Saturday, 31 March 2012 21:27 |
*ATAKA KUONGOZA MIAKA MITANO AWAACHIE VIJANA
Na Sheilla Sezzy, Mwanza MWANASIASA machachari ambaye pia ni Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta ametangaza nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015 na kutamba kuwa ana nafasi nzuri kutokana na sifa alizojijengea ndani ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi(CCM). Sitta alitaja sifa hizo kuwa ni pamoja ile ya kuwa mteule wa rais, kwa awamu zote nne za uongozi taifa, tangu Tanzania ilipotaka uhuru wake, Desemba 9 mwaka 1961. Spika huyo mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , alisema kwa sasa anawasikiliza wananchi kama wataona anafaa na haoni ubaya wowote wa kushika nafasi hiyo ya juu katika uongozi wa taifa kwa miaka mitano tu na kuwaachia vijana waendelee. “Mimi nawasikiliza wananchi kama wataona nafanana na rais wanayemtaka, basi nitachukua maamuzi kwa wakati huo. Sioni ubaya wowote kama wakiniachia kuongoza nchi hii hata kwa miaka mitano halafu niwaachie vijana waendelee,”alisema Sitta. Alisema kuwa ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2014, kila kitu kitakuwa wazi na haweza kukataa majukumu atayopewa na wananchi wake kwani anatambua wanamuamini kwamba ana uwezo wa kuchapa kazi. Sitta ambaye pia ni Mbunge Urambo Mashariki na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa( NEC) ya CCM, aliyasema hayo jana muda mfupi kabla ya kupanda jukwaani kufunga kampeni za udiwani za CCM, Kata ya Kirumba. Mwanasiasa huyo ambaye umaarufu wake umepanda kwa kasi katika miaka ya hivi karubuni kutokana na msimamo wake wa kuongoza mapambano dhidi ya ufisadi ndani ya CCM, alitamba kuwa amefanya mambo mengi ndani ya Serikali ya CCM, ambayo yamesaidia kuleta mageuzi makubwa nchini. Alisema kadri siku zinavyokwenda rais wa Tanzania atajulikana kwa matendo yake na kubainisha kuwa mtu mbaya hawezi kubadilika kuwa mzuri kwa kipindi kifupi. “Sioni sababu ya mtu kuutafuta urais wakati wananchi wanaona na wanajadili kila siku ni rais wa aina gani wanayemuhitaji kutokana na mahitaji yao,”alisema Alisema anachofanya kipindi hiki ni kutimiza wajibu wake na wananchi ni mashahidi kila nafasi anayopewa, anatimiza wajibu wake ipasavyo na kusisitiza kuwa amefanya mengi yanayoonekana machoni pa watu na kudhihirisha kwamba ni kiongozi bora. Akizungumzia umri wa urais, alisema mijadala kuwa vijana hawawezi kuongoza haina msingi. Alifafanua kuwa kiongozi mzuri ni yule mwenye uwezo wa kuwaongoza wananchi na kuwaletea maendeleo. Alisema rais anachaguliwa na wananchi hivyo maamuzi yote ya nani anafaa kwa nafasi hiyo na umri upi, ipo mikononi mwa wananchi wenyewe. Katika hatua nyingine Sitta, aliwashangaa wanasiasa wanaopigana vijembe majukwaani na kueleza kwamba tabia ya kumtukana mtu mmoja mmoja, haina maana yoyote. Aliwashauri viongozi wa CCM kutojibu mapigo ya wapinzani na kuwataka kutumia busara kila wanapokutana na kauli chafu kwani nia ya kudumisha amani ya nchi. Alionya kuwa amani ya nchi ikitoweka, itakayobebeshwa lawama ni CCM na Serikali yake. “Kauli nyingi za majukwaani zinachochea chuki miongoni mwa wananchi, matokeo yake zinaweza kuibua machafuko na waathirika watakuwa wananchi wenyewe, tena wale wasio na uwezo wa kujiokoa,’’ alisema Sitta. Alisema kuwa katika miaka 50 ya utawala wa CCM, kuna mambo mengi yamefanyika na kwamba wapinzani hawana haja kubeza kwani yanaonekana kwa macho. Alisema kuwa katika mafanikio hayo, kuna mengi yamefanywa na Rais Jakaya Kikwete, mfano mzuri ni kampuni tano za madini kulipa kodi na wananchi kuanza kufaidika na rasilimali za nchi yao. Hofu ya mahasimu wake Akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali katika Tamasha Vyombo vya Habari lililofanyika wiki iliyopita kwenye Ukumbi Msasanki Beach, Dar es Salaam, Sitta alieleza kuwa anashangazwa na watu wanaoweweseka wakisikia anataka kuwania urais mwaka 2015. "Nashangaa watu wanapata kiwewe kusikia nataka kuwania urais, kuwania urais ni haki ya kila Mtanzania na Watanzania ndiyo watakaoamua nani ni mzuri na atawafaa," alisema Sitta na kushangiliwa na waliohudhuria tamasha hilo. "2015 tunataka kuwa na mwelekeo mzuri, nikiwa na maana mambo ya hongo, ubadhirifu hatutaki yawe na nafasi, alisema Sitta na kuongeza: Alisema watu wanatumia fedha nyingi kusaka urais na hata wengine kutumia ndumba kwa kwenda Mlingotini, Bagamoyo, kwa nia ya kutaka uongozi na matokeo yake wanaposhinda lengo lao la kwanza linakuwa kurudisha fedha walizotumia. |
Sunday, April 1, 2012
Sitta kugombea Urais 2015
Subscribe to:
Posts (Atom)