Thursday, June 21, 2012

Kwa nini mkulima Mwamwindi alimpiga risasi RC Dk. Kleruu?

Maggid Mjengwa
IRINGA ina historia ndefu ya harakati za mapambano ya kudai uhuru. Harakati za kijamii, kisiasa na kiuchumi. Wakati huu nchi yetu ikielekea kwenye kuadhimisha miaka 50 ya uhuru si vibaya tukakumbushana tulikotoka ili tuweze kuelewa tulipo sasa na tunakokwenda.
Hakika, simulizi ya Mkulima Saidi Mwamwindi aliyepambana na dola ni moja ya simulizi zilizowagusa wasomaji wangu wengi.
Ni simulizi iliyonifanya nihamasike kutafuta habari zaidi za Watanzania mfano wa Mwamwindi ambao, hata kama huko nyuma jamii ilitakiwa iwaone kama wasaliti, lakini, jamii si mkusanyiko wa watu wajinga. Kuna walioulewa ukweli, waliamua kukaa kimya. Na wakati mwingine walisema na hata kuimba kile ambacho watawala waliwataka waimbe na kusema.
Hata hivyo, mioyoyoni mwao, waliujua ukweli. Kuna walioimba huku wakilia mioyoni. Kuna waliosema huku wakisononeka mioyoni.
 
Huu ni wakati wa kujaribu kuusema ukweli ili tuweze kwenda mbele kama taifa.
Simulizi ya mkulima, Saidi Mwamwindi ni jaribio la kuutafuta ukweli huo. Na hii ni simulizi shirikishi yenye kukukaribisha ewe msomaji, uje na unachokijua juu ya kilichotokea zaidi ya miaka 40 iliyopita.
 
Mwamwindi ni kielelezo cha hali iliyokuwepo wakati huo. Mathalan, utekelezaji wa Sera za Ujamaa na kilimo cha ushirika ulitakiwa utekelezwe kwa kuzingatia mazingira ya kila mahala.
 
Inakuwaje basi kwa mkuu wa nchi unapomweka mkuu wa mkoa kijana anayeanza kwa kuwahutubia wakulima wakubwa mfano wa Saidi Mwamwindi habari za kilimo cha heka nne nne?
 
Wakulima ambao tayari, hata kabla ya Uhuru wameweza kuwa na matreka na hata kuanzisha ushirika wao wa wakulima. Ndio, inawezekana vipi kwa mkulima wa shamba la ekari mia nne akajisikia furaha kuwa kwenye mkutano na mkuu wa mkoa anayezungumzia kilimo cha ekari nne nne? Mbinu gani ya kiuongozi ilihitajika ili kumfanya mkulima mkubwa kama Mwamwindi ashiriki na kuwasaidia wakulima wadogo wadogo?
 
Na hapa inaanza simulizi ya Mwamwindi;
Mwanzoni mwa miaka ya 1970 mkulima, Saidi Mwamwindi alikabiliwa na shitaka la kumwua Dk Wilbert Kleruu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa wakati huo.
 
Mshitakiwa Mwamwindi alijitetea kuwa alipokuwa anamwua marehemu Kleruu alirukwa na akili . Hivyo, akapotewa na fahamu ya kuweza kuelewa kile alichokuwa anakitenda. Jaji Onyiuke kutoka Nigeria aliukataa utetezi wa Mwamwindi kwa kutilia maanani kwamba baada ya mshitakiwa kughadhibishwa ndipo alipokwenda ndani kuchukua bunduki ambayo aliitumia kumwua marehemu.
 
Oktoba mwaka 2010, nikiwa njiani kwenda Dodoma na Arusha, nilipita kijijini Isimani. Hapo ndipo yalipokuwa makazi ya Mwamwindi. Ni umbali wa kilomita zipatazo 40 kutoka Iringa Mjini. Kijijini Isimani Saidi Mwamwindi bado anaonekana ni shujaa kwa kukataa kunyanyaswa na Mkuu wa Mkoa.
 
Inasimuliwa, kuwa ilikuwa siku ya Jumapili, tena siku ya Krismasi, pale Mkuu wa Mkoa, Dk Kleruu, alipofika Isimani na kumkemea Mwamwindi mbele ya wake zake kwa vile alifanya kazi za shamba siku ya Sikukuu.
 
Inasimuliwa, kuwa Dk. Kleruu alifikia hata hatua ya kuanza kudhihaki makaburi ya mababu zake Mwamwindi akimwambia Mwamwindi: “Humu ndimo mlimozika mirija yenu”. Alifanya hivyo huku akionyesha makaburi yake kwa kutumia fimbo aliyoshika mkononi. Mwamwindi alikasirika sana. Akaficha hasira yake.
 
Kutoka makaburini, Mwamwindi aliongozana na Kleruu hadi nje ya nyumba yake. Akamwomba Mkuu huyo wa Mkoa abaki nje. Mwamwindi akaingia ndani chumbani.
 
Mke wake Mwamwindi alimwona mume wake akichukua bunduki na kusimama dirishani. Mama huyo alidhani mumewe amepanga kwenda kuwinda. Kumbe, Mwamwindi alitokea dirishani na kumwelekea Kleruu aliyedhani Mwamwindi angetoka nje kwa kupitia mlangoni.
 
Basi, Mwamwindi akamlenga Mkuu wa Mkoa sawa kichwani. Dk kleruu alinyoosha mikono juu na kuomba asemehewe. Mwamwindi alikaa kimya. Kisha akafyatua risasi. Kishindo kilisikika kijijini. Baada ya hapo, kwa mikono yake, Mwamwindi akaubeba mwili wa Mkuu wa Mkoa na kuuweka nyuma ya boneti ya gari alilojia mkuu huyo wa mkoa.
 
Mwamwindi alichukua kofia ya pama aliyovaa Kleruu. Akaivaa kichwani na kuanza kuendesha gari hilo hadi kituo cha polisi Iringa. Waliokutana na Mwamwindi njiani walimshangaa akiendesha gari hilo la Mkuu wa Mkoa akiwa amevalia kofia ya mkuu huyo. Hatimaye Mwamwindi akafika kituo cha Polisi.
 
Akatoka na kwenda mapokezi. Hapo akaripoti tukio kwa kutamka; " Nendeni mkamchukue mbwa wenu nyuma ya gari!"
 
Tukio lile bado linatuachia maswali? Je, ni kwanini Dk Kleruu alikwenda nyumbani kwa Mwamwindi siku ya Jumapili na hususan siku ya Krismasi?
 
Je, yawezekana Mwamwindi na Dk Kleruu walikuwa na ugomvi mwingine kabla ya tukio?
 
Kuna waliokuwepo na wanasimulia kana kwamba ilikuwa ni jana tu. Mmoja wa watu hao ni mwana wa Mwamwindi aitwaye Amani Mwamwindi ambaye ndiye Meya wa Manispaa ya Iringa kwa sasa. Amani Mwamwindi anakumbuka nini juu ya siku hiyo?
 
MKE wake Mwamwindi alimwona mume wake akichukua bunduki na kusimama dirishani. Mama huyo alidhani mumewe amepanga kwenda kuwinda. Kumbe, Mwamwindi alitokea dirishani na kumwelekea Kleruu, aliyedhani Mwamwindi angetoka nje kwa kupitia mlangoni.
 
Basi, Mwamwindi akamlenga Mkuu wa Mkoa kichwani. Dk. Kleruu alinyosha mikono juu na kuomba asemehewe. Mwamwindi alikaa kimya. Kisha akafyatua risasi. Kishindo kilisikika kijijini. Baada ya hapo, kwa mikono yake, Mwamwindi akaubeba mwili wa Mkuu wa Mkoa na kuuweka nyuma ya boneti ya gari alilotumia mkuu huyo wa mkoa.
 
