Wednesday, May 23, 2012

Kizazi kipya na wasomi wapya

29 Feb 2012
Mwanafunzi Elifuraha John
jogofefu@yahoo.com
SAUT Tabora
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT)
+255-0769023574
Ndugu Mhariri,
ELIMU ni nyenzo muhimu katika kumkomboa mwanadamu katika nyanja zote za kimaisha. Elimu si tu kuingia darasani na kusoma vitabu bali ni kuwa na upeo mpana wa kuchanganua mambo yanayotokea katika jamii. Elimu makini na sahihi ni lazima imfanye mhitimu kuenzi tamaduni nzuri zilizopo katika jamii inayomzunguka. Msomi ni mtu anayepaswa kuigwa kwa matendo yake yenye hekima katika jamii.
Katika nchi yetu wasomi wengi “hawajisomi” na baadhi yao wamekuwa wakiishi mithili ya wanyama kwa kutotumia elimu yao katika kudadisi mambo. Ni watu wasiofuata na kuheshimu utamaduni wa kitanzania badala yake, wanasujudia utamaduni wa kigeni usiokuwa na manufaa kwa wanajamii. Mimi niko chuo kikuu nina ushahidi na haya ninayoeleza.
Kitambo nilifikiri kwamba elimu ingekuwa silaha nzuri sana kwa Mtanzania kujikomboa kifikra za kiutamaduni, lakini wapi. Elimu ndio imekuwa chombo cha kumfanya msomi kutojitambua kabisa. Leo hii wasomi wengi hasa wa vyuo vikuu baada ya kupata elimu, sasa wamepata nafasi ya kutembea nusu uchi kwa madaha.
Wamepata nafasi ya kuchubua ngozi kwa mikorogo mikali ili kufanana na mzungu, wamepata nafasi ya kuzungumza kwa kubana sauti kama manawali wa Ubelgiji na kuishi kwa utamaduni wa nchi za magharibi. Huyu ndiye msomi wetu wa leo hajitambui, hajithamini na wala hajielewi. Si wote wako hivyo la hasha! Wapo wengine wanaotambua umuhimu wao katika jamii na kujiheshimu kama wasomi.
Niliwahi kuandika makala mbili katika moja ya magazeti nchini Desemba, mwaka 2010, chini ya kichwa cha habari “hawa ndio wasomi wetu wa leo” na “kama huu ni uongo ukweli ni upi” nikijaribu kueleza hisia zangu juu ya mmomonyoko mkubwa wa maadili miongoni mwa wanazuoni wetu, baada ya kupata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu.
Katika hali isiyotarajiwa, baadhi ya wanachuo waliopata kusoma makala zile walinishambulia kwa matusi na kunikejeli kwa madai ya kupotosha umma na kujenga mitazamo hasi dhidi ya wasomi wetu. Nilifikiri kuwa nimekosea lakini leo hii nimejiridhisha kwa uchunguzi niliofanya na kukiri kuwa wengi wa wasomi wetu ni chachu ya mmomonyoko wa maadili katika jamii zetu.
Mbali na hapo wengi wao ni wavivu wa kufikiri. Ni wasomi ambao wanapenda kusoma habari nyepesi katika magazeti ya udaku badala ya kutafuta habari muhimu ambazo ni za uhakika. Ni wavivu wa kusoma majarida na vitabu lakini badala yake wamewekeza bidii katika kusikiliza muziki hata kama hakuna ujumbe wa msingi kwao.
Sikatazi kusikiliza muziki bali tujitahidi kupembua na kudadisi mambo ya msingi. Hata mimi napenda kusikiliza muziki pale ninapochoka lakini wengi hatuko hivyo. Waangalie vijana wanaosoma katika taasisi mbalimbali za elimu wengi wao wanawaza kujilimbikizia mali pindi wanapopata nafasi nyeti za kazi au utawala waanze kula mpaka waote vitambi.
Wanawaza kuwa wezi wa mali ya umma na kuwa mafisadi hata kabla hawajapata fursa hizo maridhawa. Sasa wakipata itakuwaje? Kwa nchi kama hii yenye wananchi masikini, kama kila msomi atawaza kujilimbikizia mali kamwe hatutafikia maendeleo. Uzalendo kwa baadhi ya wanazuoni umetoweka kabisa. Maendeleo dhaifu katika nchi yetu ni matokeo ya Watanzania hasa wasomi kutanguliza maslahi yao binafsi kuliko ya jamii kwa ujumla.
Wasomi wengi wamekuwa bingwa wa kushabikia starehe hasa wale wa vyuo vikuu. Ukiyaeleza haya utaonekana adui wa umma. Lakini wale wenye utashi na walio makini watakubali ukweli huu usiopingika. Ndugu mhariri,naomba ieleweke kuwa barua hii haijumlishi wanazuoni wote bali ni wale wenye tabia niliyotaja hapo juu.
Kwa kuhitimisha, nafikiri kuna umuhimu wa kutilia mkazo suala la utamaduni na maadili bora katika ngazi zote za elimu ili kujenga jamii bora yenye maadili na inayowajibika. Hii ni pamoja na kuanzisha somo la maadili ya jamii katika mitaala yetu ya elimu.

No comments:

Post a Comment