KUNA
mengi yanayotendwa na viongozi wa Kiafrika yenye kuchafua roho. Kuna ya kuudhi
na kuna ya kukirihisha.
Ni
vitendo vya hao viongozi vyenye kuwafanya baadhi ya Waafrika wavunjike moyo kwa
vile hufikiri kwamba hili bara letu la Afrika halina dawa. Wengine hufika hadi
ya kuamini kwamba labda bara hili limelaaniwa.
Moja
lenye kukirihisha ni kuwaona viongozi wetu wakituibia mali zetu huku
wakijigamba kwamba wao ni wazalendo. Bila ya kupepesa wala kuona haya huku
wanaiba na wakati huohuo wanawalaani wageni kuwa ndio waporaji wa utajiri wa
Afrika, ilhali mara nyingi wao ndio wenye kushirikiana na hao wageni katika
njama ya kuwaghilibu Waafrika wenzao.
Jumatano
iliyopita mahakama moja nchini Zambia ilimhukumu waziri wa zamani wa leba
Austin Liato wa nchi hiyo kifungo cha miaka miwili gerezani na kazi ngumu.
Mwezi Novemba mwaka jana polisi waliyafukua masanduku mawili yaliyokuwa
yamezikwa kwenye shamba lake na juu yake yakawekewa saruji.
Misanduku
hiyo ilijaa fedha taslimu. Mwenyewe Liato hakujuwa kwa uhakika ni kiasi gani
cha fedha alizozistiri chini ya ardhi lakini zilipohesabiwa zilionekana kufikia
kwacha bilioni 2.1 (sawa na dola za Kimarekani milioni 42). Hizo si fedha za
mchezo.
Alipofikishwa
mahakamani na kuulizwa na hakimu alizipataje fedha zote hizo na kwa nini
alizizika chini ya ardhi, Liato alikaa kimya. Hakuwa na la kusema. Bila ya
shaka alikuwa nalo jibu moyoni mwake lakini hakutaka kulitangaza. Alikhiyari
alizike pia hilo jibu. Ndipo hakimu alipoamua kwamba ukimya huo wa Liaoo
ulikuwa na maana kwamba alizipata fedha hizo kwa njia za haramu. Na akampa
adhabu aliyompa.
Tukiyaangalia
magereza katika nchi nyingi za Kiafrika tunaona kwamba yamejaa wezi. Lakini
aghalabu wezi hao huwa ni wezi wa kuku, mbuzi, sidiria au wa vitu vingine
vidogodogo. Ile mijizi yenye kuhatarisha chumi za nchi, yenye kuiba mamilioni
ya dola za Kimarekani ni nadra kutiwa mbaroni. Nao ni viongozi — ama wa
serikali au wa mashirika ya umma.
Nchini
Zambia mambo yanabadilika siku hizi kwa vile serikali mpya ya Rais Michael Sata
imeanza kuwachukulia hatua wakuu wa serikali ya zamani wanaoshtumiwa kwa
ufisadi. Kesi ya Liato ni ya mwanzo tu kati ya kesi tutazozishuhudia siku
zijazo na zitazowahusu na kuwanasa mawaziri na wakuu kadhaa wa serikali
iliyopita ya Rais Rupiah Banda. Sitostaajabu ikiwa karibuni tutaona jela za
Zambia zimejaa wakuu wa serikali ya zamani.
Tayari
serikali ya Sata imekwishaanza kuichunguza mikataba kadhaa ya kibiashara
iliyokubaliwa na serikali ya Banda. Tofauti ya Zambia na Tanzania, ni kwamba
serikali ya Zambia inaonyesha kuwa kweli imejitolea kuufyeka ufisadi na
kuwafanya wahusika na uovu huo wawajibike.
Watu
wengi duniani, si barani Afrika tu, wanajiuliza ilikuwaje hata bara hili lenye
utajiri mkubwa wa mali za asili zikiwa pamoja na maadini, almasi, dhahabu na mafuta
leo liwe bara lenye watu walio masikini kushinda wa sehemu nyingine za dunia?
Si
taabu kulipatia jawabu swali hilo. Sababu kubwa inatokana na viongozi wetu
kutokuwa na ari ya uzalendo. Wangekuwa na uzalendo wasingelithubutu kujiingiza
katika mambo ya rushwa na ya kutaka kujitayarisha wao wenyewe binafsi bila ya
kujali maslahi ya nchi zao na watu wao.
Wangekuwa
wazalendo wasingeliachia bara letu tunalolienzi liwe hivi lilivyo likiwa
limejaa mafukara. Hivi lilivyo bara la Afrika limegeuzwa kuwa yatima. Halina
baba halina mama wa kuliangalia. Mamilioni ya watoto wake wamelikimbia
wakitawanyika sehemu mbalimbali za dunia kujitafutia riziki.
Kama
kweli hawa viongozi wetu wana angalau chembe tu ya uzalendo basi wangekaa na
kuyajadili kwa kina masaibu yanayozidi kulikumba bara letu. Na wangejadili
hatua gani za kuchukua ili nchi zetu ziweze kusonga mbele kwa moyo wa umajumui
wa Kiafrika (Pan-Africanism).
Wasingekuwa
na ajizi kuwachukulia hatua wenzao wenye kusema uongo na wenye kuiba na wote
wale mafisadi wanaozihaulisha fedha za umma kutoka Afrika na kwenda kuziweka
katika akaunti zao kwenye mabenki yaliyo nje ya nchi zao.
Kama
kweli ni wazalendo basi hawa viongozi wetu kila asubuhi wanapoamka wangekuwa
wanataabishwa na hali iliyozagaa ya watu wengi walio masikini kuwa wanaishi
katika bara lenye utajiri mkubwa.
Kwame
Nkrumah, Rais wa mwanzo wa Ghana, hakukosea hata kidogo aliposema kwamba Afrika
“ni kitendawili kinachoudhihirisha ukoloni mamboleo. Ardhi yake ni tajiri
lakini bidhaa zake zitokazo chini na juu ya udongo wake zinaendelea
kuwatajirisha, si Waafrika, bali makundi na watu binafsi wanaoendesha shughuli
zao kwa kuifanya Afrika iwe fukara.”
Matokeo
ya yote hayo ni kwamba takriban nusu ya wakazi wa nchi za Kiafrika zilizo
kusini mwa Jangwa la Sahara wanaishi kwa kasoro ya dola moja ya Kimarekani kwa
siku. Miongoni mwa nchi 48 zilizo maskini duniani 32 ziko katika eneo hilo la
dunia. Kadhalika, kuna asilimia kubwa ya wakazi wa nchi za Afrika ya Magharibi
wanaoishi kwa kasoro ya dola mbili kwa siku.
Tukiziangalia
takwimu nyingine tunaona kwamba ni asilimia 61 tu ya wakazi wa nchi za Afrika
kusini mwa Jangwa la Sahara wenye uwezo wa kujipatia maji safi kulinganishwa na
asilimia zaidi ya 90 ya wakazi wa nchi za Amerika ya Kusini na za visiwa vya
Caribbean, nchi za Afrika ya Kaskazini na sehemu kubwa za bara la Asia.
Isitoshe.
Zaidi ya asilimia 40 ya watu wote duniani wasio na uwezo wa kujipatia maji ya
kunywa wako barani Afrika kusini mwa Sahara.
Tunaambiwa
pia kwamba kufikia mwaka 2030 Waafrika wapatao milioni 650 huenda wakakosa
umeme. Hapo ndipo inapotulazimu kujiuliza kwa nini yale mabwawa ya Inga
yaliyopendekezwa yajengwe kusini magharibi ya Kinshasa yanaendelea kuwa ndoto
tu ilhali Waafrika wachache tu ndio wenye uwezo wa kupata umeme?
Yatapojengwa
mabwawa hayo yatakuwa ndio mradi mkubwa kabisa duniani wa kuzalisha umeme na
utasaidia pakubwa katika kuviendesha viwanda barani Afrika.
Sina
haja ya kutoa takwimu zaidi kuhusu vifo vya watoto wachanga barani Afrika au
hali duni za huduma zetu za afya au za elimu barani Afrika. Sote tunazielewa.
Lakini mzalendo halisi atatutaka tulitafakari hili na tujiulize kwa nini hali
ya mambo ikawa hivyo.
Utajiri
wote wa mafuta na madini umepotelea wapi? Kwa nini mali yote hiyo haikutumiwa
kuwanufaisha wananchi wa bara hili?
Wenye
kukumbuka watakumbuka kwamba mwaka 1960 ulinadiwa kote duniani kuwa ni ‘Mwaka
wa Afrika’. Leo zaidi ya miaka 50 baadaye Afrika haimudu kujilisha yenyewe.
Swali
jingine ambalo tunapaswa tuwe tunajiuliza ni kwa nini Afrika inawasomesha
madaktari ambao baadaye wanakimbilia kwenda kufanya kazi katika mahospitali ya
nchi za Ulaya au Amerika ya Kaskazini?
Mzalendo
halisi Wakiafrika hatochoka kujiuliza maswali. Kati ya hayo ni hili: Ikiwa
kweli, kama alivyosema Marcus Garvey, kwamba Afrika iwe “ya Waafrika walio
nyumbani na ughaibuni” kwa nini basi ikawa leo masuala kuhusu Afrika
yanaamuliwa katika miji mikuu ya nchi za nje? Na hayo ni pamoja na masuala ya
vita na amani, ya uhai na kifo.
Ilikwenda
kwendaje hata ikawa ni NATO na si Afrika iliyoamua kuhusu mustakbali wa Libya
na majaaliwa yake.
Hapa
hatuna budi ila tukubaliane na yale aliyoyasema Julius Nyerere katika hotuba
yake ya mwaka mpya aliyoitoa Januari mosi 1968 alipotamka kwamba: “Hakuna taifa
lenye haki ya kulifanyia maamuzi taifa jingine; hakuna watu wenye haki ya
kuwaamulia watu wengine mambo yao.”
Mzalendo
halisi atapojaribu kuyajibu maswali hayo hatokuwa na budi ila kuwatumbukiza
viongozi wa Kiafrika katika kundi la wenye kulizulia balaa na kila aina ya
matatizo bara letu la Afrika. Ni wao wenye kuzikandamiza haki za wanawake, haki
za wafanyakazi na wenye kuupalilia utawala mbovu.
Ni
wao, kwa uchu wao wa madaraka, wanaopendelea kuselelea madarakani wakijifanya
kama watawala wa kijadi, kama wafalme au machifu, tena wa kurithiwa na watoto
wao au jamaa zao.
Ni
viongozi haohao wanaojidai kwamba ni wazalendo na wanaodai kuwa mpango kama wa
NEPAD ni mpango wa kiuchumi Wakiafrika lakini wanazikimbilia nchi za Magharibi
ziupe baraka zao na ziugharamie.
Mzalendo
halisi anashangaa kuona kwamba barani Afrika hakuna mahakama inayowashtaki
viongozi wa Kiafrika kama akina Hissene Habre, Thomas Lubanga, Laurent Gbagbo
na Charles Taylor na kwamba ni mahakama ya kimataifa ya jinai (ICC) ndiyo
inayowapandisha kizimbani.
Lakini
mzalendo halisi hatoshangaa tu na kujiuliza maswali. Atataka kuchukua hatua.
Kwa mfano, atawataka Waafrika walio barani Afrika na walio ughaibuni waungane
na wawe na ajenda ya kimaendeleo ya kulinyanyua bara la Afrika.
Atajaribu
kuwa na mkakati wa kuwafanya Waafrika walio Uingereza, Ufaransa, Canada,
Brazil, Marekani na kwingineko, waweze kuzishawishi sera za nchi hizo kuhusu
Afrika.
Kila
kipimo tunachokitumia kinatuonyesha kwamba bara letu liko nyuma kimaendeleo;
limejaa magonjwa na maradhi sampuli sampuli, lina umasikini uliokithiri, ukame
na ukosefu wa umeme. Huduma zake za afya na za elimu pamoja na nyingine za
kijamii zote ni duni.
Badala
ya kuwa na hisia za kizalendo viongozi wetu wanakuwa na hisia za kibinafsi.
Hisia hizo ndizo zinazowafanya wapendelee kuwa na mifumo ya utawala
usiowajibika inayowawezesha kupora mali za taifa na kuziponda haki za wananchi
wenzao toka za kiraia hadi za binadamu.
Afrika
ilianza kudidimia kiuchumi na kiutawala pale viongozi wake walipojisahau. Wengi
wao walibabaishwa au labda walilewa madaraka kiasi cha kuwafanya wazione nchi
zao kuwa ni milki zao binafsi. Kwa hivyo walifanya watakavyo.
Waliziminya
haki za wananchi wenzao, waliifanya mikono yao iwe myepesi kuchota kutoka
kwenye hazina za serikali zao, walijinyakulia maekari kwa maekari ya ardhi kwa
faida zao au za jamaa zao na, kwa jumla, walisahau kwamba kuwa na madaraka ni
kuwa na dhamana.
Inafaa
mara kwa mara tuwe tunajikumbusha kwamba katika mwaka 1960 Ghana na Nigeria,
kwa mfano, zilikuwa zimeendelea mbele sana na tajiri kushinda Malaysia ilhali
hii leo hiyo Malaysia imepiga hatua kubwa mbele na kuziacha nyuma hizo nchi za
Kiafrika.
Kujikumbusha
hilo ni muhimu tunapokuwa tunatafakari na kujiuliza kwa nini barani Asia kuna
‘chui wa kiuchumi’ (nchi kama Hong Kong ambayo sasa ni sehemu ya China,
Malaysia, Indonesia, Thailand, Taiwan, Singapore na Korea ya Kusini) wakati
Bara la Afrika likiwa halina ‘simba wa kiuchumi’? Badala yake bara hili lina
‘visungura tu vya kiuchumi’ kwani mara nyingi chumi za nchi nyingi za bara hilo
zinaendeshwa kijanjajanja tu.
Swali
jingine tunalopaswa kujiuliza ni: kwa nini Waafrika wengi wamekufa katika vita
ya wenyewe kwa wenyewe zaidi ya wale waliofariki katika mapambano ya kupigania
uhuru kutoka kwa wakoloni?
Kwa
mujibu wa Anke Hoeffler wa Kituo cha Mtaala wa Chumi za Afrika cha Chuo Kikuu
cha Oxford: “Mnamo 1960 hadi 2002 Waafrika wapatao milioni 1.55 waliuawa katika
vita barani Afrika, takriban asilimia 40 ya jumla ya watu waliofariki vitani
duniani kote. Hivyo bara la Afrika ni eneo lenye idadi kubwa ya watu waliokufa
vitani.”
Je,
Bara la Afrika linaweza kuwa na mwanzo mpya? Baada ya kuanguka hivi
lilivyoanguka Bara la Afrika linaweza kujizoazoa, likainuka na kuanza kupiga
hatua mpya?
Amilcar
Cabral, yule mnadharia wa Cape Verde na shujaa wa mapambano dhidi ya ukoloni,
aliwahi kusema kwamba wazee wetu waliopigania uhuru hawakuwa wakipigania dhana,
“vitu vilivyo kichwani.”
Walipigana
ili wana wa Afrika wapate manufaa, wapate vitu vitavyowawezesha kuishi maisha
yaliyo bora zaidi na kwa amani. “Walipigana ili maisha yao yaendelee mbele na
waweze kuhakikisha kwamba watoto wao watakuwa na mustakbali mwema.”
Viongozi
wetu walipigania uhuru na ukombozi wakiwa na malengo hayo lakini walishindwa
kuyatendea haki malengo yao walipopata madaraka. Walishindwa na walilikhini
bara zima la Afrika. Wakiuzungumzia ‘umoja wa Afrika’ lakini hawakujitolea kwa
dhati kuleta umoja wa kisiasa au wa kiuchumi.
Ushahidi
wa hayo uko wazi. Tunauona kila tunapoziangalia Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa
ya Afrika ya Magharibi (Ecowas), Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Jumuiya ya
Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Muungano
wa kisiasa umewapiga chenga na bado kuna vizingiti vya kibiashara na uhamiaji.
Ndiyo maana hii leo utaona kuwa ni wafanya biashara za magendo na si marais
wetu walio wanaumajumui Wakiafrika kwa sababu wafanya biashara hao hawaitambui
mipaka ya nchi za Kiafrika iliyowekwa na wakoloni.
Je,
itikadi au imani ya umajumui Wakiafrika (Pan-Africanism) ina maana yoyote
katika karne hii ya 21? Jibu langu ni ndiyo, lakini lazima ukombozi wa Bara la
Afrika uwe ndio kitovu au kiini cha juhudi zake. Lazima mapinduzi yarejeshwe
katika ajenda ya Afrika.
Mapinduzi
hayo lakini yawe mapinduzi ya akili, mapinduzi ya namna tunavyojiangalia na
kujiona wenyewe, mapinduzi ya namna ya kubadili jinsi tunavyoyakabili na
kuyatanzua matatizo. Yanayohitajika basi ni mapinduzi ya mtazamo.
Mapinduzi
aina hiyo ni muhimu katika kukipata kizazi kipya cha viongozi, waliojaa shauku
ya moyo wa umajumui Wakiafrika. Bila ya shaka hayo pekee hayatoshi kuzalisha
kizazi kipya cha viongozi walio waadilifu.
Kuna
hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuufanya utawala uwe bora na wenye maadili.
Miongoni mwazo ni kuwawajibisha viongozi watangaze mali zao na itapodhihirika
kwamba mali zao zimeongezeka sana waweze kueleza walizichumaje hizo mali za
ziada. Hatua hiyo itawafanya waogope kupora mali.
Jingine
linaloweza kufanywa ni kuweka vikomo kwenye mihula ya urais. Ikishakubaliwa
kwamba rais hawezi kuwa rais baada ya kipindi fulani basi kanuni hiyo
iheshimiwe na pasiwepo na kijisababu chochote cha kutumiwa kama udhuru wa
kumfanya rais aukiuke mwiko huo.
Hatua
nyingine inayoweza kuchangia pakubwa katika kuustawisha utawala bora ni
kuzitawanya shughuli za serikali na kuzifikisha mikoani na si kuzifanya
zihodhiwe na serikali kuu.
Katiba
mpya ya Kenya, kwa mfano, inalihakikisha hilo ingawa gharama za muundo wake wa
ule inaouita utawala wa ‘kigatuzi’ huenda zikawa kubwa mno.
Pana
haja pia ya jeshi la kijamhuri katika kila nchi ya Kiafrika lisifungamane na
chama chochote kile cha kisiasa.
Kadhalika,
siasa zenyewe ziwe ni siasa zinazojumuisha na si za kuwagawanya. Siasa mithili
ya hizo zitaiwezesha, kwa mfano, serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini
Tanzania iwe na mawaziri kutoka vyama vingine vya kisiasa ilimradi mawaziri hao
wawe na uweledi na sifa za ufarisi na uwezo.
Ili
kuliwezesha Bara la Afrika liweze kujikwamua kutoka kwenye shida lilizo nazo
panahitajika juhudi barani kote za kustawisha mafungamano na kisiasa na
kiuchumi kwanza baina ya nchi za kanda moja na baadaye baina ya nchi za Bara
zima la Afrika.
Afrika
haiwezi kusema kwamba inajitawala yenyewe na inajitendea haki yenyewe huku
ikiwa inategemea taasisi za kisheria na za kutoa haki kama vile ile Mahakama ya
Jinai ya Kimataifa (ICC). Afrika ni lazima iwe na taasisi zake za kisheria
zenye uwezo wa kisheria kama ule wa ICC.
Ni
muhimu pia kwamba pawepo na utamaduni wa uwazi katika shughuli zote za utawala
na za kiuchumi barani kote Afrika.
Hizo
ni baadhi tu ya hatua ambazo zitawezesha kuleta mapinduzi ya fikra barani
Afrika na kuhakikisha kwamba viongozi wa siku zijazo hawatolisaliti bara hili
kama walivyolisaliti viongozi waliowatangulia.
Yaliyowafika
hivi karibuni akina Charles Taylor, rais wa zamani wa Liberia, na Hosni
Mubarak, rais wa zamani wa Misri, ni mafunzo makubwa kwa viongozi wenzao ambao
karibuni tu walikuwa wakinywa nao chai na kukumbatiana nao.
Kuna
wakati Taylor na Mubarak wakiogopwa nchini mwao na hata na wengine walio nje ya
mipaka ya nchi zao. Lakini sasa tunatambua kwamba wote hao, na kuna wengi
wengine kama wao barani Afrika, si chochote ila ‘chui wa karatasi’ chambacho
Mwenyekiti Mao.
Watawala
aina yao ndio waliolifikisha bara la Afrika hapa lilipo. Bara la Afrika
halikuapizwa. Limetumbukizwa katika nakama na viongozi wasiojali maslahi ya
Waafrika wenzao. Viongozi hao wamekuwa wakilaghai, wakidanganya, wakisema uongo
na wakituficha jinsi wanavyoshirikiana na waporaji wakigeni maliasili za
Afrika.
Na
hata ikiwa Bara la Afrika limeapizwa basi zindiko lipo. Nalo ni kizazi kipya
cha viongozi wataotawala kuzifuata kanuni za umajumui Wakiafrika zitazowiana na
mahitaji ya karne ya 21.
Viongozi
aina hiyo nikimnukuu tena Cabral watapaswa: “Wasiwafiche chochote watu wao.
Wasiseme uongo. Wafichue uongo kila wanapoambiwa. Wasiyafiche matatizo, makosa
au kushindwa kwao. Wasidai ushindi wa haraka.”
No comments:
Post a Comment