Mwamwindi alichukua kofia ya pama aliyovaa Kleruu. Akaivaa kichwani na kuanza kuendesha gari hilo hadi kituo cha polisi Iringa. Waliokutana na Mwamwindi njiani walimshangaa akiendesha gari hilo la Mkuu wa Mkoa akiwa amevalia kofia ya mkuu huyo. Hatimaye Mwamwindi akafika kituo cha Polisi.
 
Akatoka na kwenda mapokezi. Hapo akaripoti tukio kwa kutamka; "Nendeni mkamchukue mbwa wenu nyuma ya gari!".
 
Tukio lile bado linatuachia maswali? Je, ni kwa nini Dk. Kleruu alikwenda nyumbani kwa Mwamwindi siku ya Jumapili, tena siku ya Krismasi?
 
Je, yawezekana Mwamwindi na Dk. Kleruu walikuwa na ugomvi mwingine kabla ya tukio? Tuendelee na simulizi hii kama ifuatavyo.
 
“Niliporudi nyumbani kutoka Ifunda nikazikuta habari hizo mbaya. Nikaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Mzee pale Mshindo. Nikawakuta akina mama wanalia.
 
“Ilikuwa ni kilio. Hiyo bado ilikuwa, siku ya Krismasi. Nikauliza; kuna aliyekwenda kumwona baba pale polisi? Jibu likawa hapana. Nikaenda moja kwa moja polisi ili nikamwone baba na nimsikie kauli yake.
 
Nilipofika polisi nikaanza kujieleza kwa askari polisi kuomba ruhusa ya kuongea na Mzee. Wakati nikifanya hivyo mzee nae alisikia sauti yangu. Akatamka; ” Mwanangu huyo, mruhusu niongee nae”. Nikaongea na Mzee.
 
“Niliweza kuongea na Mzee na kupata picha ya kilichotokea. Niliondoka kurudi nyumbani. Habari zilishasambaa. Hali haikuwa nzuri. Mji wa Iringa ulitulia sana. Halafu ukaja mtikisiko mkubwa. Wazee wengi walioishi mjini na waliokuwa wakilima na Mzee kule Isimani walisombwa na vyombo vya usalama.”
 
Je, ni kina nani hao? Namwuliza Amani Mwamwindi. Anajibu; “Mzee kama Ibrahim Khalili, Mursali na wengine. Watu kama 30 hivi walisombwa na kupelekwa sehemu mbalimbali za nchi. Kuna waliopelekwa Mwanza, Shinyanga hata Zanzibar. Kwa namna fulani walitenganishwa katika sehemu hizo.”
 
Je, na wewe ulikumbwa na msukosuko huo? “Ndio, hata mimi nilihojiwa ingawa niliachwa niendelee na kazi zangu. Kumbuka nilikuwa kijana wa miaka 21 tu, na siku ya tukio nilikuwa shambani kwangu Ifunda. Hapa nyumbani kwangu kulikuwa na askari wa FFU muda wote. Katika kuhojiwa kwangu maswali mengine yalikuwa hayana msingi.
 
Kwa mfano, niliulizwa; Mzee alipokuja hapa kwako kutoka Isimani siku ya tukio alitaka kukwambia nini? Sasa, mimi hakunikuta nyumbani na hatukuongea, nitajuaje alichotaka kuniambia siku hiyo? Anaeleza Amani Mwamwindi, akionyesha kushangaa, hata hii leo.
 
Je, kwa wakati huo, wewe na familia yenu mlihisi kutengwa na jamii kutokana na kitendo alichofanya Mzee Mwamwindi? Namwuliza. Namwona Amani Mwamwindi akionyesha kuguswa sana na swali hili.
 
“Tulikuwa na wakati mgumu sana kama familia. Kibaya zaidi kwetu ilikuwa ni kuingia kwenye uhasama na ndugu wa jamaa ambao wazee wao walisombwa na vyombo vya usalama na kwenda kusikojulikana.
 
“Kwao waliamini kama isingekuwa Mzee wetu Mwamwindi kufanya tendo lile, basi, wazee wao wangebaki salama na kuendelea na shughuli zao za kilimo. Hivyo basi tulisakamwa na wengine ambao ni ndugu zetu.”
 
Mlifanyaje kuikabiili hali hiyo? “Tulifikia uamuzi mimi niende Dodoma kwenye gereza alikokuwa Mzee Mwamwindi. Niende nikamjulishe baba juu ya hali iliyotokea huku nyumbani. Kwamba tuna uhasama na jamaa wa waliosombwa na vyombo vya dola.
 
Nilipata kibali cha DC hapa Iringa. Kibali cha kwenda kumwona Mzee kule Dodoma. Nilipofika Dodoma nikaonana naye. Tukazungumza. Nikamwambia shida ya nyumbani. Alisikitika sana.
 
Akaniuliza; “Sasa tufanyeje?”. Nikamshauri aandike barua kwenda kwa Nyerere kumwomba atusaidie. Baba aliandika barua siku hiyo hiyo. Alimwandikia Nyerere kumwambia na kumhakikishia kuwa ni yeye Said Mwamwindi na si mtu mwingine yeyote aliyehusika na tendo alilofanya; kumpiga risasi na kumuua Kleruu.
 
Barua ile ilifika kwa Nyerere, na haukupita muda mrefu, wazee wale wakulima wa Isimani waliachiwa huru na kurudishwa Iringa. ”
 
Je, hali ya uhusiano na waliowachukia ilibadilika na kuwa njema baada ya wazee hao kurudi Iringa? Namuuliza Mzee Amani Mwamwindi.
 
“Ndio, kabisa. Hali ikawa shwari. ” Je, wazee wale wakulima wa Isimani walirudi na kuendelea na kazi zao za kilimo?
 
“Niseme kuwa walirudi Iringa wakiwa wameathirika kisaikolojia. Kuna ambao hawakutaka kabisa kurudi tena Isimani. Baadhi yao hawakuishi muda mrefu, walifariki. Sijui nini kiliwatokea.”
 
Je, unafikiri Iringa ingekuwaje kama tukio lile la siku ya Krismasi mwaka 1971 lisingetokea?
 
“Naamini kabisa, Iringa isingekuwa kama ilivyo sasa. Ingeendelea sana. Unajua kulikuwa hakuna mahala pengine katika nchi hii ambapo kulikuwa kunazalishwa mahindi kushinda Isimani.
 
“Mzee na wenzake walilima ekari nyingi sana. Naamini wangelima zaidi. Walianza kujijenga na hata waliunda ushirika wao. Tukio lile lilisimamisha kasi ya kilimo Isimani. Ni kama laana fulani vile, maana, tangu wakati ule mvua zimekuwa za taabu Isimani,” anasema Mzee Amani Mwamwindi. Kisha namwuliza tena.
 
“Nilifika pale nyumbani kwenu Isimani, nikaona mnara wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu, kwanza nilifikiri ni kumbukumbu ya Mwamwindi. Je, unajisikiaje kuona nyumbani kwenu kuna mnara wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu na si ya baba yenu?”
 
“Mimi naona ni sawa kabisa kwa mnara ule kuwa pale”. Ananijibu Mzee Amani Mwamwindi huku akionyesha kuchangamka. Anaendelea.
 
“Unajua hata Nyerere alipofika Isimani wakati fulani aliuliza; ” Hivi huu mnara ni wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu au Said Mwamwindi?” Nyerere alikuwa na maana yake.” Ananiambia Mzee Amani Mwamwindi. Kuna kitu anataka kufafanua, anasita. Namwacha aendelee kutafakari.
 
Kisha ananiuliza swali gumu. Nabaini ni mara ya kwanza katika mazungumzo yetu ameamua kunirushia swali. Kwa mtazamo wangu ni swali la kifalsafa. Mzee Amani Mwamwindi ananiuliza; “Bwana Mjengwa, mche unaochipua ardhini unahitaji kumwagiliwa maji ili uendelee kuchipua. Ukisimama vema unauacha ukue wenyewe. Na je, ukishakua na kukomaa unaufanyaje?”. Mzee Amani Mwamwindi ananiuliza huku akinitazama usoni.
 
