida na mtafuta mafanikio.
Ni dhahiri kwa maelezo haya umepata mwanga mwingine mzuri kuhusu dhana ya ujasiriamali. Haya ni maelezo ya mmoja wa wataalamu ambao mara kwa mara nimekuwa nikisisitiza ama kuwaona kwa ushauri au basi tusome machapisho yao yatakayotuwezesha kubadili mienendo yetu ya biashara na maisha yetu kwa jumla.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment