Maggid Mjengwa
IRINGA
ina historia ndefu ya harakati za mapambano ya kudai uhuru. Harakati za
kijamii, kisiasa na kiuchumi. Wakati huu nchi yetu ikielekea kwenye kuadhimisha
miaka 50 ya uhuru si vibaya tukakumbushana tulikotoka ili tuweze kuelewa tulipo
sasa na tunakokwenda.
Hakika,
simulizi ya Mkulima Saidi Mwamwindi aliyepambana na dola ni moja ya simulizi
zilizowagusa wasomaji wangu wengi.
Ni
simulizi iliyonifanya nihamasike kutafuta habari zaidi za Watanzania mfano wa
Mwamwindi ambao, hata kama huko nyuma jamii ilitakiwa iwaone kama wasaliti,
lakini, jamii si mkusanyiko wa watu wajinga. Kuna walioulewa ukweli, waliamua
kukaa kimya. Na wakati mwingine walisema na hata kuimba kile ambacho watawala
waliwataka waimbe na kusema.
Hata
hivyo, mioyoyoni mwao, waliujua ukweli. Kuna walioimba huku wakilia mioyoni.
Kuna waliosema huku wakisononeka mioyoni.
Huu
ni wakati wa kujaribu kuusema ukweli ili tuweze kwenda mbele kama taifa.
Simulizi
ya mkulima, Saidi Mwamwindi ni jaribio la kuutafuta ukweli huo. Na hii ni
simulizi shirikishi yenye kukukaribisha ewe msomaji, uje na unachokijua juu ya
kilichotokea zaidi ya miaka 40 iliyopita.
Mwamwindi
ni kielelezo cha hali iliyokuwepo wakati huo. Mathalan, utekelezaji wa Sera za
Ujamaa na kilimo cha ushirika ulitakiwa utekelezwe kwa kuzingatia mazingira ya
kila mahala.
Inakuwaje
basi kwa mkuu wa nchi unapomweka mkuu wa mkoa kijana anayeanza kwa kuwahutubia
wakulima wakubwa mfano wa Saidi Mwamwindi habari za kilimo cha heka nne nne?
Wakulima
ambao tayari, hata kabla ya Uhuru wameweza kuwa na matreka na hata kuanzisha
ushirika wao wa wakulima. Ndio, inawezekana vipi kwa mkulima wa shamba la ekari
mia nne akajisikia furaha kuwa kwenye mkutano na mkuu wa mkoa anayezungumzia
kilimo cha ekari nne nne? Mbinu gani ya kiuongozi ilihitajika ili kumfanya
mkulima mkubwa kama Mwamwindi ashiriki na kuwasaidia wakulima wadogo wadogo?
Na
hapa inaanza simulizi ya Mwamwindi;
Mwanzoni
mwa miaka ya 1970 mkulima, Saidi Mwamwindi alikabiliwa na shitaka la kumwua Dk
Wilbert Kleruu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa wakati huo.
Mshitakiwa
Mwamwindi alijitetea kuwa alipokuwa anamwua marehemu Kleruu alirukwa na akili .
Hivyo, akapotewa na fahamu ya kuweza kuelewa kile alichokuwa anakitenda. Jaji
Onyiuke kutoka Nigeria aliukataa utetezi wa Mwamwindi kwa kutilia maanani
kwamba baada ya mshitakiwa kughadhibishwa ndipo alipokwenda ndani kuchukua bunduki
ambayo aliitumia kumwua marehemu.
Oktoba
mwaka 2010, nikiwa njiani kwenda Dodoma na Arusha, nilipita kijijini Isimani.
Hapo ndipo yalipokuwa makazi ya Mwamwindi. Ni umbali wa kilomita zipatazo 40
kutoka Iringa Mjini. Kijijini Isimani Saidi Mwamwindi bado anaonekana ni shujaa
kwa kukataa kunyanyaswa na Mkuu wa Mkoa.
Inasimuliwa,
kuwa ilikuwa siku ya Jumapili, tena siku ya Krismasi, pale Mkuu wa Mkoa, Dk
Kleruu, alipofika Isimani na kumkemea Mwamwindi mbele ya wake zake kwa vile
alifanya kazi za shamba siku ya Sikukuu.
Inasimuliwa,
kuwa Dk. Kleruu alifikia hata hatua ya kuanza kudhihaki makaburi ya mababu zake
Mwamwindi akimwambia Mwamwindi: “Humu ndimo mlimozika mirija yenu”. Alifanya
hivyo huku akionyesha makaburi yake kwa kutumia fimbo aliyoshika mkononi.
Mwamwindi alikasirika sana. Akaficha hasira yake.
Kutoka
makaburini, Mwamwindi aliongozana na Kleruu hadi nje ya nyumba yake. Akamwomba
Mkuu huyo wa Mkoa abaki nje. Mwamwindi akaingia ndani chumbani.
Mke
wake Mwamwindi alimwona mume wake akichukua bunduki na kusimama dirishani. Mama
huyo alidhani mumewe amepanga kwenda kuwinda. Kumbe, Mwamwindi alitokea
dirishani na kumwelekea Kleruu aliyedhani Mwamwindi angetoka nje kwa kupitia
mlangoni.
Basi,
Mwamwindi akamlenga Mkuu wa Mkoa sawa kichwani. Dk kleruu alinyoosha mikono juu
na kuomba asemehewe. Mwamwindi alikaa kimya. Kisha akafyatua risasi. Kishindo
kilisikika kijijini. Baada ya hapo, kwa mikono yake, Mwamwindi akaubeba mwili
wa Mkuu wa Mkoa na kuuweka nyuma ya boneti ya gari alilojia mkuu huyo wa mkoa.
Mwamwindi
alichukua kofia ya pama aliyovaa Kleruu. Akaivaa kichwani na kuanza kuendesha
gari hilo hadi kituo cha polisi Iringa. Waliokutana na Mwamwindi njiani
walimshangaa akiendesha gari hilo la Mkuu wa Mkoa akiwa amevalia kofia ya mkuu
huyo. Hatimaye Mwamwindi akafika kituo cha Polisi.
Akatoka
na kwenda mapokezi. Hapo akaripoti tukio kwa kutamka; " Nendeni mkamchukue
mbwa wenu nyuma ya gari!"
Tukio
lile bado linatuachia maswali? Je, ni kwanini Dk Kleruu alikwenda nyumbani kwa
Mwamwindi siku ya Jumapili na hususan siku ya Krismasi?
Je,
yawezekana Mwamwindi na Dk Kleruu walikuwa na ugomvi mwingine kabla ya tukio?
Kuna
waliokuwepo na wanasimulia kana kwamba ilikuwa ni jana tu. Mmoja wa watu hao ni
mwana wa Mwamwindi aitwaye Amani Mwamwindi ambaye ndiye Meya wa Manispaa ya
Iringa kwa sasa. Amani Mwamwindi anakumbuka nini juu ya siku hiyo?
MKE
wake Mwamwindi alimwona mume wake akichukua bunduki na kusimama dirishani. Mama
huyo alidhani mumewe amepanga kwenda kuwinda. Kumbe, Mwamwindi alitokea
dirishani na kumwelekea Kleruu, aliyedhani Mwamwindi angetoka nje kwa kupitia
mlangoni.
Basi,
Mwamwindi akamlenga Mkuu wa Mkoa kichwani. Dk. Kleruu alinyosha mikono juu na
kuomba asemehewe. Mwamwindi alikaa kimya. Kisha akafyatua risasi. Kishindo
kilisikika kijijini. Baada ya hapo, kwa mikono yake, Mwamwindi akaubeba mwili
wa Mkuu wa Mkoa na kuuweka nyuma ya boneti ya gari alilotumia mkuu huyo wa
mkoa.
Mwamwindi
alichukua kofia ya pama aliyovaa Kleruu. Akaivaa kichwani na kuanza kuendesha
gari hilo hadi kituo cha polisi Iringa. Waliokutana na Mwamwindi njiani
walimshangaa akiendesha gari hilo la Mkuu wa Mkoa akiwa amevalia kofia ya mkuu
huyo. Hatimaye Mwamwindi akafika kituo cha Polisi.
Akatoka
na kwenda mapokezi. Hapo akaripoti tukio kwa kutamka; "Nendeni mkamchukue mbwa
wenu nyuma ya gari!".
Tukio
lile bado linatuachia maswali? Je, ni kwa nini Dk. Kleruu alikwenda nyumbani
kwa Mwamwindi siku ya Jumapili, tena siku ya Krismasi?
Je,
yawezekana Mwamwindi na Dk. Kleruu walikuwa na ugomvi mwingine kabla ya tukio?
Tuendelee na simulizi hii kama ifuatavyo.
“Niliporudi
nyumbani kutoka Ifunda nikazikuta habari hizo mbaya. Nikaenda moja kwa moja
hadi nyumbani kwa Mzee pale Mshindo. Nikawakuta akina mama wanalia.
“Ilikuwa
ni kilio. Hiyo bado ilikuwa, siku ya Krismasi. Nikauliza; kuna aliyekwenda
kumwona baba pale polisi? Jibu likawa hapana. Nikaenda moja kwa moja polisi ili
nikamwone baba na nimsikie kauli yake.
Nilipofika
polisi nikaanza kujieleza kwa askari polisi kuomba ruhusa ya kuongea na Mzee.
Wakati nikifanya hivyo mzee nae alisikia sauti yangu. Akatamka; ” Mwanangu
huyo, mruhusu niongee nae”. Nikaongea na Mzee.
“Niliweza
kuongea na Mzee na kupata picha ya kilichotokea. Niliondoka kurudi nyumbani.
Habari zilishasambaa. Hali haikuwa nzuri. Mji wa Iringa ulitulia sana. Halafu
ukaja mtikisiko mkubwa. Wazee wengi walioishi mjini na waliokuwa wakilima na
Mzee kule Isimani walisombwa na vyombo vya usalama.”
Je,
ni kina nani hao? Namwuliza Amani Mwamwindi. Anajibu; “Mzee kama Ibrahim
Khalili, Mursali na wengine. Watu kama 30 hivi walisombwa na kupelekwa sehemu
mbalimbali za nchi. Kuna waliopelekwa Mwanza, Shinyanga hata Zanzibar. Kwa
namna fulani walitenganishwa katika sehemu hizo.”
Je,
na wewe ulikumbwa na msukosuko huo? “Ndio, hata mimi nilihojiwa ingawa
niliachwa niendelee na kazi zangu. Kumbuka nilikuwa kijana wa miaka 21 tu, na
siku ya tukio nilikuwa shambani kwangu Ifunda. Hapa nyumbani kwangu kulikuwa na
askari wa FFU muda wote. Katika kuhojiwa kwangu maswali mengine yalikuwa hayana
msingi.
Kwa
mfano, niliulizwa; Mzee alipokuja hapa kwako kutoka Isimani siku ya tukio
alitaka kukwambia nini? Sasa, mimi hakunikuta nyumbani na hatukuongea,
nitajuaje alichotaka kuniambia siku hiyo? Anaeleza Amani Mwamwindi, akionyesha
kushangaa, hata hii leo.
Je,
kwa wakati huo, wewe na familia yenu mlihisi kutengwa na jamii kutokana na
kitendo alichofanya Mzee Mwamwindi? Namwuliza. Namwona Amani Mwamwindi
akionyesha kuguswa sana na swali hili.
“Tulikuwa
na wakati mgumu sana kama familia. Kibaya zaidi kwetu ilikuwa ni kuingia kwenye
uhasama na ndugu wa jamaa ambao wazee wao walisombwa na vyombo vya usalama na
kwenda kusikojulikana.
“Kwao
waliamini kama isingekuwa Mzee wetu Mwamwindi kufanya tendo lile, basi, wazee
wao wangebaki salama na kuendelea na shughuli zao za kilimo. Hivyo basi tulisakamwa
na wengine ambao ni ndugu zetu.”
Mlifanyaje
kuikabiili hali hiyo? “Tulifikia uamuzi mimi niende Dodoma kwenye gereza
alikokuwa Mzee Mwamwindi. Niende nikamjulishe baba juu ya hali iliyotokea huku
nyumbani. Kwamba tuna uhasama na jamaa wa waliosombwa na vyombo vya dola.
Nilipata
kibali cha DC hapa Iringa. Kibali cha kwenda kumwona Mzee kule Dodoma.
Nilipofika Dodoma nikaonana naye. Tukazungumza. Nikamwambia shida ya nyumbani.
Alisikitika sana.
Akaniuliza;
“Sasa tufanyeje?”. Nikamshauri aandike barua kwenda kwa Nyerere kumwomba
atusaidie. Baba aliandika barua siku hiyo hiyo. Alimwandikia Nyerere kumwambia
na kumhakikishia kuwa ni yeye Said Mwamwindi na si mtu mwingine yeyote
aliyehusika na tendo alilofanya; kumpiga risasi na kumuua Kleruu.
Barua
ile ilifika kwa Nyerere, na haukupita muda mrefu, wazee wale wakulima wa
Isimani waliachiwa huru na kurudishwa Iringa. ”
Je,
hali ya uhusiano na waliowachukia ilibadilika na kuwa njema baada ya wazee hao
kurudi Iringa? Namuuliza Mzee Amani Mwamwindi.
“Ndio,
kabisa. Hali ikawa shwari. ” Je, wazee wale wakulima wa Isimani walirudi na
kuendelea na kazi zao za kilimo?
“Niseme
kuwa walirudi Iringa wakiwa wameathirika kisaikolojia. Kuna ambao hawakutaka
kabisa kurudi tena Isimani. Baadhi yao hawakuishi muda mrefu, walifariki. Sijui
nini kiliwatokea.”
Je,
unafikiri Iringa ingekuwaje kama tukio lile la siku ya Krismasi mwaka 1971
lisingetokea?
“Naamini
kabisa, Iringa isingekuwa kama ilivyo sasa. Ingeendelea sana. Unajua kulikuwa
hakuna mahala pengine katika nchi hii ambapo kulikuwa kunazalishwa mahindi
kushinda Isimani.
“Mzee
na wenzake walilima ekari nyingi sana. Naamini wangelima zaidi. Walianza
kujijenga na hata waliunda ushirika wao. Tukio lile lilisimamisha kasi ya
kilimo Isimani. Ni kama laana fulani vile, maana, tangu wakati ule mvua
zimekuwa za taabu Isimani,” anasema Mzee Amani Mwamwindi. Kisha namwuliza tena.
“Nilifika
pale nyumbani kwenu Isimani, nikaona mnara wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu, kwanza
nilifikiri ni kumbukumbu ya Mwamwindi. Je, unajisikiaje kuona nyumbani kwenu
kuna mnara wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu na si ya baba yenu?”
“Mimi
naona ni sawa kabisa kwa mnara ule kuwa pale”. Ananijibu Mzee Amani Mwamwindi
huku akionyesha kuchangamka. Anaendelea.
“Unajua
hata Nyerere alipofika Isimani wakati fulani aliuliza; ” Hivi huu mnara ni wa
kumbukumbu ya Dk. Kleruu au Said Mwamwindi?” Nyerere alikuwa na maana yake.”
Ananiambia Mzee Amani Mwamwindi. Kuna kitu anataka kufafanua, anasita. Namwacha
aendelee kutafakari.
Kisha
ananiuliza swali gumu. Nabaini ni mara ya kwanza katika mazungumzo yetu ameamua
kunirushia swali. Kwa mtazamo wangu ni swali la kifalsafa. Mzee Amani Mwamwindi
ananiuliza; “Bwana Mjengwa, mche unaochipua ardhini unahitaji kumwagiliwa maji
ili uendelee kuchipua. Ukisimama vema unauacha ukue wenyewe. Na je, ukishakua
na kukomaa unaufanyaje?”. Mzee Amani Mwamwindi ananiuliza huku akinitazama
usoni.
Naam,
ni swali gumu lenye kunihitaji, sio tu kufikiri, bali kufikiri kwa bidii. Jibu
lake lazima lifuatiwe na majadala.
Ewe
msomaji mpendwa, kabla sijaingia kwenye nilichomjibu Mzee Amani Mwamwindi na
mwendelezo wa mazungumzo yetu nakutoa nje ya nyumba ya Amani Mwamwindi pale
Mlandege.
Maana,
mpaka kufikia hapa tumemsikia Mzee Amani Mwamwindi, kama mwanafamilia ya
marehemu Said Mwamwindi akisimulia kilichotokea.
Iringa
Mjini kuna mmoja wa wazee wa siku nyingi, Mzee Omar Mselem Nzowa. Huyu ni mmoja
wa wazee walionipokea nilipofika Iringa miaka sita iliyopita. Mzee Nzowa
alimfahamu marehemu Said Mwamwindi, baba wa Amani Mwamwindi . Jumamosi moja ya
mwezi Novemba, 2010 naamua kwenda nyumbani kwa Mzee Nzowa.
Tumekaa
sebuleni, mimi na Mzee Nzowa. Tunaongea huku tukipata kikombe cha chai.
“Ndio
Mzee wangu, nisimulie habari za Marehemu Said Mwamwindi, maana nimekutana na
mwanae, Amani Mwamwindi, naye kuna aliyonisimulia. Je, ulipata kukutana na
marehemu Said Mwamwindi wakati wa uhai wake?”
Aah!
Said Mwamwindi, nilimfahamu sana." Ananiambia huku anacheka. Kisha
anaendelea kusema;
"Unajua,
tulikua naye hapa mjini. Na hata siku ile ya tukio mimi na vijana wenzangu wa
wakati ule tulikuwa tunacheza bao pale Miyomboni, tulishangaa sana kumwona Said
amesimamisha gari la Dk. Kleruu nyumbani kwa shangazi yake na huku amevalia
pama la Dk. Kleruu.
“Nakumbuka
alitunyoshea mkono akiwa anatabasamu. Tulizungumza kwa kushangaa, tukajiuliza;
jamani hivi Serikali leo imempa Said Mwamwindi gari atembelee? Yakafuata
yaliyofuatia. Maggid, ninayo mengi ya kukusimulia kwa yaliyotokea katika wakati
ule….” Anasema Mzee Nzowa.
“Ndiyo, nilimfahamu Said, na jina lake hasa
aliitwa Said Abdalah Siulanga Mwamwindi. Nyumba ya baba yake ilikuwa pale
Mshindo karibu na ukumbi wa Welfare. Baba yake aliwahi kuwa Jumbe enzi za
ukoloni. Kwa kweli Said alikuwa ni mtu wa kilimo na nakumbuka alianzia kwenye
magari. Alikuwa dereva kabla hajaenda kufyeka mapori ya kilimo kule Isimani.”
Je,
unakumbuka wajihi wa marehemu Said Mwamwindi?
“Ah,
yule bwana alikuwa pande la jitu. Mrefu na aliyeshiba hasa. Ukimwona utasema
huyu jamaa amekaa kiutemi-utemi. Yaani, unavyoomwona mwanae, Amani Mwamwindi
sasa, ndivyo kwa kiasi kikubwa alivyoonekana Said Mwamwindi. Wamefanana
sana."
Na
je, Dk.Kleruu, alikuwa mtu wa namna gani, wajihi wake na mengineyo?
”Alaa,
Dk.Kleruu. Tulikuwa vijana wakati ule, na yeye alikuwa Mkuu wa Mkoa kijana hapa
Iringa. Nafikiri alichukua nafasi ya Bw. Chamshama. Alikuwa mfupi kidogo. Ila
bwana, alikuwa machachari sana . Nikisema ’machachari’ nadhani unanielewa.
Haraka
sana tuliona dalili kuwa Dk.Kleruu asingekuwa na wakati mzuri hapa Iringa.
Alianza
mapema sana kuonyesha tabia za ubwana na hata kunyanyasa aliowaongoza. Na
katika hao aliowaongoza, kulikuwa na watu wazima waliomzidi umri. Watu wenye
hekima na busara kumzidi yeye, ingawa hawakusoma elimu ya darasani.”
Je,
unaweza kutoka mfano wa ’ubwana’ mkubwa wa Dk.Kleruu aliouonyesha wakati huo?
”Iko
mifano mingi, na ukweli Dk.Kleruu alisemwa vibaya katika midomo ya watu hapa
Iringa. Ilifika mahala dereva akilipiga overtake gari la Dk.Kleruu hapa Iringa,
basi, atasimamishwa na anaweza kuzabwa vibao na Kleruu mwenyewe. Aah! Jamaa
yule alikuwa mbabe bwana!” Anasema Mzee Omary Nzowa huku akicheka kwa sauti.
Kisha anaendelea.
”Unajua
Dk.Kleruu alitokea Mtwara kabla ya kuja Iringa. Sasa kuna wakati alitamka;
'Hamnijui mimi, kawaulizeni watu wa Mtwara!' Sasa hayo si maneno ya kuwaambia
watu wa Iringa, na hata mahali pengine popote,” akisimulia zaidi.
”Na
nikwambie kitu kimoja Maggid, muhimu katika maisha ni kuishi vema na watu. Hata
kama ni kiongozi, huwezi kufanikiwa katika kazi yako kama huna mahusiano mazuri
na unaowaongoza. Na hata katika maisha ya kawaida, unaweza kuingia katika
misukosuko isiyo ya lazima kama huna mahusiano mazuri na wenzako katika jamii.
”Nitakupa
mfano hai unaonihusu mimi. Mwishoni mwa miaka ya 50 nilikamatwa nyumbani kwa
kutokulipa kodi ya kichwa. Tulikuwa bado kwenye utawala wa mkoloni. Nilikuwa
nadaiwa shilingi saba tu. Sikuwa nazo.
”Basi,
nikaambiwa na askari wa kodi tuongozane hadi ofisini kwa DC. Tena walinifunga
kamba mikononi. Nilifahamu, huko kwa DC ningeishia kuchapwa bakora na hata
kuwekwa ndani. Unajua Maggid enzi hizo damu ilikuwa ikichemka na sisi vijana
ndio tuliokuwa tukionekana kuiunga mkono TANU, ” ananiambia Mzee Nzowa
akikumbuka enzi za ujana wake.
”Sasa
basi, wakati tunakwenda kwa DC, niliwaomba sana wale askari wa kodi. Walikuwa
Waafrika wenzetu. Nikawaambia, jamani ee, tafadhali tupite njia hii ya sokoni.
Ni soko lile la zamani ambalo mpaka leo hii bado linatumika. Askari walikubali
wakidhani nimechagua mwenyewe njia nitakayoonekana na watu na hivyo
kujidhalilisha mwenyewe. Kumbe, mimi nilikuwa na maana yangu.
Tulipofika
eneo la sokoni nikasikia jamaa zangu wakiuliza kwa sauti; ” Omary shida gani?”.
Nikajibu kwa sauti; ” Kodi, shilingi 7!”. Basi, huwezi kuamini, hata kabla
sijamaliza soko, vijana wale wa sokoni walichangishana. Shilingi saba
zikapatikana. Kodi ile nikalipa na nikaachiwa huru. Pointi yangu hapo ni
umuhimu wa mahusiano mema na watu.”
Je,
unafikiri ni kwanini Dk. Kleruu alipata tabu sana kufanya kazi na watu wa
Iringa?
Anasema
Mzee Nzowa: ” Mi nadhani Kleruu, kwa jinsi alivyokuwa, angepata tabu kufanya
kazi mahali po pote pale. Tatizo ni ile hali ya kutanguliza ubwana na
kuwadharau wananchi. Hakika wakati ule Mwalimu Julius Nyerere alipata tabu sana
na namna ya ku-deal na viongozi kama akina Kleruu. Kumbuka ,Tanzania kama nchi
ilikuwa taifa changa sana. Hatukuwa na wasomi wengi. Nilimfahamu Nyerere, hili
la Kleruu lilimsumbua sana Mwalimu.
”Nikwambie
Maggid, Ujamaa na Kujitegemea kama itikadi na sera za Mwalimu haukuwa tatizo.
Tatizo lilikuwa kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya utekelezaji. Hawa
hawakuwa wanasiasa, wakati mwingine walionekana kama Wanyapara. Mwalimu wakati
ule hakujua kila kitu kuhusu watu aliowateua kumsaidia.
”Ni
kweli Mwalimu alitia saini hukumu ya kunyongwa kwa Mwamwindi, lakini naamini
hakufurahia, bali hali ya wakati ule ilimlazimisha kufanya vile.
”Sisi
tuliomfahamu Mwalimu tunajua kuwa hukumu ile ni moja ya maamuzi magumu
yaliyomsononesha sana Mwalimu. Unajua wakati ule kuna Wakuu wa Mikoa waliojenga
hoja, kuwa kama Mwamwindi kwa tendo lile asingepata adhabu ile, basi utendaji
wao wa kazi mikoani ungekuwa mgumu. Ndiyo, hoja hizo ziliibuka. Kwa kiongozi wa
nchi ni mtihani. Siyasemi haya kumtetea Mwalimu bali ni kutambua ukweli kuwa
Mwalimu alikuwa ni binadamu kama wewe na mimi.”
Unasema
ulimfahamu Nyerere na kwamba unaamini kwa wakati ule tatizo kwa Mwalimu Nyerere
ilikuwa kwa baadhi ya aliowapa dhamana ya kumsaidia katika utekelezaji. Je,
Mwalimu aliwahi kulizungumza jambo hili nawe ukamsikia?
”Huo
ndio ukweli. Mimi nimekuwa katika chama (TANU) tangu mwaka 1956. Kadi yangu ya
uanachama wa TANU niliikatia Mbeya. Ni Nyerere mwenyewe, kwa mkono wake, pale
Mbeya, mwaka 1956 alinijazia kadi yangu ya TANU. Alianza na Kanali Ayoub Simba
ikaja ya kwangu.
”Hata
leo, ukiangalia namba za kadi ya TANU ya Kanali Ayoub Simba na ya kwangu
zinafuatana. Tulikuwa bado vijana sana, na Mwalimu alifanya mwenyewe kazi ya
kuhamasisha vijana kuingia TANU. Mwenzangu Ayoub yeye akaja akaingia jeshini ,
akafikia mpaka cheo cha ukanali, akawa mbunge pia, kule Mafia. Yule ni kada wa
siku nyingi.
”Sasa
nimepata kumsikia Mwalimu akiongea kuhusu hili la uongozi? Kwa kweli si mara
moja. Nimemsikia Mwalimu akitamka, kuwa njia iliyo nzuri sana ya kumsaidia
katika uongozi wake ni kwa tulio karibu na watu kumwambia moja kwa moja juu ya
mazuri na mabaya wanayofanya wateule wake.
”Kwamba
ni hatari wananchi wakianza ama kuchoka kulalamika au kuwaogopa viongozi wao.
Unajua Mwalimu hakuishia tu kutumia watu wa Usalama wa Taifa, aliwatumia pia
watu wa kawaida kupata taarifa sahihi.” Mzee, turudi kwenye kilichotokea kule
Isimani, inasemekana kulikuwa na mtikisiko mkubwa hapa Iringa baada ya
Dk.Kleruu kupigwa risasi na Mwamwindi. Je, hali ilikuwaje hasa?
”
Ni sahihi, hali ilikuwa ngumu. Wengi tuliathirika na mkasa ule, kwa namna moja
au nyingine. Unajua ilifika mahali wakati ule mtu ukigongewa mlango usiku,
basi, unavaa kabisa, shati, suruali na viatu, maana huenda ukifungua mlango
usirudi tena kitandani kwako!”
Hivi
Iringa ya wakati ule ilionekaje, unakumbuka?
Anajibu
Mzee Nzowa: ” Mji huu wa Iringa ulikuwa mdogo sana, wengi tulikuwa tunajuana.
Hebu ngoja nipekue kwenye kabati langu kuona kama nina picha za zamani”. Mzee
Nzowa anainuka kitini. Anakwenda kupekua picha za zamani. Nasubiri kwa shauku.
Wakati
tukimsubiri Mzee Nzowa , Jumatatu moja usiku napokea simu kutoka Uingereza;
”E bwana Maggid, niko Uingereza, nafuatilia kisa hiki cha Mwamwindi na Dk.
Kleruu. Mimi nilikuwa kijijini Nyang’olo wakati wa tukio lile. Ni kijiji cha
jirani na alikoishi Said Mwamwindi. Nilikuwa na miaka kumi. Nakumbuka mambo
mengi sana , hata Dk. Kleruu nilimwona, alipenda sana kuja Nyang’olo. Sasa
unasikia....”
Hivi
Iringa ya wakati ule ilionekanaje, unakumbuka? Namwuliza Mzee Nzowa.” Mji huu
wa Iringa ulikuwa mdogo sana, wengi tulikuwa tunajuana. Hebu ngoja nipekue
kwenye kabati langu kuona kama nina picha za zamani”. Mzee Nzowa anainuka
kitini. Anakwenda kupekua picha za zamani. Nasubiri kwa shauku.
Wakati
tukimsubiri Mzee Nzowa, Jumatatu moja usiku napokea simu kutoka Uingereza;
“Ebwana Maggid, niko Uingereza, nafuatilia kisa hiki cha Mwamwindi na Dk.
Kleruu. Mimi nilikuwa kijijini Nyang’olo wakati wa tukio lile. Ni kijiji cha
jirani na alikoishi marehemu Said Mwamwindi. Nilikuwa na miaka 10. Nakumbuka
mambo mengi sana, hata Dk. Kleruu nilimwona, alipenda sana kuja Nyang’olo. Sasa
unasikia....”
“Dk.
Kleruu alikuwa akija na gari lake. Nyang’olo ni mji wa barabarani. Unajua ndio
ilikuwa njia kuu ya kwenda Dodoma mpaka Arusha. Kulikuwa na biashara sana.
Kulikuwa na wasomali hata waarabu. Nakumbuka Dk. Kleruu alikuwa akishika
kifimbo chake na kuwafokea wazee juu ya mambo ya maendeleo. Kwa kweli wazee wa
Nyang’olo hawakumpenda Kleruu,” anasema msomaji huyu ambaye sasa ana miaka 50
na anaishi nchini Uingereza.
Na
wakati tukiendelea na simulizi hii ya Mwamwindi zimenifikia habari mbaya. Ni
taarifa ya msiba wa Mzee Augustino Hongole Mzee Hongole ambaye, hadi kifo chake
alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri wa gazeti la Kwanza Jamii, Njombe
amefariki majuma mawili yaliyopita. Amezikwa kijijini kwao Lupembe., Njombe.
Kwangu
mimi, Mzee Hongole ni mmoja wa wazee waliochangia sana katika kuifanya simulizi
hii iwe na maana kubwa. Maana, katika utafiti wangu juu ya kisa hiki cha
Mwamwindi na Mkuu wa Mkoa Dk. Kleruu, nimepata bahati ya kufanya mazungumzo
marefu ya ana kwa ana na hata kwa njia ya simu na marehemu Mzee Hongole.
Na
kweli mwandishi wa habari mwandamizi wa magazeti ya HabariLeo na Daily News,
Beda Msimbe ndiye aliyenisisitiza sana umuhimu wa kumhoji Mzee Hongole huku
kaka yangu Msimbe akisema; “Usichelewe sana, maana wazee hao ndio wanaondoka
taratibu”.
Na
hakika nimefanya jitihada za ziada za kupokea simulizi za Mzee Hongole juu ya
anachokikumbuka katika wakati ule wa tukio.
Na
katika hili la simulizi ya Mwamwindi mchango wa marehemu Mzee Hongole ni mkubwa
sana. Mzee Hongole amechangia kutoa elimu kubwa ya kimapokeo. Hakika, nina
maelezo mengi ya Mzee Hongole ambayo nimeyahifadhi kwa simulizi za baadae.
Huko
nyuma nimewahi kusimulia yafuatayo niliyoyapokea kutoka kwa Mzee Hongole juu ya
tukio la mkulima Mwamwindi kumpiga risasi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu.
Mzee
Hongole aliyepata kuwa mwandishi wa habari kijana sana wakati wa tukio la
Mwamwindi kumuua Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu lililopotokea anasema;
"Ndio kwanza nilikuwa nimepangiwa kufanya kazi kama mwandishi wa habari
kwenye gazeti la Kanisa pale Iringa.
“Lilikuwa
tukio kubwa sana. Kama mwandishi nilitamani kuandika kilichotokea na kupata
maoni ya watu wa Iringa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla. Kwa wakati
ule mfumo haukuruhusu kitu kama hicho. Mwamwindi story was an embargoed one
(Stori ya Mwamwindi ilikuwa haiandikiki). Lakini nataka kukwambia: "Watu
wengi wa Iringa hawakumpenda Dk. Kleruu kutokana na unyanyasaji wake".
Mzee
Hongole anazidi kusema; “Unajua wakati huo kulikuwa na hofu kubwa juu ya dola.
Waliokuwa tayari kumtetea Mwamwindi hadharani walihofia kukamatwa na makachero.
Na mimi kalamu yangu ikawa nzito kwa kuogopa jela.
Lakini,
kikubwa ni kuwa watu wa kanda hii walikuwa wamoja katika kumuunga mkono
Mwamwindi. Shida kubwa ilikuwa kwenye uUtekelezaji wa Azimio la Arusha.
Utekelezaji ule kwa mtazamo wangu ulifanywa kimakosa katika maeneo mengi ya
nchi ikiwamo kanda yetu hii. Wananchi hawakuulizwa wanataka nini.
Walilazimishwa tu na viongozi.
Nakumbuka
kule Ilembula kuna wanafunzi waliolazimishwa baada ya masomo waende wakapande
miche ya kahawa kwenye shamba la kijiji. Wazazi hawakupenda kilimo cha kahawa,
lakini, Serikali ilitaka walime kahawa. Basi, ikatokea, kwa wazazi kuwaambia
watoto wao, kuwa wakifika shambani waigeuze miche ya kahawa. Wapande juu chini.
Hivyo hawakupanda, walipandua,” anasema Mzee Hongole.
Mzee
Hongole anaendelea kusema; “Unajua ni mazingira kama hayo ndio yaliyochangia
uzalishaji upungue. Wananchi walijisikia kushurutishwa. Hawakufanya kazi kwa
moyo. Na vyombo vya habari navyo havikuwa huru kuweza kuelezea hali halisi za
wananchi. Hapa utaona jinsi tulivyokuwa, kama taifa, tukitoka kwenye reli.
Maggid, nawaonea wivu sana katika wakati wenu huu kama wanahabari.
“Sisi
tulisomea taaluma hii. Tena mimi nilipelekwa na Kanisa mpaka Sweden. Lakini,
taaluma zetu zikaishia kufanya kazi ya kusifia Serikali tu, hata kwa mambo ya
kipuuzi yaliyofanywa na baadhi ya viongozi. Wakati huo wa tukio la Mwamwindi
watu wengi walikuwa na hamu ya kutaka kuujua ukweli. Lakini, sisi wanahabari
tuliogopa hata kufika kijijini kwa Mwamwindi kuwahoji waliokuwepo siku ya
tukio”
Mzee
Hongole anasisitiza kwa kusema kuwa wakati umefika kwa Watanzania kuipitia upya
historia yao. Hii itasaidia kuwafanya vijana wa kizazi hiki kujitambua.
Watajenga mioyo ya uzalendo na kuwa tayari kuipigania nchi yao.
“Mimi
nina shaka kuwa vijana wa siku hizi wamekosa kujiamini kwa vile hawajitambui.
Hawaijui historia yao. Wana kiu ya kutaka kuifahamu historia yao. Ni kazi yenu
nyinyi waandishi vijana kufanya tafiti juu ya historia yetu na kuisimulia,”
anasema Mzee Augustino Hongole. . Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi, Amen.
UKIMWONA
kwenye mitaa ya Iringa bado anatembea kwa hatua za kijeshi. Ni Mzee David
Butinini. Alipata kuwa askari polisi na alishuhudia kwa macho yake, siku
Mkulima Said Mwamwindi alipofika kituo cha Polisi Iringa akiwa na mwili wa
marehemu Dk. Kleruu kwenye gari aliloendesha.
Dk.
Kleruu alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliyeuawa na Mwamwindi kwa kupigwa
risasi. Mzee David Butinini alikuwa pia mmoja wa mashahidi kwenye kesi ya
mauaji iliyomkabili marehemu Mwamwindi.
Mzee
David Butinini ni rafiki yangu wa muda mrefu. Jioni ya Jumapili moja tunakutana
Soko Kuu Iringa. Namuuliza juu ya kumbukumbu zake ya kilichotokea miaka 40
iliyopita.
Tunazungumza
huku kwa pamoja tukikiangalia kituo cha polisi kilicho mbele yetu na ambapo
Mzee David Polisi alifanya kazi kama Polisi miaka 40 iliyopita.
“Unasikia
Maggid, nilishuhudia kwa macho yangu. Nilikuwa bado kijana enzi hizo. Nilikuwa
mwanamichezo pia. Nilikuwa kwenye kikosi cha polisi cha mpira wa miguu.
Nakumbuka ilikuwa jioni ya Jumapili ya Krismasi . Ni kwenye saa kumi na moja
hivi.
Tulikuwa
kama askari watatu hivi tumevalia kiraia na tulisimama pale nje ya kituo,” Mzee
David ananieleza huku akionionyesha kwa mkono mahali hapo.
Kelele
za makuli wabeba mizigo sokoni zinatufanya mimi na Mzee Butinini tusisikilazane
vema. Wote, kutokana na utamu wa simulizi hii tunajikuta tunasogea mbele kidogo
na kusimama kando ya kibanda cha rafiki yangu Mwarami. Kijana anayeuza matunda
Soko Kuu la Iringa.
“Unajua
Maggid, Iringa ya wakati huo ilikuwa na watu wachache sana hapa katikati ya
mji. Na magari nayo yalikuwa ya kuhesabika. Na Jumapili ile ya Krismasi ilikuwa
tulivu kupita kiasi. Ghafla tukasikia muungurumo wa motokaa kama tulivyokuwa
tukiyaita magari enzi hizo.
“Mita
mia tano mbele yetu tukaliona gari likitokea kwenye mtaa huu tuliosimama. Ni
Mtaa wa Jamatini wengine wanauita Uhindini. Na kama ilivyo sasa, na enzi hizo pia
barabara hii ni one way. Gari zinakwenda njia moja tu.
Zinashuka
kusini, hazipandi kaskazini.
Je,
ni wakati gani mlibaini kuwa ni gari la mkuu wa mkoa? Namwuliza Mzee Butinini.
“Kwanza
kama askari tukabaki tukijiuliza; kwa nini dereva wa gari linalokuja anavunja
taratibu za barabarani? Lakini, gari lilipokaribia tukabaini haraka kuwa ni
Peugeot 404 rangi ya buluu. Ni gari la mkuu wa mkoa. Na pembeni lilikuwa na
maandishi ’ RC-Iringa’. Sikumbuki namba za usajili wa gari lile. Tukahisi kuwa
mkuu wa mkoa amekuwa na dharura iliyomfanya avunje taratibu za barabarani,”
anasema Mzee Butinini anayeonekana kuwa na kumbukumbu nzuri ya tukio kana
kwamba lilitokea juzi tu.
Unasema
mlihisi mkuu wa mkoa alikuwa na dharura fulani. Je, gari lilikuwa likiendeshwa
kwa mwendo gani na dereva wa gari alifunga wapi breki ya kwanza? Mbele ya
kituo? Nyuma ya kituo au kando ya kituo? Namuuliza Mzee Butinini.
“Kwa
kweli hata mwendo haukuwa wa kasi sana. Ni wa kawaida tu. Dereva alipunguza
mwendo baada ya kupita kituo cha polisi. Akakata kulia na kufunga breki kando
ya kituo pale kwenye ule mnara wa kumbukumbu ya askari waliopigana Vita Kuu ya
Dunia,” anajibu.
Nini
kikatokea? Namuuliza tena Mzee Butinini ambaye wakati huo alikuwa askari kijana
sana.
“Tukamuona
mtu ambaye hakuwa mkuu wa mkoa akifungua mlango na kuelekea mlango wa mapokezi.
Alikuwa mtu mrefu, mnene kiasi na nakumbuka alikuwa na sharubu kiasi.”
Namkatisha
Mzee Butinini kwa kumwuliza; kwa vile mlifahamu kuwa gari lilikuwa la mkuu wa
mkoa na dereva hakuwa mkuu wa mkoa wala dereva wake, hamkuona kuwa ni jambo la
kushangaza? Mlichukua hatua gani kabla dereva huyo hajafika ‘kaunta’ ya
mapokezi pale polisi?
“Bwana
Maggid, kila kitu kilikuwa cha kushangaza na kilikwenda haraka sana. Maana,
yule Bwana Mwamwindi alikwenda moja kwa moja kaunta na pale alikutana na afande
Mbete, nakumbuka alikuwa kijana wa Zanzibar. Mara tukamwona akitoka tena na
kurudi kwenye gari. Akachukua bunduki na kuja nayo tena kaunta ya polisi.
Alikwenda ‘kuisarenda’ kwa maana ya kuikabidhi,” anasema Mzee Butinini.
Je,
nyinyi askari mliokuwa nje mlibaki hapo hapo na umesema mlivaa kiraia. Je,
mlikuwa makachero?
“Kazi
ya uaskari ni kazi ya ukachero pia, lakini kwamba tulivaa kiraia siku ile ni
kwa vile ilikuwa Jumapili na tena siku ya Krisimas. Na kwa kweli hatukuwa na pa
kwenda. Tulikuwa tukijiandaa kusafiri kwenda Moshi kesho yake. Nilikuwa kwenye
kikosi cha mpira na tulikuwa na mashindano ya polisi kule Moshi.
Kwa
sisi askari vijana kituo cha polisi ilikuwa ni kama kijiwe pia cha kukutania na
kupiga stori tukiwa nje. Si unaona hata sasa hivi kuna askari vijana pale
kituoni wamevalia kiraia wanapiga gumzo. Na sisi ilikuwa hivyo hivyo enzi
zetu,” anasema Mzee Butinini huku akinionyesha askari wale vijana nje ya Kituo
cha Polisi Iringa, siku ile ya Jumapili jioni.
Namrudisha
tena Mzee Butunini kwenye reli ya mazungumzo kwa kumkumbushia swali langu; Je,
mlifanya nini baada ya kumwona Mwamwindi akiwapita na bunduki kwenda kukabidhi
kituoni?
“Ahaa!
Tuliingiwa na shauku ya kipolisi ya kutaka kwenda kuichunguza gari ya mkuu wa
mkoa. Nakumbuka wakati Mwamwindi akiandikisha maelezo yake tuliizunguka gari
ile ya mkuu wa mkoa kugagua kilicho ndani.
“Mimi
nilikuwa wa kwanza kumtambua Mkuu wa Mkoa, Dk. Kleruu aliyekuwa amelazwa kiti
cha nyuma akiwa amevalia overall nyeusi na miwani machoni. Nikasema
jamani huyu ni RC Kleruu!” Mzee David anaelezea picha yake ya kwanza ya kifo
cha Dk. Kleruu. Namwuliza ni kipi kikatokea baada ya hapo.
Anajibu;
“Kwa kweli mambo yalikwenda haraka sana. Nakumbuka kulikuwa na pilikapilika
nyingi pale kituoni. Mimi nilikuwa mtaalamu wa chumba cha mawasiliano tukiita signals.
Taarifa zilianza kusambazwa kupitia chumba cha signals nilikofanyia
kazi.
Ilikuwa
mshikemshike. Tarumbeta la polisi likapulizwa. Askari wakakusanyika.
Tukatangaziwa rasmi kifo cha mkuu wa mkoa. Kuna askari waliotumwa hospitalini
kwenda kuchukua kitanda cha magurudumu cha kumlaza Dk. Kleruu na kumpeleka
kumuhifadhi chumba cha maiti.
“Gari
la mkuu wa mkoa likazungushwa na kuingizwa uani kwenye kituo cha polisi.
Wanamichezo
tuliokuwa tukijiandaa na safari ya Moshi kesho yake tukaambiwa tuendelee na
mipango ya safari. Tuliondoka asubuhi yake na basi la Relwe.
“Nyuma
yetu tuliacha vumbi kubwa. Msako mkali wa kipolisi ulianza usiku ule ule wa
kuamkia safari yetu ya Moshi. Iringa ilitikisika na ikaendelea kutisikika kwa
wiki kadhaa.
“Kuna
jamaa wa mjini na ambao walikuwa ni wakulima na walimchukia sana Dk. Kleruu.
Baadhi nawakumbuka kwa majina. Jamaa hawa walipopata habari ya kifo cha Dk.
Kleruu, basi, mmoja wao alinunua kreti za bia na kuanza kunywa na wenzake
kusheherekea. Kati ya watu wa kwanza kunaswa kwenye msako wa kipolisi ni jamaa
hawa.
Maswali
kwa askari huyo wa zamani yanaendelea, namuuliza; Je, Dk. Kleruu alikuwa ni mtu
wa namna gani?
“Bwana
Maggid, na kwa bahati nilimfahamu sana Dk. Kleruu, maana kabla ya kuhamishiwa
Iringa alitokea Mtwara. Na mimi nilifanya kazi Polisi Mtwara wakati Kleruu
akiwa Mkuu wa Mkoa. Naweza kusema namfahamu Dk. Kleruu. Na ninayo ya kumwelezea
hata sasa. ”
NIPO
katika mgahawa wa Neema Craft mjini Iringa. Mzee David Butinini na mimi
tumepanga tukutane mahali hapa kwa chakula cha mchana na mazungumzo kuhusu
alichokishuhudia miaka 40 iliyopita. Inahusu tukio la mkulima Said Mwamwindi
kumpiga risasi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu.
Zikiwa
zimebaki dakika mbili kabla ya kutimu saa saba mchana tuliyoahidiana, namwona
Mzee Butinini akipandisha ngazi za mgahawa. Pamoja na umri wake mkubwa, Mzee
Butinini bado anaonekana kuwa na mwili wa kimichezo pia.
Kwa
wasiomjua, kwenye miaka ya sitini na wakati akiwa kwenye Jeshi la Polisi, Mzee
Butinini alipata pia kuchezea klabu ya soka ya Ushirika ya Mwanza wakati huo
ikiitwa Mwanza-Coop. Huyu ndiye baba pia wa wanamichezo mahiri; marehemu Duncan
Butinini kwenye soka na Jane Butinini kwenye mpira wa pete.
Namuuliza
Mzee Butinini; “Dk. Kleruu alipata kuwatamkia watu wa Iringa, kuwa kama
hawamjui wawaulize watu wa Mtwara. Na wewe unasema ulikuwa naye Mtwara kabla
hajahamishimiwa Iringa, je, Dk. Kleruu unayemfahamu wewe ni mtu wa namna gani?
“Sikumfahamu
Dk. Kleruu kama rafiki, nilikuwa namwona zaidi kikazi. Kikazi nilianzia Masasi,
Mtwara. Na nakumbuka akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk. Kleruu alifika Masasi na
kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara. Nilikutana naye pia wilayani
Newala. Ni kweli, hata kule Mtwara Dk. Kleruu alionekana kuwa ni kiongozi mkali
na mwenye kuhimiza mambo kwa nguvu.
Lakini
pia ieleweke hapa, kuwa maeneo kama Newala na sehemu nyingine za Mtwara
yalikuwa ni maeneo ya Vita. Itakumbukwa tulikuwa kwenye kuwasaidia ndugu zetu
wa Msumbiji hususan Frelimo kwenye mapambano yao ya ukombozi kutoka kwenye
utawala wa Wareno. Sasa labda hali kule Mtwara ilikuwa ni tofauti na ilimtaka
mtu kama Dk. Kleruu,” anasema Mzee Butinini.
Na
umesema kuwa Kleruu alipohamishiwa Iringa nawe ukahamishiwa Iringa pia. Je, Dk.
Kleruu uliyemwona Mtwara alikuwa na tofauti gani na Dk. Kleruu uliyekutana naye
Iringa?
Niliripoti
Iringa mwezi Machi. Nami nilikuwa mgeni pia na mkoa huu wa Iringa. Nilikuwa
askari kijana sana pia. Kule Mtwara Dk. Kleruu alikuwa zaidi kwenye kuhimiza
wananchi kwenye masuala ya maendeleo lakini zaidi kwenye hali ya kijeshi
ikiwamo mambo ya kuchimba mahandaki kutokana na hali niliyoielezea hapo.
Na
watu wa Mtwara walikuwa katika hali duni sana kimaendeleo. Mtwara Dk. Kleruu
hakukumbana na upinzani katika kutoa amri zake.
Sasa
nadhani hapa Iringa Dk. Kleruu alikutana na hali tofauti. Kwa mawazo yangu
nadhani Dk. Kleruu kama Mkuu wa Mkoa alipaswa kujiandaa na zaidi kujifunza juu
ya mila na desturi za watu wa Iringa. Maana, watu wa Iringa ni watu wa Iringa.
Dk.
Kleruu alikuwa kijana mdogo sana kwenye macho ya wazee wa mji huu wa Iringa. Na
mji huu wa Iringa ulikuwa na kundi dogo la wakulima wazawa waliokuwa na kipato
kikubwa. Ndio waliokuwa wakiijenga Iringa. Hawa hawakuwa wakulima wadogo
wadogo. Walikuwa wanamiliki mashamba makubwa sana. Walikuwa wanamiliki magari,
malori na matrekta ya kulimia. Mmoja wa wakulima hao ndiye huyu mkulima Said
Mwamwindi.
Namuuliza
tena; Mzee Butinini, umeaniambia huko nyuma kuwa mara baada ya kupigwa risasi
na kuawa kwa Dk. Kleruu kuna wakulima hapa mjini Iringa waliokamatwa na kutiwa
nguvuni. Je, inakuwaje wakulima waishi mjini?
Anajibu;
Unajua Maggid, Iringa ilikuwa tofauti sana. Wakulima wakubwa wa Iringa walikuwa
na mashamba yao pale Isimani. Ni umbali wa kilomita arobaini hivi kutoka hapa.
Sasa kule shamba walijenga nyumba za kufikia tu wakati wa msimu. Lakini makazi
yao haswa ya kudumu ilikuwa hapa mjini.
Kuna
wakulima waliokwenda shamba asubuhi na usafiri wao na jioni walirudi Iringa
Mjini. Na kuna ambao mjini hapa walikuwa wamewekeza kwenye shughuli nyingine.
Hawa watu walikuwa matajiri hata kwa kiwango cha wakati ule. Walikuwa ni watu
wenye ushawishi pia. Walisikilizwa na watu, waliheshimiwa.”
Namuuliza
swali hili Mzee Butinini; Mmoja wa wazee nilioongea nao kwa simu na natarajia
nitakutana nae kwa mazungumzo ya ana kwa ana ni mkulima Mzee Pesambili na
ambaye alikuwa rafiki wa Said Mwamwindi. Huyu bwana ni mmoja kati ya wale
waliokamatwa na kuwekwa kizuizini. Je, unafikiri ataniambia nini kuhusu
kilichotokea?
Mzee
Pesambili is still bitter! Unasikia, huyu bwana ana machungu sana. Na nadhani
huenda atafurahi kuongea nawe ili aseme machungu yake. Na wakati nakuja kukutana
na wewe, nimemwona anatembea kwa miguu pale Stendi ya Daladala ya Miyomboni.
Amevalia pama lake. Hatukusalimiana. Ukiongea nae ujue, kuwa utakutana na mtu
mwenye machungu ya yaliyomkuta.
Maana,
usiku ule wa tukio aliposikia polisi tunamfuatilia alikimbia makazi yake.
Akaenda kukamatiwa Mufindi huko. Na baadae akapelekwa kusikojulikana. Aliporudi
akakikuta kiwanja chake pale Kihesa kimechukuliwa. Kimsingi maisha yake
yakaharibika. Ari na moyo wa kuendelea na kilimo ikamwishia. Na mifano mingine
ya watu kama mkulima Pesambili.
Wakati
wa sakata lile, watu waliokuwa wakikamatwa walikuwa wakisafirishwa usiku na
ndege ya jeshi. Huko walikokwenda walitawanywa. Hawakukutana. Na huku nyuma
mambo yakazidi kuwa mabaya. Unajua Maggid, unapomkamata mzee mwenye mji wake.
Kisha akapelekwa mahali ambako ndugu zake hawajui, basi, unawaweka wana ukoo
katika hali ya mashaka. Na pengine jamii ambayo mtu huyo aliishi. Tunajua kuwa
kuna wenyeji ambao walipinga kilichokuwa kinafanyika. Lakini hofu ilitawala.
Na
siku zote, watu ni watu. Hata wakikaa kimya, wanasema katika kimya hicho.
Nakumbuka wakati wa operesheni ile kulikuwa na vituo vya usalama kwenye maeneo
ya vijijini. Mimi nilipangiwa eneo la Igula. Kwenye vilabu vya pombe wenyeji
waliimba kwa mafumbo na kwa lugha yao, nyimbo za kushutumu dola. Lakini, huwezi
kumfungulia mshtaka mtu kwa kuimba nyimbo ya mafumbo!
Nikuulize
Mzee Butinini; Fikiri kama tukio lile lisingetokea siku ile ya Jumapili ya
Desemba 25, 1971, je, Iringa leo ingekuwaje?
Iringa
ingekuwa imeendelea sana, lakini hili lingetegemea pia na sera za nchi. Maana,
tatizo lingebaki kama sera zingebaki kuwa zile zile. Ukumbuke kuwa Dk. Kleruu
alikuwa anaamini anatekeleza sera za Azimio la Arusha za Ujamaa na Kujitegemea.
Kwamba kumfuata mtu shambani kwake, tena siku ya Krismasi, kwa Dk. Kleruu
aliamini hiyo ni sehemu ya kazi yake ya kuhimiza kilimo. Ingawa, bado ni
kitendawili, kwa nini afanye hivyo siku ya Krismasi?
Na
nadhani ugomvi mkubwa kati ya Dk. Kleruu na wakulima wakubwa wa Iringa ulikuwa
kwenye sera ya kuchangia mashamba. Haya mambo ya mashamba ya ushirika. Dk.
Kleruu alishindwa kwenye right approach kwa maana ya msogeleo sahihi kwa
wenyeji katika kuifanya kazi yake.
Sasa
basi, hata kama Mwamwindi asingefanya tendo lile baya la kuua, bado, mazingira
ya wakati ule yangefanya kuwepo na mgongano mkubwa kati ya wakulima wakubwa na
watawala. Na hili kwa kweli lilijitokeza mahali pengi hapa nchini.”
Mzee
Butinini alinijibu; Mzee Pesambili is still bitter!
Unasikia, huyu bwana ana machungu sana. Na nadhani huenda atafurahi kuongea
nawe ili aseme machungu yake. Na wakati nakuja kukutana na wewe, nimemwona
anatembea kwa miguu pale Stendi ya Daladala ya Miyomboni. Amevalia pama lake.
Hatukusalimiana. Ukiongea nae ujue kuwa utakutana na mtu mwenye machungu ya
yaliyomkuta.
Maana,
usiku ule wa tukio aliposikia polisi tunamfuatilia alikimbia makazi yake.
Akaenda kukamatiwa Mufindi huko. Na baadaye akapelekwa kusikojulikana.
Aliporudi akakikuta kiwanja chake pale Kihesa kimechukuliwa. Kimsingi maisha
yake yakaharibika. Ari na moyo wa kuendelea na kilimo ikamwishia. Kuna mifano
mingine ya watu kama mkulima Pesambili,” anasema Mzee Butinini.
Taarifa
hizi za kamata kamata kwa baadhi ya wakulima wakubwa bado ziko kwenye
kumbukumbu za baadhi ya wenyeji wa Iringa. Kuna taarifa pia za wenyeji wa
Iringa kuonyesha wazi hisia zao za kuchukukizwa na uongozi wa Dk. Kleruu na
hivyo kuwa tayari kusimama upande wa mkulima Mwamwindi.
Kuna
taarifa za kuwapo kwa wakulima waliochangishana fedha kwa madhumuni ya kukodi
wakili kutoka Uingereza aje kumtetea Mwamwindi kwenye kesi hiyo. Inasemekana
vyombo vya usalama viliinasa orodha ya majina ya waliochangisha fedha na
iliitumia orodha hiyo katika zoezi la kumkamata mmoja baada ya mwingine
miongoni mwa wachangiaji.
Hali
ilikuwa ni ya shaka sana wakati huo. Kuna wakati, wanafunzi wa Chuo cha Ualimu
waliambiwa waandamane kupinga kitendo cha mauaji kilichofanywa na mkulima
Mwamwindi. Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa wanafunzi wa chuo
hicho waliokuwepo wakati huo, mandamano hayo ilibidi wayatawanye wenyewe mara
walipoingia mitaa ya mji wa Iringa, maana, walikutana na sura nyingi za wenyeji
wa Iringa walioonyeshwa kukerwa na kitendo kile cha wanafunzi kuandamana.
”Tulihofia tusije tukapigwa mishale, tukatawanyika wenyewe kurudi chuoni,”
anasema mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho ambacho baadaye kikaja kujulikana kama
Chuo Cha Ualimu Cha Kleruu”.
Hakika,
tukio lile la Mkuu wa Mkoa kupigwa risasi na Mkulima Mwamwindi halikutikisa
Iringa tu, bali nchi nzima. Na kwenye maeneo mengine ya nchi hii watu wa kabila
la Wahehe walihofiwa kwa kudhaniwa ni wenye hulka ya kuua kama Mwamwindi.
Ikafika wakati, nje ya Iringa, mwanamume wa Kihehe akiingia kwenye baa, kuna
wenyeji wa sehemu hizo waliotania kwa kusema; ameingia Mwamwindi.
Na
taarifa juu ya siku ile ya tukio la mauji zimekuwa zikiwachanganya wengi hadi
hii leo. Kupitia mfululizo wa simulizi hizi, zimeanza kujitokeza taarifa mpya zinazotoa
mwanga wa kilichotokea. Mathalan, kuna polisi mstaafu aitwaye Mushi na ambaye
kwa sasa anaishi Moshi akiendesha kampuni ya ulinzi ana haya ya kusema; Bwana
Maggid, mimi nilikuwa kaunta siku ile ya tukio; Jumapili ya Krismasi, Desema
25, 1971. Bwana Butunini uliyeongea naye tulikuwa naye pale polisi Iringa. Siku
ile ya tukio, asubuhi kabisa Dk. Kleruu alifika pale polisi baada ya kutoka kwa
RPC Aboubakar.
Kleruu
na mimi tulikuwa marafiki baada ya kumsaidia kwenye upepelezi wa wizi uliotokea
nyumbani kwake na nikafanikiwa kupata vitu vyake karibu vyote vilivyoibwa
nyumbani kwake. Ulikuwa wizi wa ajabu maana nyumba ya Mkuu wa Mkoa ilikuwa
inalindwa,” anasema Mushi. Kisha anaendelea kusimulia; Tangu hapo tukawa na
uhusiano wa kirafiki na Mkuu wa Mkoa Kleruu. Nakumbuka siku ile ya tukio
alipofika pale kituoni aliniaga kwa kuniambia anaenda Nyang’olo kwenye mambo ya
kilimo. Kisha akanikaribisha jioni hiyo niende nyumbani kwake nikale Krismasi.
Basi, baadaye tukajua kuwa afande RPC Aboubakar alimwambia ampe walinzi wa
kwenda nao, lakini Kleruu alikataa.”
Basi,
jioni ile ndio tukaona gari lake likingiia kituoni. Aliyeliendesha hakuwa Dk.
Kleruu. Mimi ndiye niliyepokea bunduki aliyoikabidhi Mwamwindi. Ilikuwa ya
midomo miwili. Hata gari la Mkuu wa Mkoa ndiye mimi niliyeliendesha
kulizungusha kule uani polisi baada ya mwili wa marehemu kutolewa,” anasema
polisi mstaafu Mushi.
Hakika,
maelezo hayo yanathibitisha kitendawili kigumu juu ya kilichotokea siku hiyo.
Kama ilivyoelezwa huko nyuma na Amani Mwamwindi. Huyu ni mtoto wa mkulima
Mwamwindi. Alisema haya; ” Siku hiyo Kleruu, pamoja na kuwa ni Mkristo, aliamua
kutokula Krismasi. Alivaa kofia yake ya pama. Kleruu akaendesha mwenyewe gari
lake la mkuu wa mkoa aina ya Peugeot Injection, rangi ya bluu. Katika orodha
yake, Kleruu alikuwa na watu watatu wa kuwashughulikia miongoni mwa wakulima
wale wakubwa wa Isimani. Target nambari moja alikuwa Rashid Juma wa
Nyang’olo. Nambari mbili ni marehemu baba. Namba tatu simjui.
Kleruu
alipofika Nyang’olo hakumkuta mkulima Rashid Juma. Siku hiyo ya Krismasi
Rashidi Juma alipata habari, kuwa kuna ng’ombe wake walipotelea milimani.
Alikwenda huko milimani kusaka ng’ombe wake. Hivyo, Kleruu akafunga safari
kurudi kwa target namba mbili, baba yangu Mzee Mwamwindi. Ni njia hiyo
hiyo, Nyang´olo iko mbele ya ilipokuwa ngome ya mzee.”
”Basi,
Kleruu akafika kwa Mzee. Baba akiwa shambani akaliona gari la Kleruu limesimama
nje ya mji wake. Kisha akamwona Kleruu akitembea kumfuata shambani. Baba
alihisi tu, kuwa Kleruu amekuja na shari.
Kleruu
akamuuliza Mzee kwa ukali, ”Mbona mnafanya kazi leo siku ya Krismasi?” Baba
akamwomba Kleruu waende wakazungumze nyumbani. Akamwambia mdogo wangu Mohammed
aendelee kulima. Mzee akatangulia mbele, nyuma anamfuatia Kleruu. Kabla ya
kufika kwenye nyumba yake wakayapita makaburi. Kleruu akamtamkia baba mzee
Mwamwindi; Hapa ndipo unapozika mirija yako?” Alitamka hivyo huku akimtomasa
tomasa mzee na kifimbo alichoshika mkononi.
Jambo
hilo lilizidi kumkasirisha marehemu mzee. Akafika nyumbani kwake. Mlangoni alisimama
mke wake mdogo. Inaonekana mzee alishafanya uamuzi. Jana yake alikwenda
kuwinda. Hakupata mnyama. Bunduki yake moja aina ya riffle kati ya
bunduki zake mbili ilikuwa bado ina risasi. Akamwambia mke wake mdogo huku
Kleruu akiwa anasikia; kanichulie bunduki yangu,” anasema Amani Mwamwindi,
mtoto wa Mkulima Mwamwindi.
Mwanga
zaidi juu ya tukio hili unazidi kupatikana. Lakini, kuna mengine yanayotakiwa
kufanyiwa utafiti ili kubaini ukweli wa kilichotokea. Bila shaka, mahojiano
yangu na mkulima Pesambili na ambaye alikuwa ni rafiki wa mkulima Mwamwindi
yatatupa mwanga mwingine. Na kuna wengine wanaozidi kuchangia katika kutupa
mwanga. Na je, ni nini tafsiri ya hukumu ya kesi ya Mwamwindi.