Tuesday, June 12, 2012

Uzalendo na mbinu za kujikomboa

Ahmed Rajab
KUNA mengi yanayotendwa na viongozi wa Kiafrika yenye kuchafua roho. Kuna ya kuudhi na kuna ya kukirihisha.
Ni vitendo vya hao viongozi vyenye kuwafanya baadhi ya Waafrika wavunjike moyo kwa vile hufikiri kwamba hili bara letu la Afrika halina dawa. Wengine hufika hadi ya kuamini kwamba labda bara hili limelaaniwa.
Moja lenye kukirihisha ni kuwaona viongozi wetu wakituibia mali zetu huku wakijigamba kwamba wao ni wazalendo. Bila ya kupepesa wala kuona haya huku wanaiba na wakati huohuo wanawalaani wageni kuwa ndio waporaji wa utajiri wa Afrika, ilhali mara nyingi wao ndio wenye kushirikiana na hao wageni katika njama ya kuwaghilibu Waafrika wenzao.
Jumatano iliyopita mahakama moja nchini Zambia ilimhukumu waziri wa zamani wa leba Austin Liato wa nchi hiyo kifungo cha miaka miwili gerezani na kazi ngumu. Mwezi Novemba mwaka jana polisi waliyafukua masanduku mawili yaliyokuwa yamezikwa kwenye shamba lake na juu yake yakawekewa saruji.
Misanduku hiyo ilijaa fedha taslimu. Mwenyewe Liato hakujuwa kwa uhakika ni kiasi gani cha fedha alizozistiri chini ya ardhi lakini zilipohesabiwa zilionekana kufikia kwacha bilioni 2.1 (sawa na dola za Kimarekani milioni 42). Hizo si fedha za mchezo.

Alipofikishwa mahakamani na kuulizwa na hakimu alizipataje fedha zote hizo na kwa nini alizizika chini ya ardhi, Liato alikaa kimya. Hakuwa na la kusema. Bila ya shaka alikuwa nalo jibu moyoni mwake lakini hakutaka kulitangaza. Alikhiyari alizike pia hilo jibu. Ndipo hakimu alipoamua kwamba ukimya huo wa Liaoo ulikuwa na maana kwamba alizipata fedha hizo kwa njia za haramu. Na akampa adhabu aliyompa.

Tukiyaangalia magereza katika nchi nyingi za Kiafrika tunaona kwamba yamejaa wezi. Lakini aghalabu wezi hao huwa ni wezi wa kuku, mbuzi, sidiria au wa vitu vingine vidogodogo. Ile mijizi yenye kuhatarisha chumi za nchi, yenye kuiba mamilioni ya dola za Kimarekani ni nadra kutiwa mbaroni. Nao ni viongozi — ama wa serikali au wa mashirika ya umma.
Nchini Zambia mambo yanabadilika siku hizi kwa vile serikali mpya ya Rais Michael Sata imeanza kuwachukulia hatua wakuu wa serikali ya zamani wanaoshtumiwa kwa ufisadi. Kesi ya Liato ni ya mwanzo tu kati ya kesi tutazozishuhudia siku zijazo na zitazowahusu na kuwanasa mawaziri na wakuu kadhaa wa serikali iliyopita ya Rais Rupiah Banda. Sitostaajabu ikiwa karibuni tutaona jela za Zambia zimejaa wakuu wa serikali ya zamani.
Tayari serikali ya Sata imekwishaanza kuichunguza mikataba kadhaa ya kibiashara iliyokubaliwa na serikali ya Banda. Tofauti ya Zambia na Tanzania, ni kwamba serikali ya Zambia inaonyesha kuwa kweli imejitolea kuufyeka ufisadi na kuwafanya wahusika na uovu huo wawajibike.
Watu wengi duniani, si barani Afrika tu, wanajiuliza ilikuwaje hata bara hili lenye utajiri mkubwa wa mali za asili zikiwa pamoja na maadini, almasi, dhahabu na mafuta leo liwe bara lenye watu walio masikini kushinda wa sehemu nyingine za dunia?
Si taabu kulipatia jawabu swali hilo. Sababu kubwa inatokana na viongozi wetu kutokuwa na ari ya uzalendo. Wangekuwa na uzalendo wasingelithubutu kujiingiza katika mambo ya rushwa na ya kutaka kujitayarisha wao wenyewe binafsi bila ya kujali maslahi ya nchi zao na watu wao.
Wangekuwa wazalendo wasingeliachia bara letu tunalolienzi liwe hivi lilivyo likiwa limejaa mafukara. Hivi lilivyo bara la Afrika limegeuzwa kuwa yatima. Halina baba halina mama wa kuliangalia. Mamilioni ya watoto wake wamelikimbia wakitawanyika sehemu mbalimbali za dunia kujitafutia riziki.
Kama kweli hawa viongozi wetu wana angalau chembe tu ya uzalendo basi wangekaa na kuyajadili kwa kina masaibu yanayozidi kulikumba bara letu. Na wangejadili hatua gani za kuchukua ili nchi zetu ziweze kusonga mbele kwa moyo wa umajumui wa Kiafrika (Pan-Africanism).
Wasingekuwa na ajizi kuwachukulia hatua wenzao wenye kusema uongo na wenye kuiba na wote wale mafisadi wanaozihaulisha fedha za umma kutoka Afrika na kwenda kuziweka katika akaunti zao kwenye mabenki yaliyo nje ya nchi zao.
Kama kweli ni wazalendo basi hawa viongozi wetu kila asubuhi wanapoamka wangekuwa wanataabishwa na hali iliyozagaa ya watu wengi walio masikini kuwa wanaishi katika bara lenye utajiri mkubwa.
Kwame Nkrumah, Rais wa mwanzo wa Ghana, hakukosea hata kidogo aliposema kwamba Afrika “ni kitendawili kinachoudhihirisha ukoloni mamboleo. Ardhi yake ni tajiri lakini bidhaa zake zitokazo chini na juu ya udongo wake zinaendelea kuwatajirisha, si Waafrika, bali makundi na watu binafsi wanaoendesha shughuli zao kwa kuifanya Afrika iwe fukara.”
Matokeo ya yote hayo ni kwamba takriban nusu ya wakazi wa nchi za Kiafrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara wanaishi kwa kasoro ya dola moja ya Kimarekani kwa siku. Miongoni mwa nchi 48 zilizo maskini duniani 32 ziko katika eneo hilo la dunia. Kadhalika, kuna asilimia kubwa ya wakazi wa nchi za Afrika ya Magharibi wanaoishi kwa kasoro ya dola mbili kwa siku.
Tukiziangalia takwimu nyingine tunaona kwamba ni asilimia 61 tu ya wakazi wa nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara wenye uwezo wa kujipatia maji safi kulinganishwa na asilimia zaidi ya 90 ya wakazi wa nchi za Amerika ya Kusini na za visiwa vya Caribbean, nchi za Afrika ya Kaskazini na sehemu kubwa za bara la Asia.
Isitoshe. Zaidi ya asilimia 40 ya watu wote duniani wasio na uwezo wa kujipatia maji ya kunywa wako barani Afrika kusini mwa Sahara.
Tunaambiwa pia kwamba kufikia mwaka 2030 Waafrika wapatao milioni 650 huenda wakakosa umeme. Hapo ndipo inapotulazimu kujiuliza kwa nini yale mabwawa ya Inga yaliyopendekezwa yajengwe kusini magharibi ya Kinshasa yanaendelea kuwa ndoto tu ilhali Waafrika wachache tu ndio wenye uwezo wa kupata umeme?
Yatapojengwa mabwawa hayo yatakuwa ndio mradi mkubwa kabisa duniani wa kuzalisha umeme na utasaidia pakubwa katika kuviendesha viwanda barani Afrika.
Sina haja ya kutoa takwimu zaidi kuhusu vifo vya watoto wachanga barani Afrika au hali duni za huduma zetu za afya au za elimu barani Afrika. Sote tunazielewa. Lakini mzalendo halisi atatutaka tulitafakari hili na tujiulize kwa nini hali ya mambo ikawa hivyo.
Utajiri wote wa mafuta na madini umepotelea wapi? Kwa nini mali yote hiyo haikutumiwa kuwanufaisha wananchi wa bara hili?
Wenye kukumbuka watakumbuka kwamba mwaka 1960 ulinadiwa kote duniani kuwa ni ‘Mwaka wa Afrika’. Leo zaidi ya miaka 50 baadaye Afrika haimudu kujilisha yenyewe.
Swali jingine ambalo tunapaswa tuwe tunajiuliza ni kwa nini Afrika inawasomesha madaktari ambao baadaye wanakimbilia kwenda kufanya kazi katika mahospitali ya nchi za Ulaya au Amerika ya Kaskazini?
Mzalendo halisi Wakiafrika hatochoka kujiuliza maswali. Kati ya hayo ni hili: Ikiwa kweli, kama alivyosema Marcus Garvey, kwamba Afrika iwe “ya Waafrika walio nyumbani na ughaibuni” kwa nini basi ikawa leo masuala kuhusu Afrika yanaamuliwa katika miji mikuu ya nchi za nje? Na hayo ni pamoja na masuala ya vita na amani, ya uhai na kifo.
Ilikwenda kwendaje hata ikawa ni NATO na si Afrika iliyoamua kuhusu mustakbali wa Libya na majaaliwa yake.
Hapa hatuna budi ila tukubaliane na yale aliyoyasema Julius Nyerere katika hotuba yake ya mwaka mpya aliyoitoa Januari mosi 1968 alipotamka kwamba: “Hakuna taifa lenye haki ya kulifanyia maamuzi taifa jingine; hakuna watu wenye haki ya kuwaamulia watu wengine mambo yao.”
Mzalendo halisi atapojaribu kuyajibu maswali hayo hatokuwa na budi ila kuwatumbukiza viongozi wa Kiafrika katika kundi la wenye kulizulia balaa na kila aina ya matatizo bara letu la Afrika. Ni wao wenye kuzikandamiza haki za wanawake, haki za wafanyakazi na wenye kuupalilia utawala mbovu.
Ni wao, kwa uchu wao wa madaraka, wanaopendelea kuselelea madarakani wakijifanya kama watawala wa kijadi, kama wafalme au machifu, tena wa kurithiwa na watoto wao au jamaa zao.
Ni viongozi haohao wanaojidai kwamba ni wazalendo na wanaodai kuwa mpango kama wa NEPAD ni mpango wa kiuchumi Wakiafrika lakini wanazikimbilia nchi za Magharibi ziupe baraka zao na ziugharamie.
Mzalendo halisi anashangaa kuona kwamba barani Afrika hakuna mahakama inayowashtaki viongozi wa Kiafrika kama akina Hissene Habre, Thomas Lubanga, Laurent Gbagbo na Charles Taylor na kwamba ni mahakama ya kimataifa ya jinai (ICC) ndiyo inayowapandisha kizimbani.
Lakini mzalendo halisi hatoshangaa tu na kujiuliza maswali. Atataka kuchukua hatua. Kwa mfano, atawataka Waafrika walio barani Afrika na walio ughaibuni waungane na wawe na ajenda ya kimaendeleo ya kulinyanyua bara la Afrika.
Atajaribu kuwa na mkakati wa kuwafanya Waafrika walio Uingereza, Ufaransa, Canada, Brazil, Marekani na kwingineko, waweze kuzishawishi sera za nchi hizo kuhusu Afrika.
Kila kipimo tunachokitumia kinatuonyesha kwamba bara letu liko nyuma kimaendeleo; limejaa magonjwa na maradhi sampuli sampuli, lina umasikini uliokithiri, ukame na ukosefu wa umeme. Huduma zake za afya na za elimu pamoja na nyingine za kijamii zote ni duni.
Badala ya kuwa na hisia za kizalendo viongozi wetu wanakuwa na hisia za kibinafsi. Hisia hizo ndizo zinazowafanya wapendelee kuwa na mifumo ya utawala usiowajibika inayowawezesha kupora mali za taifa na kuziponda haki za wananchi wenzao toka za kiraia hadi za binadamu.
Afrika ilianza kudidimia kiuchumi na kiutawala pale viongozi wake walipojisahau. Wengi wao walibabaishwa au labda walilewa madaraka kiasi cha kuwafanya wazione nchi zao kuwa ni milki zao binafsi. Kwa hivyo walifanya watakavyo.
Waliziminya haki za wananchi wenzao, waliifanya mikono yao iwe myepesi kuchota kutoka kwenye hazina za serikali zao, walijinyakulia maekari kwa maekari ya ardhi kwa faida zao au za jamaa zao na, kwa jumla, walisahau kwamba kuwa na madaraka ni kuwa na dhamana.
Inafaa mara kwa mara tuwe tunajikumbusha kwamba katika mwaka 1960 Ghana na Nigeria, kwa mfano, zilikuwa zimeendelea mbele sana na tajiri kushinda Malaysia ilhali hii leo hiyo Malaysia imepiga hatua kubwa mbele na kuziacha nyuma hizo nchi za Kiafrika.
Kujikumbusha hilo ni muhimu tunapokuwa tunatafakari na kujiuliza kwa nini barani Asia kuna ‘chui wa kiuchumi’ (nchi kama Hong Kong ambayo sasa ni sehemu ya China, Malaysia, Indonesia, Thailand, Taiwan, Singapore na Korea ya Kusini) wakati Bara la Afrika likiwa halina ‘simba wa kiuchumi’? Badala yake bara hili lina ‘visungura tu vya kiuchumi’ kwani mara nyingi chumi za nchi nyingi za bara hilo zinaendeshwa kijanjajanja tu.
Swali jingine tunalopaswa kujiuliza ni: kwa nini Waafrika wengi wamekufa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe zaidi ya wale waliofariki katika mapambano ya kupigania uhuru kutoka kwa wakoloni?
Kwa mujibu wa Anke Hoeffler wa Kituo cha Mtaala wa Chumi za Afrika cha Chuo Kikuu cha Oxford: “Mnamo 1960 hadi 2002 Waafrika wapatao milioni 1.55 waliuawa katika vita barani Afrika, takriban asilimia 40 ya jumla ya watu waliofariki vitani duniani kote. Hivyo bara la Afrika ni eneo lenye idadi kubwa ya watu waliokufa vitani.”
Je, Bara la Afrika linaweza kuwa na mwanzo mpya? Baada ya kuanguka hivi lilivyoanguka Bara la Afrika linaweza kujizoazoa, likainuka na kuanza kupiga hatua mpya?
Amilcar Cabral, yule mnadharia wa Cape Verde na shujaa wa mapambano dhidi ya ukoloni, aliwahi kusema kwamba wazee wetu waliopigania uhuru hawakuwa wakipigania dhana, “vitu vilivyo kichwani.”
Walipigana ili wana wa Afrika wapate manufaa, wapate vitu vitavyowawezesha kuishi maisha yaliyo bora zaidi na kwa amani. “Walipigana ili maisha yao yaendelee mbele na waweze kuhakikisha kwamba watoto wao watakuwa na mustakbali mwema.”
Viongozi wetu walipigania uhuru na ukombozi wakiwa na malengo hayo lakini walishindwa kuyatendea haki malengo yao walipopata madaraka. Walishindwa na walilikhini bara zima la Afrika. Wakiuzungumzia ‘umoja wa Afrika’ lakini hawakujitolea kwa dhati kuleta umoja wa kisiasa au wa kiuchumi.
Ushahidi wa hayo uko wazi. Tunauona kila tunapoziangalia Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika ya Magharibi (Ecowas), Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Muungano wa kisiasa umewapiga chenga na bado kuna vizingiti vya kibiashara na uhamiaji. Ndiyo maana hii leo utaona kuwa ni wafanya biashara za magendo na si marais wetu walio wanaumajumui Wakiafrika kwa sababu wafanya biashara hao hawaitambui mipaka ya nchi za Kiafrika iliyowekwa na wakoloni.
Je, itikadi au imani ya umajumui Wakiafrika (Pan-Africanism) ina maana yoyote katika karne hii ya 21? Jibu langu ni ndiyo, lakini lazima ukombozi wa Bara la Afrika uwe ndio kitovu au kiini cha juhudi zake. Lazima mapinduzi yarejeshwe katika ajenda ya Afrika.
Mapinduzi hayo lakini yawe mapinduzi ya akili, mapinduzi ya namna tunavyojiangalia na kujiona wenyewe, mapinduzi ya namna ya kubadili jinsi tunavyoyakabili na kuyatanzua matatizo. Yanayohitajika basi ni mapinduzi ya mtazamo.
Mapinduzi aina hiyo ni muhimu katika kukipata kizazi kipya cha viongozi, waliojaa shauku ya moyo wa umajumui Wakiafrika. Bila ya shaka hayo pekee hayatoshi kuzalisha kizazi kipya cha viongozi walio waadilifu.
Kuna hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuufanya utawala uwe bora na wenye maadili. Miongoni mwazo ni kuwawajibisha viongozi watangaze mali zao na itapodhihirika kwamba mali zao zimeongezeka sana waweze kueleza walizichumaje hizo mali za ziada. Hatua hiyo itawafanya waogope kupora mali.
Jingine linaloweza kufanywa ni kuweka vikomo kwenye mihula ya urais. Ikishakubaliwa kwamba rais hawezi kuwa rais baada ya kipindi fulani basi kanuni hiyo iheshimiwe na pasiwepo na kijisababu chochote cha kutumiwa kama udhuru wa kumfanya rais aukiuke mwiko huo.
Hatua nyingine inayoweza kuchangia pakubwa katika kuustawisha utawala bora ni kuzitawanya shughuli za serikali na kuzifikisha mikoani na si kuzifanya zihodhiwe na serikali kuu.
Katiba mpya ya Kenya, kwa mfano, inalihakikisha hilo ingawa gharama za muundo wake wa ule inaouita utawala wa ‘kigatuzi’ huenda zikawa kubwa mno.
Pana haja pia ya jeshi la kijamhuri katika kila nchi ya Kiafrika lisifungamane na chama chochote kile cha kisiasa.
Kadhalika, siasa zenyewe ziwe ni siasa zinazojumuisha na si za kuwagawanya. Siasa mithili ya hizo zitaiwezesha, kwa mfano, serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania iwe na mawaziri kutoka vyama vingine vya kisiasa ilimradi mawaziri hao wawe na uweledi na sifa za ufarisi na uwezo.
Ili kuliwezesha Bara la Afrika liweze kujikwamua kutoka kwenye shida lilizo nazo panahitajika juhudi barani kote za kustawisha mafungamano na kisiasa na kiuchumi kwanza baina ya nchi za kanda moja na baadaye baina ya nchi za Bara zima la Afrika.
Afrika haiwezi kusema kwamba inajitawala yenyewe na inajitendea haki yenyewe huku ikiwa inategemea taasisi za kisheria na za kutoa haki kama vile ile Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC). Afrika ni lazima iwe na taasisi zake za kisheria zenye uwezo wa kisheria kama ule wa ICC.
Ni muhimu pia kwamba pawepo na utamaduni wa uwazi katika shughuli zote za utawala na za kiuchumi barani kote Afrika.
Hizo ni baadhi tu ya hatua ambazo zitawezesha kuleta mapinduzi ya fikra barani Afrika na kuhakikisha kwamba viongozi wa siku zijazo hawatolisaliti bara hili kama walivyolisaliti viongozi waliowatangulia.
Yaliyowafika hivi karibuni akina Charles Taylor, rais wa zamani wa Liberia, na Hosni Mubarak, rais wa zamani wa Misri, ni mafunzo makubwa kwa viongozi wenzao ambao karibuni tu walikuwa wakinywa nao chai na kukumbatiana nao.
Kuna wakati Taylor na Mubarak wakiogopwa nchini mwao na hata na wengine walio nje ya mipaka ya nchi zao. Lakini sasa tunatambua kwamba wote hao, na kuna wengi wengine kama wao barani Afrika, si chochote ila ‘chui wa karatasi’ chambacho Mwenyekiti Mao.
Watawala aina yao ndio waliolifikisha bara la Afrika hapa lilipo. Bara la Afrika halikuapizwa. Limetumbukizwa katika nakama na viongozi wasiojali maslahi ya Waafrika wenzao. Viongozi hao wamekuwa wakilaghai, wakidanganya, wakisema uongo na wakituficha jinsi wanavyoshirikiana na waporaji wakigeni maliasili za Afrika.
Na hata ikiwa Bara la Afrika limeapizwa basi zindiko lipo. Nalo ni kizazi kipya cha viongozi wataotawala kuzifuata kanuni za umajumui Wakiafrika zitazowiana na mahitaji ya karne ya 21.
Viongozi aina hiyo nikimnukuu tena Cabral watapaswa: “Wasiwafiche chochote watu wao. Wasiseme uongo. Wafichue uongo kila wanapoambiwa. Wasiyafiche matatizo, makosa au kushindwa kwao. Wasidai ushindi wa haraka.”

No comments:

Post a Comment