Naam, ni swali gumu lenye kunihitaji, sio tu kufikiri, bali kufikiri kwa bidii. Jibu lake lazima lifuatiwe na majadala.
 
Ewe msomaji mpendwa, kabla sijaingia kwenye nilichomjibu Mzee Amani Mwamwindi na mwendelezo wa mazungumzo yetu nakutoa nje ya nyumba ya Amani Mwamwindi pale Mlandege.
 
Maana, mpaka kufikia hapa tumemsikia Mzee Amani Mwamwindi, kama mwanafamilia ya marehemu Said Mwamwindi akisimulia kilichotokea.
 
Iringa Mjini kuna mmoja wa wazee wa siku nyingi, Mzee Omar Mselem Nzowa. Huyu ni mmoja wa wazee walionipokea nilipofika Iringa miaka sita iliyopita. Mzee Nzowa alimfahamu marehemu Said Mwamwindi, baba wa Amani Mwamwindi . Jumamosi moja ya mwezi Novemba, 2010 naamua kwenda nyumbani kwa Mzee Nzowa.
 
Tumekaa sebuleni, mimi na Mzee Nzowa. Tunaongea huku tukipata kikombe cha chai.
 
“Ndio Mzee wangu, nisimulie habari za Marehemu Said Mwamwindi, maana nimekutana na mwanae, Amani Mwamwindi, naye kuna aliyonisimulia. Je, ulipata kukutana na marehemu Said Mwamwindi wakati wa uhai wake?”
 
Aah! Said Mwamwindi, nilimfahamu sana." Ananiambia huku anacheka. Kisha anaendelea kusema;
 
"Unajua, tulikua naye hapa mjini. Na hata siku ile ya tukio mimi na vijana wenzangu wa wakati ule tulikuwa tunacheza bao pale Miyomboni, tulishangaa sana kumwona Said amesimamisha gari la Dk. Kleruu nyumbani kwa shangazi yake na huku amevalia pama la Dk. Kleruu.
 
“Nakumbuka alitunyoshea mkono akiwa anatabasamu. Tulizungumza kwa kushangaa, tukajiuliza; jamani hivi Serikali leo imempa Said Mwamwindi gari atembelee? Yakafuata yaliyofuatia. Maggid, ninayo mengi ya kukusimulia kwa yaliyotokea katika wakati ule….” Anasema Mzee Nzowa.
 
“Ndiyo, nilimfahamu Said, na jina lake hasa aliitwa Said Abdalah Siulanga Mwamwindi. Nyumba ya baba yake ilikuwa pale Mshindo karibu na ukumbi wa Welfare. Baba yake aliwahi kuwa Jumbe enzi za ukoloni. Kwa kweli Said alikuwa ni mtu wa kilimo na nakumbuka alianzia kwenye magari. Alikuwa dereva kabla hajaenda kufyeka mapori ya kilimo kule Isimani.”
 
Je, unakumbuka wajihi wa marehemu Said Mwamwindi?
 
“Ah, yule bwana alikuwa pande la jitu. Mrefu na aliyeshiba hasa. Ukimwona utasema huyu jamaa amekaa kiutemi-utemi. Yaani, unavyoomwona mwanae, Amani Mwamwindi sasa, ndivyo kwa kiasi kikubwa alivyoonekana Said Mwamwindi. Wamefanana sana."
 
Na je, Dk.Kleruu, alikuwa mtu wa namna gani, wajihi wake na mengineyo?
 
”Alaa, Dk.Kleruu. Tulikuwa vijana wakati ule, na yeye alikuwa Mkuu wa Mkoa kijana hapa Iringa. Nafikiri alichukua nafasi ya Bw. Chamshama. Alikuwa mfupi kidogo. Ila bwana, alikuwa machachari sana . Nikisema ’machachari’ nadhani unanielewa.
 
Haraka sana tuliona dalili kuwa Dk.Kleruu asingekuwa na wakati mzuri hapa Iringa.
 
Alianza mapema sana kuonyesha tabia za ubwana na hata kunyanyasa aliowaongoza. Na katika hao aliowaongoza, kulikuwa na watu wazima waliomzidi umri. Watu wenye hekima na busara kumzidi yeye, ingawa hawakusoma elimu ya darasani.”
 
Je, unaweza kutoka mfano wa ’ubwana’ mkubwa wa Dk.Kleruu aliouonyesha wakati huo?
 
”Iko mifano mingi, na ukweli Dk.Kleruu alisemwa vibaya katika midomo ya watu hapa Iringa. Ilifika mahala dereva akilipiga overtake gari la Dk.Kleruu hapa Iringa, basi, atasimamishwa na anaweza kuzabwa vibao na Kleruu mwenyewe. Aah! Jamaa yule alikuwa mbabe bwana!” Anasema Mzee Omary Nzowa huku akicheka kwa sauti. Kisha anaendelea.
”Unajua Dk.Kleruu alitokea Mtwara kabla ya kuja Iringa. Sasa kuna wakati alitamka; 'Hamnijui mimi, kawaulizeni watu wa Mtwara!' Sasa hayo si maneno ya kuwaambia watu wa Iringa, na hata mahali pengine popote,” akisimulia zaidi.
”Na nikwambie kitu kimoja Maggid, muhimu katika maisha ni kuishi vema na watu. Hata kama ni kiongozi, huwezi kufanikiwa katika kazi yako kama huna mahusiano mazuri na unaowaongoza. Na hata katika maisha ya kawaida, unaweza kuingia katika misukosuko isiyo ya lazima kama huna mahusiano mazuri na wenzako katika jamii.
”Nitakupa mfano hai unaonihusu mimi. Mwishoni mwa miaka ya 50 nilikamatwa nyumbani kwa kutokulipa kodi ya kichwa. Tulikuwa bado kwenye utawala wa mkoloni. Nilikuwa nadaiwa shilingi saba tu. Sikuwa nazo.
”Basi, nikaambiwa na askari wa kodi tuongozane hadi ofisini kwa DC. Tena walinifunga kamba mikononi. Nilifahamu, huko kwa DC ningeishia kuchapwa bakora na hata kuwekwa ndani. Unajua Maggid enzi hizo damu ilikuwa ikichemka na sisi vijana ndio tuliokuwa tukionekana kuiunga mkono TANU, ” ananiambia Mzee Nzowa akikumbuka enzi za ujana wake.
”Sasa basi, wakati tunakwenda kwa DC, niliwaomba sana wale askari wa kodi. Walikuwa Waafrika wenzetu. Nikawaambia, jamani ee, tafadhali tupite njia hii ya sokoni. Ni soko lile la zamani ambalo mpaka leo hii bado linatumika. Askari walikubali wakidhani nimechagua mwenyewe njia nitakayoonekana na watu na hivyo kujidhalilisha mwenyewe. Kumbe, mimi nilikuwa na maana yangu.
Tulipofika eneo la sokoni nikasikia jamaa zangu wakiuliza kwa sauti; ” Omary shida gani?”. Nikajibu kwa sauti; ” Kodi, shilingi 7!”. Basi, huwezi kuamini, hata kabla sijamaliza soko, vijana wale wa sokoni walichangishana. Shilingi saba zikapatikana. Kodi ile nikalipa na nikaachiwa huru. Pointi yangu hapo ni umuhimu wa mahusiano mema na watu.”
Je, unafikiri ni kwanini Dk. Kleruu alipata tabu sana kufanya kazi na watu wa Iringa?
Anasema Mzee Nzowa: ” Mi nadhani Kleruu, kwa jinsi alivyokuwa, angepata tabu kufanya kazi mahali po pote pale. Tatizo ni ile hali ya kutanguliza ubwana na kuwadharau wananchi. Hakika wakati ule Mwalimu Julius Nyerere alipata tabu sana na namna ya ku-deal na viongozi kama akina Kleruu. Kumbuka ,Tanzania kama nchi ilikuwa taifa changa sana. Hatukuwa na wasomi wengi. Nilimfahamu Nyerere, hili la Kleruu lilimsumbua sana Mwalimu.
”Nikwambie Maggid, Ujamaa na Kujitegemea kama itikadi na sera za Mwalimu haukuwa tatizo. Tatizo lilikuwa kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya utekelezaji. Hawa hawakuwa wanasiasa, wakati mwingine walionekana kama Wanyapara. Mwalimu wakati ule hakujua kila kitu kuhusu watu aliowateua kumsaidia.
”Ni kweli Mwalimu alitia saini hukumu ya kunyongwa kwa Mwamwindi, lakini naamini hakufurahia, bali hali ya wakati ule ilimlazimisha kufanya vile.
”Sisi tuliomfahamu Mwalimu tunajua kuwa hukumu ile ni moja ya maamuzi magumu yaliyomsononesha sana Mwalimu. Unajua wakati ule kuna Wakuu wa Mikoa waliojenga hoja, kuwa kama Mwamwindi kwa tendo lile asingepata adhabu ile, basi utendaji wao wa kazi mikoani ungekuwa mgumu. Ndiyo, hoja hizo ziliibuka. Kwa kiongozi wa nchi ni mtihani. Siyasemi haya kumtetea Mwalimu bali ni kutambua ukweli kuwa Mwalimu alikuwa ni binadamu kama wewe na mimi.”
Unasema ulimfahamu Nyerere na kwamba unaamini kwa wakati ule tatizo kwa Mwalimu Nyerere ilikuwa kwa baadhi ya aliowapa dhamana ya kumsaidia katika utekelezaji. Je, Mwalimu aliwahi kulizungumza jambo hili nawe ukamsikia?
”Huo ndio ukweli. Mimi nimekuwa katika chama (TANU) tangu mwaka 1956. Kadi yangu ya uanachama wa TANU niliikatia Mbeya. Ni Nyerere mwenyewe, kwa mkono wake, pale Mbeya, mwaka 1956 alinijazia kadi yangu ya TANU. Alianza na Kanali Ayoub Simba ikaja ya kwangu.
 
”Hata leo, ukiangalia namba za kadi ya TANU ya Kanali Ayoub Simba na ya kwangu zinafuatana. Tulikuwa bado vijana sana, na Mwalimu alifanya mwenyewe kazi ya kuhamasisha vijana kuingia TANU. Mwenzangu Ayoub yeye akaja akaingia jeshini , akafikia mpaka cheo cha ukanali, akawa mbunge pia, kule Mafia. Yule ni kada wa siku nyingi.
”Sasa nimepata kumsikia Mwalimu akiongea kuhusu hili la uongozi? Kwa kweli si mara moja. Nimemsikia Mwalimu akitamka, kuwa njia iliyo nzuri sana ya kumsaidia katika uongozi wake ni kwa tulio karibu na watu kumwambia moja kwa moja juu ya mazuri na mabaya wanayofanya wateule wake.
”Kwamba ni hatari wananchi wakianza ama kuchoka kulalamika au kuwaogopa viongozi wao. Unajua Mwalimu hakuishia tu kutumia watu wa Usalama wa Taifa, aliwatumia pia watu wa kawaida kupata taarifa sahihi.” Mzee, turudi kwenye kilichotokea kule Isimani, inasemekana kulikuwa na mtikisiko mkubwa hapa Iringa baada ya Dk.Kleruu kupigwa risasi na Mwamwindi. Je, hali ilikuwaje hasa?
” Ni sahihi, hali ilikuwa ngumu. Wengi tuliathirika na mkasa ule, kwa namna moja au nyingine. Unajua ilifika mahali wakati ule mtu ukigongewa mlango usiku, basi, unavaa kabisa, shati, suruali na viatu, maana huenda ukifungua mlango usirudi tena kitandani kwako!”
Hivi Iringa ya wakati ule ilionekaje, unakumbuka?
 
Anajibu Mzee Nzowa: ” Mji huu wa Iringa ulikuwa mdogo sana, wengi tulikuwa tunajuana. Hebu ngoja nipekue kwenye kabati langu kuona kama nina picha za zamani”. Mzee Nzowa anainuka kitini. Anakwenda kupekua picha za zamani. Nasubiri kwa shauku.
 
Wakati tukimsubiri Mzee Nzowa , Jumatatu moja usiku napokea simu kutoka Uingereza;

”E bwana Maggid, niko Uingereza, nafuatilia kisa hiki cha Mwamwindi na Dk. Kleruu. Mimi nilikuwa kijijini Nyang’olo wakati wa tukio lile. Ni kijiji cha jirani na alikoishi Said Mwamwindi. Nilikuwa na miaka kumi. Nakumbuka mambo mengi sana , hata Dk. Kleruu nilimwona, alipenda sana kuja Nyang’olo. Sasa unasikia....”
Hivi Iringa ya wakati ule ilionekanaje, unakumbuka? Namwuliza Mzee Nzowa.” Mji huu wa Iringa ulikuwa mdogo sana, wengi tulikuwa tunajuana. Hebu ngoja nipekue kwenye kabati langu kuona kama nina picha za zamani”. Mzee Nzowa anainuka kitini. Anakwenda kupekua picha za zamani. Nasubiri kwa shauku.
Wakati tukimsubiri Mzee Nzowa, Jumatatu moja usiku napokea simu kutoka Uingereza; “Ebwana Maggid, niko Uingereza, nafuatilia kisa hiki cha Mwamwindi na Dk. Kleruu. Mimi nilikuwa kijijini Nyang’olo wakati wa tukio lile. Ni kijiji cha jirani na alikoishi marehemu Said Mwamwindi. Nilikuwa na miaka 10. Nakumbuka mambo mengi sana, hata Dk. Kleruu nilimwona, alipenda sana kuja Nyang’olo. Sasa unasikia....”
“Dk. Kleruu alikuwa akija na gari lake. Nyang’olo ni mji wa barabarani. Unajua ndio ilikuwa njia kuu ya kwenda Dodoma mpaka Arusha. Kulikuwa na biashara sana. Kulikuwa na wasomali hata waarabu. Nakumbuka Dk. Kleruu alikuwa akishika kifimbo chake na kuwafokea wazee juu ya mambo ya maendeleo. Kwa kweli wazee wa Nyang’olo hawakumpenda Kleruu,” anasema msomaji huyu ambaye sasa ana miaka 50 na anaishi nchini Uingereza.
Na wakati tukiendelea na simulizi hii ya Mwamwindi zimenifikia habari mbaya. Ni taarifa ya msiba wa Mzee Augustino Hongole Mzee Hongole ambaye, hadi kifo chake alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri wa gazeti la Kwanza Jamii, Njombe amefariki majuma mawili yaliyopita. Amezikwa kijijini kwao Lupembe., Njombe.
Kwangu mimi, Mzee Hongole ni mmoja wa wazee waliochangia sana katika kuifanya simulizi hii iwe na maana kubwa. Maana, katika utafiti wangu juu ya kisa hiki cha Mwamwindi na Mkuu wa Mkoa Dk. Kleruu, nimepata bahati ya kufanya mazungumzo marefu ya ana kwa ana na hata kwa njia ya simu na marehemu Mzee Hongole.
Na kweli mwandishi wa habari mwandamizi wa magazeti ya HabariLeo na Daily News, Beda Msimbe ndiye aliyenisisitiza sana umuhimu wa kumhoji Mzee Hongole huku kaka yangu Msimbe akisema; “Usichelewe sana, maana wazee hao ndio wanaondoka taratibu”.
Na hakika nimefanya jitihada za ziada za kupokea simulizi za Mzee Hongole juu ya anachokikumbuka katika wakati ule wa tukio.
Na katika hili la simulizi ya Mwamwindi mchango wa marehemu Mzee Hongole ni mkubwa sana. Mzee Hongole amechangia kutoa elimu kubwa ya kimapokeo. Hakika, nina maelezo mengi ya Mzee Hongole ambayo nimeyahifadhi kwa simulizi za baadae.
Huko nyuma nimewahi kusimulia yafuatayo niliyoyapokea kutoka kwa Mzee Hongole juu ya tukio la mkulima Mwamwindi kumpiga risasi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu.
Mzee Hongole aliyepata kuwa mwandishi wa habari kijana sana wakati wa tukio la Mwamwindi kumuua Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu lililopotokea anasema; "Ndio kwanza nilikuwa nimepangiwa kufanya kazi kama mwandishi wa habari kwenye gazeti la Kanisa pale Iringa.
“Lilikuwa tukio kubwa sana. Kama mwandishi nilitamani kuandika kilichotokea na kupata maoni ya watu wa Iringa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla. Kwa wakati ule mfumo haukuruhusu kitu kama hicho. Mwamwindi story was an embargoed one (Stori ya Mwamwindi ilikuwa haiandikiki). Lakini nataka kukwambia: "Watu wengi wa Iringa hawakumpenda Dk. Kleruu kutokana na unyanyasaji wake".
Mzee Hongole anazidi kusema; “Unajua wakati huo kulikuwa na hofu kubwa juu ya dola. Waliokuwa tayari kumtetea Mwamwindi hadharani walihofia kukamatwa na makachero. Na mimi kalamu yangu ikawa nzito kwa kuogopa jela.
Lakini, kikubwa ni kuwa watu wa kanda hii walikuwa wamoja katika kumuunga mkono Mwamwindi. Shida kubwa ilikuwa kwenye uUtekelezaji wa Azimio la Arusha. Utekelezaji ule kwa mtazamo wangu ulifanywa kimakosa katika maeneo mengi ya nchi ikiwamo kanda yetu hii. Wananchi hawakuulizwa wanataka nini. Walilazimishwa tu na viongozi.
Nakumbuka kule Ilembula kuna wanafunzi waliolazimishwa baada ya masomo waende wakapande miche ya kahawa kwenye shamba la kijiji. Wazazi hawakupenda kilimo cha kahawa, lakini, Serikali ilitaka walime kahawa. Basi, ikatokea, kwa wazazi kuwaambia watoto wao, kuwa wakifika shambani waigeuze miche ya kahawa. Wapande juu chini. Hivyo hawakupanda, walipandua,” anasema Mzee Hongole.
Mzee Hongole anaendelea kusema; “Unajua ni mazingira kama hayo ndio yaliyochangia uzalishaji upungue. Wananchi walijisikia kushurutishwa. Hawakufanya kazi kwa moyo. Na vyombo vya habari navyo havikuwa huru kuweza kuelezea hali halisi za wananchi. Hapa utaona jinsi tulivyokuwa, kama taifa, tukitoka kwenye reli. Maggid, nawaonea wivu sana katika wakati wenu huu kama wanahabari.
“Sisi tulisomea taaluma hii. Tena mimi nilipelekwa na Kanisa mpaka Sweden. Lakini, taaluma zetu zikaishia kufanya kazi ya kusifia Serikali tu, hata kwa mambo ya kipuuzi yaliyofanywa na baadhi ya viongozi. Wakati huo wa tukio la Mwamwindi watu wengi walikuwa na hamu ya kutaka kuujua ukweli. Lakini, sisi wanahabari tuliogopa hata kufika kijijini kwa Mwamwindi kuwahoji waliokuwepo siku ya tukio”
Mzee Hongole anasisitiza kwa kusema kuwa wakati umefika kwa Watanzania kuipitia upya historia yao. Hii itasaidia kuwafanya vijana wa kizazi hiki kujitambua. Watajenga mioyo ya uzalendo na kuwa tayari kuipigania nchi yao.
 
“Mimi nina shaka kuwa vijana wa siku hizi wamekosa kujiamini kwa vile hawajitambui. Hawaijui historia yao. Wana kiu ya kutaka kuifahamu historia yao. Ni kazi yenu nyinyi waandishi vijana kufanya tafiti juu ya historia yetu na kuisimulia,” anasema Mzee Augustino Hongole. . Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi, Amen.
UKIMWONA kwenye mitaa ya Iringa bado anatembea kwa hatua za kijeshi. Ni Mzee David Butinini. Alipata kuwa askari polisi na alishuhudia kwa macho yake, siku Mkulima Said Mwamwindi alipofika kituo cha Polisi Iringa akiwa na mwili wa marehemu Dk. Kleruu kwenye gari aliloendesha.
Dk. Kleruu alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliyeuawa na Mwamwindi kwa kupigwa risasi. Mzee David Butinini alikuwa pia mmoja wa mashahidi kwenye kesi ya mauaji iliyomkabili marehemu Mwamwindi.
 
Mzee David Butinini ni rafiki yangu wa muda mrefu. Jioni ya Jumapili moja tunakutana Soko Kuu Iringa. Namuuliza juu ya kumbukumbu zake ya kilichotokea miaka 40 iliyopita.
Tunazungumza huku kwa pamoja tukikiangalia kituo cha polisi kilicho mbele yetu na ambapo Mzee David Polisi alifanya kazi kama Polisi miaka 40 iliyopita.
“Unasikia Maggid, nilishuhudia kwa macho yangu. Nilikuwa bado kijana enzi hizo. Nilikuwa mwanamichezo pia. Nilikuwa kwenye kikosi cha polisi cha mpira wa miguu. Nakumbuka ilikuwa jioni ya Jumapili ya Krismasi . Ni kwenye saa kumi na moja hivi.
Tulikuwa kama askari watatu hivi tumevalia kiraia na tulisimama pale nje ya kituo,” Mzee David ananieleza huku akionionyesha kwa mkono mahali hapo.
Kelele za makuli wabeba mizigo sokoni zinatufanya mimi na Mzee Butinini tusisikilazane vema. Wote, kutokana na utamu wa simulizi hii tunajikuta tunasogea mbele kidogo na kusimama kando ya kibanda cha rafiki yangu Mwarami. Kijana anayeuza matunda Soko Kuu la Iringa.
 
“Unajua Maggid, Iringa ya wakati huo ilikuwa na watu wachache sana hapa katikati ya mji. Na magari nayo yalikuwa ya kuhesabika. Na Jumapili ile ya Krismasi ilikuwa tulivu kupita kiasi. Ghafla tukasikia muungurumo wa motokaa kama tulivyokuwa tukiyaita magari enzi hizo.
 
“Mita mia tano mbele yetu tukaliona gari likitokea kwenye mtaa huu tuliosimama. Ni Mtaa wa Jamatini wengine wanauita Uhindini. Na kama ilivyo sasa, na enzi hizo pia barabara hii ni one way. Gari zinakwenda njia moja tu.
 
Zinashuka kusini, hazipandi kaskazini.
 
Je, ni wakati gani mlibaini kuwa ni gari la mkuu wa mkoa? Namwuliza Mzee Butinini.
 
“Kwanza kama askari tukabaki tukijiuliza; kwa nini dereva wa gari linalokuja anavunja taratibu za barabarani? Lakini, gari lilipokaribia tukabaini haraka kuwa ni Peugeot 404 rangi ya buluu. Ni gari la mkuu wa mkoa. Na pembeni lilikuwa na maandishi ’ RC-Iringa’. Sikumbuki namba za usajili wa gari lile. Tukahisi kuwa mkuu wa mkoa amekuwa na dharura iliyomfanya avunje taratibu za barabarani,” anasema Mzee Butinini anayeonekana kuwa na kumbukumbu nzuri ya tukio kana kwamba lilitokea juzi tu.
 
Unasema mlihisi mkuu wa mkoa alikuwa na dharura fulani. Je, gari lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo gani na dereva wa gari alifunga wapi breki ya kwanza? Mbele ya kituo? Nyuma ya kituo au kando ya kituo? Namuuliza Mzee Butinini.
 
“Kwa kweli hata mwendo haukuwa wa kasi sana. Ni wa kawaida tu. Dereva alipunguza mwendo baada ya kupita kituo cha polisi. Akakata kulia na kufunga breki kando ya kituo pale kwenye ule mnara wa kumbukumbu ya askari waliopigana Vita Kuu ya Dunia,” anajibu.
 
Nini kikatokea? Namuuliza tena Mzee Butinini ambaye wakati huo alikuwa askari kijana sana.
 
“Tukamuona mtu ambaye hakuwa mkuu wa mkoa akifungua mlango na kuelekea mlango wa mapokezi. Alikuwa mtu mrefu, mnene kiasi na nakumbuka alikuwa na sharubu kiasi.”
 
Namkatisha Mzee Butinini kwa kumwuliza; kwa vile mlifahamu kuwa gari lilikuwa la mkuu wa mkoa na dereva hakuwa mkuu wa mkoa wala dereva wake, hamkuona kuwa ni jambo la kushangaza? Mlichukua hatua gani kabla dereva huyo hajafika ‘kaunta’ ya mapokezi pale polisi?
 
“Bwana Maggid, kila kitu kilikuwa cha kushangaza na kilikwenda haraka sana. Maana, yule Bwana Mwamwindi alikwenda moja kwa moja kaunta na pale alikutana na afande Mbete, nakumbuka alikuwa kijana wa Zanzibar. Mara tukamwona akitoka tena na kurudi kwenye gari. Akachukua bunduki na kuja nayo tena kaunta ya polisi. Alikwenda ‘kuisarenda’ kwa maana ya kuikabidhi,” anasema Mzee Butinini.
 
Je, nyinyi askari mliokuwa nje mlibaki hapo hapo na umesema mlivaa kiraia. Je, mlikuwa makachero?
 
“Kazi ya uaskari ni kazi ya ukachero pia, lakini kwamba tulivaa kiraia siku ile ni kwa vile ilikuwa Jumapili na tena siku ya Krisimas. Na kwa kweli hatukuwa na pa kwenda. Tulikuwa tukijiandaa kusafiri kwenda Moshi kesho yake. Nilikuwa kwenye kikosi cha mpira na tulikuwa na mashindano ya polisi kule Moshi.
 
Kwa sisi askari vijana kituo cha polisi ilikuwa ni kama kijiwe pia cha kukutania na kupiga stori tukiwa nje. Si unaona hata sasa hivi kuna askari vijana pale kituoni wamevalia kiraia wanapiga gumzo. Na sisi ilikuwa hivyo hivyo enzi zetu,” anasema Mzee Butinini huku akinionyesha askari wale vijana nje ya Kituo cha Polisi Iringa, siku ile ya Jumapili jioni.
 
Namrudisha tena Mzee Butunini kwenye reli ya mazungumzo kwa kumkumbushia swali langu; Je, mlifanya nini baada ya kumwona Mwamwindi akiwapita na bunduki kwenda kukabidhi kituoni?
 
“Ahaa! Tuliingiwa na shauku ya kipolisi ya kutaka kwenda kuichunguza gari ya mkuu wa mkoa. Nakumbuka wakati Mwamwindi akiandikisha maelezo yake tuliizunguka gari ile ya mkuu wa mkoa kugagua kilicho ndani.
 
“Mimi nilikuwa wa kwanza kumtambua Mkuu wa Mkoa, Dk. Kleruu aliyekuwa amelazwa kiti cha nyuma akiwa amevalia overall nyeusi na miwani machoni. Nikasema jamani huyu ni RC Kleruu!” Mzee David anaelezea picha yake ya kwanza ya kifo cha Dk. Kleruu. Namwuliza ni kipi kikatokea baada ya hapo.
 
Anajibu; “Kwa kweli mambo yalikwenda haraka sana. Nakumbuka kulikuwa na pilikapilika nyingi pale kituoni. Mimi nilikuwa mtaalamu wa chumba cha mawasiliano tukiita signals. Taarifa zilianza kusambazwa kupitia chumba cha signals nilikofanyia kazi.
 
Ilikuwa mshikemshike. Tarumbeta la polisi likapulizwa. Askari wakakusanyika. Tukatangaziwa rasmi kifo cha mkuu wa mkoa. Kuna askari waliotumwa hospitalini kwenda kuchukua kitanda cha magurudumu cha kumlaza Dk. Kleruu na kumpeleka kumuhifadhi chumba cha maiti.
 
“Gari la mkuu wa mkoa likazungushwa na kuingizwa uani kwenye kituo cha polisi.
 
Wanamichezo tuliokuwa tukijiandaa na safari ya Moshi kesho yake tukaambiwa tuendelee na mipango ya safari. Tuliondoka asubuhi yake na basi la Relwe.
 
“Nyuma yetu tuliacha vumbi kubwa. Msako mkali wa kipolisi ulianza usiku ule ule wa kuamkia safari yetu ya Moshi. Iringa ilitikisika na ikaendelea kutisikika kwa wiki kadhaa.
 
“Kuna jamaa wa mjini na ambao walikuwa ni wakulima na walimchukia sana Dk. Kleruu. Baadhi nawakumbuka kwa majina. Jamaa hawa walipopata habari ya kifo cha Dk. Kleruu, basi, mmoja wao alinunua kreti za bia na kuanza kunywa na wenzake kusheherekea. Kati ya watu wa kwanza kunaswa kwenye msako wa kipolisi ni jamaa hawa.
 
Maswali kwa askari huyo wa zamani yanaendelea, namuuliza; Je, Dk. Kleruu alikuwa ni mtu wa namna gani?
 
“Bwana Maggid, na kwa bahati nilimfahamu sana Dk. Kleruu, maana kabla ya kuhamishiwa Iringa alitokea Mtwara. Na mimi nilifanya kazi Polisi Mtwara wakati Kleruu akiwa Mkuu wa Mkoa. Naweza kusema namfahamu Dk. Kleruu. Na ninayo ya kumwelezea hata sasa. ”
 
NIPO katika mgahawa wa Neema Craft mjini Iringa. Mzee David Butinini na mimi tumepanga tukutane mahali hapa kwa chakula cha mchana na mazungumzo kuhusu alichokishuhudia miaka 40 iliyopita. Inahusu tukio la mkulima Said Mwamwindi kumpiga risasi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu.
 
Zikiwa zimebaki dakika mbili kabla ya kutimu saa saba mchana tuliyoahidiana, namwona Mzee Butinini akipandisha ngazi za mgahawa. Pamoja na umri wake mkubwa, Mzee Butinini bado anaonekana kuwa na mwili wa kimichezo pia.
 
Kwa wasiomjua, kwenye miaka ya sitini na wakati akiwa kwenye Jeshi la Polisi, Mzee Butinini alipata pia kuchezea klabu ya soka ya Ushirika ya Mwanza wakati huo ikiitwa Mwanza-Coop. Huyu ndiye baba pia wa wanamichezo mahiri; marehemu Duncan Butinini kwenye soka na Jane Butinini kwenye mpira wa pete.
 
Namuuliza Mzee Butinini; “Dk. Kleruu alipata kuwatamkia watu wa Iringa, kuwa kama hawamjui wawaulize watu wa Mtwara. Na wewe unasema ulikuwa naye Mtwara kabla hajahamishimiwa Iringa, je, Dk. Kleruu unayemfahamu wewe ni mtu wa namna gani?
 
“Sikumfahamu Dk. Kleruu kama rafiki, nilikuwa namwona zaidi kikazi. Kikazi nilianzia Masasi, Mtwara. Na nakumbuka akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk. Kleruu alifika Masasi na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara. Nilikutana naye pia wilayani Newala. Ni kweli, hata kule Mtwara Dk. Kleruu alionekana kuwa ni kiongozi mkali na mwenye kuhimiza mambo kwa nguvu.
 
Lakini pia ieleweke hapa, kuwa maeneo kama Newala na sehemu nyingine za Mtwara yalikuwa ni maeneo ya Vita. Itakumbukwa tulikuwa kwenye kuwasaidia ndugu zetu wa Msumbiji hususan Frelimo kwenye mapambano yao ya ukombozi kutoka kwenye utawala wa Wareno. Sasa labda hali kule Mtwara ilikuwa ni tofauti na ilimtaka mtu kama Dk. Kleruu,” anasema Mzee Butinini.
 
Na umesema kuwa Kleruu alipohamishiwa Iringa nawe ukahamishiwa Iringa pia. Je, Dk. Kleruu uliyemwona Mtwara alikuwa na tofauti gani na Dk. Kleruu uliyekutana naye Iringa?
 
Niliripoti Iringa mwezi Machi. Nami nilikuwa mgeni pia na mkoa huu wa Iringa. Nilikuwa askari kijana sana pia. Kule Mtwara Dk. Kleruu alikuwa zaidi kwenye kuhimiza wananchi kwenye masuala ya maendeleo lakini zaidi kwenye hali ya kijeshi ikiwamo mambo ya kuchimba mahandaki kutokana na hali niliyoielezea hapo.
 
Na watu wa Mtwara walikuwa katika hali duni sana kimaendeleo. Mtwara Dk. Kleruu hakukumbana na upinzani katika kutoa amri zake.
 
Sasa nadhani hapa Iringa Dk. Kleruu alikutana na hali tofauti. Kwa mawazo yangu nadhani Dk. Kleruu kama Mkuu wa Mkoa alipaswa kujiandaa na zaidi kujifunza juu ya mila na desturi za watu wa Iringa. Maana, watu wa Iringa ni watu wa Iringa.
 
Dk. Kleruu alikuwa kijana mdogo sana kwenye macho ya wazee wa mji huu wa Iringa. Na mji huu wa Iringa ulikuwa na kundi dogo la wakulima wazawa waliokuwa na kipato kikubwa. Ndio waliokuwa wakiijenga Iringa. Hawa hawakuwa wakulima wadogo wadogo. Walikuwa wanamiliki mashamba makubwa sana. Walikuwa wanamiliki magari, malori na matrekta ya kulimia. Mmoja wa wakulima hao ndiye huyu mkulima Said Mwamwindi.
 
Namuuliza tena; Mzee Butinini, umeaniambia huko nyuma kuwa mara baada ya kupigwa risasi na kuawa kwa Dk. Kleruu kuna wakulima hapa mjini Iringa waliokamatwa na kutiwa nguvuni. Je, inakuwaje wakulima waishi mjini?
 
Anajibu; Unajua Maggid, Iringa ilikuwa tofauti sana. Wakulima wakubwa wa Iringa walikuwa na mashamba yao pale Isimani. Ni umbali wa kilomita arobaini hivi kutoka hapa. Sasa kule shamba walijenga nyumba za kufikia tu wakati wa msimu. Lakini makazi yao haswa ya kudumu ilikuwa hapa mjini.
 
Kuna wakulima waliokwenda shamba asubuhi na usafiri wao na jioni walirudi Iringa Mjini. Na kuna ambao mjini hapa walikuwa wamewekeza kwenye shughuli nyingine. Hawa watu walikuwa matajiri hata kwa kiwango cha wakati ule. Walikuwa ni watu wenye ushawishi pia. Walisikilizwa na watu, waliheshimiwa.”
 
Namuuliza swali hili Mzee Butinini; Mmoja wa wazee nilioongea nao kwa simu na natarajia nitakutana nae kwa mazungumzo ya ana kwa ana ni mkulima Mzee Pesambili na ambaye alikuwa rafiki wa Said Mwamwindi. Huyu bwana ni mmoja kati ya wale waliokamatwa na kuwekwa kizuizini. Je, unafikiri ataniambia nini kuhusu kilichotokea?
 
Mzee Pesambili is still bitter! Unasikia, huyu bwana ana machungu sana. Na nadhani huenda atafurahi kuongea nawe ili aseme machungu yake. Na wakati nakuja kukutana na wewe, nimemwona anatembea kwa miguu pale Stendi ya Daladala ya Miyomboni. Amevalia pama lake. Hatukusalimiana. Ukiongea nae ujue, kuwa utakutana na mtu mwenye machungu ya yaliyomkuta.
 
Maana, usiku ule wa tukio aliposikia polisi tunamfuatilia alikimbia makazi yake. Akaenda kukamatiwa Mufindi huko. Na baadae akapelekwa kusikojulikana. Aliporudi akakikuta kiwanja chake pale Kihesa kimechukuliwa. Kimsingi maisha yake yakaharibika. Ari na moyo wa kuendelea na kilimo ikamwishia. Na mifano mingine ya watu kama mkulima Pesambili.
 
Wakati wa sakata lile, watu waliokuwa wakikamatwa walikuwa wakisafirishwa usiku na ndege ya jeshi. Huko walikokwenda walitawanywa. Hawakukutana. Na huku nyuma mambo yakazidi kuwa mabaya. Unajua Maggid, unapomkamata mzee mwenye mji wake. Kisha akapelekwa mahali ambako ndugu zake hawajui, basi, unawaweka wana ukoo katika hali ya mashaka. Na pengine jamii ambayo mtu huyo aliishi. Tunajua kuwa kuna wenyeji ambao walipinga kilichokuwa kinafanyika. Lakini hofu ilitawala.
 
Na siku zote, watu ni watu. Hata wakikaa kimya, wanasema katika kimya hicho. Nakumbuka wakati wa operesheni ile kulikuwa na vituo vya usalama kwenye maeneo ya vijijini. Mimi nilipangiwa eneo la Igula. Kwenye vilabu vya pombe wenyeji waliimba kwa mafumbo na kwa lugha yao, nyimbo za kushutumu dola. Lakini, huwezi kumfungulia mshtaka mtu kwa kuimba nyimbo ya mafumbo!
 
Nikuulize Mzee Butinini; Fikiri kama tukio lile lisingetokea siku ile ya Jumapili ya Desemba 25, 1971, je, Iringa leo ingekuwaje?
 
Iringa ingekuwa imeendelea sana, lakini hili lingetegemea pia na sera za nchi. Maana, tatizo lingebaki kama sera zingebaki kuwa zile zile. Ukumbuke kuwa Dk. Kleruu alikuwa anaamini anatekeleza sera za Azimio la Arusha za Ujamaa na Kujitegemea. Kwamba kumfuata mtu shambani kwake, tena siku ya Krismasi, kwa Dk. Kleruu aliamini hiyo ni sehemu ya kazi yake ya kuhimiza kilimo. Ingawa, bado ni kitendawili, kwa nini afanye hivyo siku ya Krismasi?
 
Na nadhani ugomvi mkubwa kati ya Dk. Kleruu na wakulima wakubwa wa Iringa ulikuwa kwenye sera ya kuchangia mashamba. Haya mambo ya mashamba ya ushirika. Dk. Kleruu alishindwa kwenye right approach kwa maana ya msogeleo sahihi kwa wenyeji katika kuifanya kazi yake.
 
Sasa basi, hata kama Mwamwindi asingefanya tendo lile baya la kuua, bado, mazingira ya wakati ule yangefanya kuwepo na mgongano mkubwa kati ya wakulima wakubwa na watawala. Na hili kwa kweli lilijitokeza mahali pengi hapa nchini.”
 
Mzee Butinini alinijibu; Mzee Pesambili is still bitter! Unasikia, huyu bwana ana machungu sana. Na nadhani huenda atafurahi kuongea nawe ili aseme machungu yake. Na wakati nakuja kukutana na wewe, nimemwona anatembea kwa miguu pale Stendi ya Daladala ya Miyomboni. Amevalia pama lake. Hatukusalimiana. Ukiongea nae ujue kuwa utakutana na mtu mwenye machungu ya yaliyomkuta.
 
Maana, usiku ule wa tukio aliposikia polisi tunamfuatilia alikimbia makazi yake. Akaenda kukamatiwa Mufindi huko. Na baadaye akapelekwa kusikojulikana. Aliporudi akakikuta kiwanja chake pale Kihesa kimechukuliwa. Kimsingi maisha yake yakaharibika. Ari na moyo wa kuendelea na kilimo ikamwishia. Kuna mifano mingine ya watu kama mkulima Pesambili,” anasema Mzee Butinini.
 
Taarifa hizi za kamata kamata kwa baadhi ya wakulima wakubwa bado ziko kwenye kumbukumbu za baadhi ya wenyeji wa Iringa. Kuna taarifa pia za wenyeji wa Iringa kuonyesha wazi hisia zao za kuchukukizwa na uongozi wa Dk. Kleruu na hivyo kuwa tayari kusimama upande wa mkulima Mwamwindi.
 
Kuna taarifa za kuwapo kwa wakulima waliochangishana fedha kwa madhumuni ya kukodi wakili kutoka Uingereza aje kumtetea Mwamwindi kwenye kesi hiyo. Inasemekana vyombo vya usalama viliinasa orodha ya majina ya waliochangisha fedha na iliitumia orodha hiyo katika zoezi la kumkamata mmoja baada ya mwingine miongoni mwa wachangiaji.
 
Hali ilikuwa ni ya shaka sana wakati huo. Kuna wakati, wanafunzi wa Chuo cha Ualimu waliambiwa waandamane kupinga kitendo cha mauaji kilichofanywa na mkulima Mwamwindi. Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho waliokuwepo wakati huo, mandamano hayo ilibidi wayatawanye wenyewe mara walipoingia mitaa ya mji wa Iringa, maana, walikutana na sura nyingi za wenyeji wa Iringa walioonyeshwa kukerwa na kitendo kile cha wanafunzi kuandamana.
 
”Tulihofia tusije tukapigwa mishale, tukatawanyika wenyewe kurudi chuoni,” anasema mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho ambacho baadaye kikaja kujulikana kama Chuo Cha Ualimu Cha Kleruu”.
 
Hakika, tukio lile la Mkuu wa Mkoa kupigwa risasi na Mkulima Mwamwindi halikutikisa Iringa tu, bali nchi nzima. Na kwenye maeneo mengine ya nchi hii watu wa kabila la Wahehe walihofiwa kwa kudhaniwa ni wenye hulka ya kuua kama Mwamwindi. Ikafika wakati, nje ya Iringa, mwanamume wa Kihehe akiingia kwenye baa, kuna wenyeji wa sehemu hizo waliotania kwa kusema; ameingia Mwamwindi.
 
Na taarifa juu ya siku ile ya tukio la mauji zimekuwa zikiwachanganya wengi hadi hii leo. Kupitia mfululizo wa simulizi hizi, zimeanza kujitokeza taarifa mpya zinazotoa mwanga wa kilichotokea. Mathalan, kuna polisi mstaafu aitwaye Mushi na ambaye kwa sasa anaishi Moshi akiendesha kampuni ya ulinzi ana haya ya kusema; Bwana Maggid, mimi nilikuwa kaunta siku ile ya tukio; Jumapili ya Krismasi, Desema 25, 1971. Bwana Butunini uliyeongea naye tulikuwa naye pale polisi Iringa. Siku ile ya tukio, asubuhi kabisa Dk. Kleruu alifika pale polisi baada ya kutoka kwa RPC Aboubakar.
 
Kleruu na mimi tulikuwa marafiki baada ya kumsaidia kwenye upepelezi wa wizi uliotokea nyumbani kwake na nikafanikiwa kupata vitu vyake karibu vyote vilivyoibwa nyumbani kwake. Ulikuwa wizi wa ajabu maana nyumba ya Mkuu wa Mkoa ilikuwa inalindwa,” anasema Mushi. Kisha anaendelea kusimulia; Tangu hapo tukawa na uhusiano wa kirafiki na Mkuu wa Mkoa Kleruu. Nakumbuka siku ile ya tukio alipofika pale kituoni aliniaga kwa kuniambia anaenda Nyang’olo kwenye mambo ya kilimo. Kisha akanikaribisha jioni hiyo niende nyumbani kwake nikale Krismasi. Basi, baadaye tukajua kuwa afande RPC Aboubakar alimwambia ampe walinzi wa kwenda nao, lakini Kleruu alikataa.”
 
Basi, jioni ile ndio tukaona gari lake likingiia kituoni. Aliyeliendesha hakuwa Dk. Kleruu. Mimi ndiye niliyepokea bunduki aliyoikabidhi Mwamwindi. Ilikuwa ya midomo miwili. Hata gari la Mkuu wa Mkoa ndiye mimi niliyeliendesha kulizungusha kule uani polisi baada ya mwili wa marehemu kutolewa,” anasema polisi mstaafu Mushi.
 
Hakika, maelezo hayo yanathibitisha kitendawili kigumu juu ya kilichotokea siku hiyo. Kama ilivyoelezwa huko nyuma na Amani Mwamwindi. Huyu ni mtoto wa mkulima Mwamwindi. Alisema haya; ” Siku hiyo Kleruu, pamoja na kuwa ni Mkristo, aliamua kutokula Krismasi. Alivaa kofia yake ya pama. Kleruu akaendesha mwenyewe gari lake la mkuu wa mkoa aina ya Peugeot Injection, rangi ya bluu. Katika orodha yake, Kleruu alikuwa na watu watatu wa kuwashughulikia miongoni mwa wakulima wale wakubwa wa Isimani. Target nambari moja alikuwa Rashid Juma wa Nyang’olo. Nambari mbili ni marehemu baba. Namba tatu simjui.
 
Kleruu alipofika Nyang’olo hakumkuta mkulima Rashid Juma. Siku hiyo ya Krismasi Rashidi Juma alipata habari, kuwa kuna ng’ombe wake walipotelea milimani. Alikwenda huko milimani kusaka ng’ombe wake. Hivyo, Kleruu akafunga safari kurudi kwa target namba mbili, baba yangu Mzee Mwamwindi. Ni njia hiyo hiyo, Nyang´olo iko mbele ya ilipokuwa ngome ya mzee.”
 
”Basi, Kleruu akafika kwa Mzee. Baba akiwa shambani akaliona gari la Kleruu limesimama nje ya mji wake. Kisha akamwona Kleruu akitembea kumfuata shambani. Baba alihisi tu, kuwa Kleruu amekuja na shari.
 
Kleruu akamuuliza Mzee kwa ukali, ”Mbona mnafanya kazi leo siku ya Krismasi?” Baba akamwomba Kleruu waende wakazungumze nyumbani. Akamwambia mdogo wangu Mohammed aendelee kulima. Mzee akatangulia mbele, nyuma anamfuatia Kleruu. Kabla ya kufika kwenye nyumba yake wakayapita makaburi. Kleruu akamtamkia baba mzee Mwamwindi; Hapa ndipo unapozika mirija yako?” Alitamka hivyo huku akimtomasa tomasa mzee na kifimbo alichoshika mkononi.
 
Jambo hilo lilizidi kumkasirisha marehemu mzee. Akafika nyumbani kwake. Mlangoni alisimama mke wake mdogo. Inaonekana mzee alishafanya uamuzi. Jana yake alikwenda kuwinda. Hakupata mnyama. Bunduki yake moja aina ya riffle kati ya bunduki zake mbili ilikuwa bado ina risasi. Akamwambia mke wake mdogo huku Kleruu akiwa anasikia; kanichulie bunduki yangu,” anasema Amani Mwamwindi, mtoto wa Mkulima Mwamwindi.
 
Mwanga zaidi juu ya tukio hili unazidi kupatikana. Lakini, kuna mengine yanayotakiwa kufanyiwa utafiti ili kubaini ukweli wa kilichotokea. Bila shaka, mahojiano yangu na mkulima Pesambili na ambaye alikuwa ni rafiki wa mkulima Mwamwindi yatatupa mwanga mwingine. Na kuna wengine wanaozidi kuchangia katika kutupa mwanga. Na je, ni nini tafsiri ya hukumu ya kesi ya Mwamwindi.

No comments:

Post a Comment